26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Azam Fc, Simba ni mtifuano


WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

VIGOGO wa soka la Tanzania, Simba na Azam FC, watashuka dimbani leo kuumana katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia za wapenzi wengi wa soka nchini kutokana na matokeo ya hivi karibuni ya vikosi vyote viwili.

Simba baada ya kutoka kuichapa Al Ahly bao 1-0, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, iliendeleza makali yake katika Ligi Kuu baada ya kuwatandika watani zao Yanga bao 1-0.

Wekundu wa Msimbazi hao, hawakupoa kwani waliendeleza kuvuna pointi tatu kwa kuipiga African Lyon mabao 3-0, mchezo uliochezwa dimba la Sheikh Amri Abeid Karume, Arusha.

Wakati Simba ikigawa vichapo hivyo, Azam imekuwa kwenye wakati mgumu, baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yake mitatu mfululizo ya ugenini.

 Azam FC ilianza kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli FC, Uwanja wa Samora, Iringa, kisha ikakung’utwa bao 1-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa matokeo ya vikosi vyote viwili, ni wazi mchezo wa leo utakuwa wa vuta ni kuvute, kwani Simba itahitaji ushindi ili kuendelea kufukuzia kiti cha uongozi ambacho kwa sasa kinakaliwa na Yanga yenye pointi 61, baada ya kushuka dimbani mara 25, wakishinda 19, sare nne na kupoteza mbili.

Katika msimamo, Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42, baada ya kucheza mechi 17, ikishinda 13, sare tatu na kupoteza moja, Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 50, baada ya kushuka dimbani mara 24, ikishinda 14, sare nane na kupoteza mbili.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Mbelgiji Patrick Aussems, kinaaminika kuwa bora kutokana na aina ya wachezaji walionao hasa wale wa kigeni wanaoendelea kutamba kama vile Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Clautos Chama.

Lakini pia katika timu ya Azam inafundishwa na Mholanzi, Hans van de Pluijm, wapo wachezaji ambao ni tishio ambao wamesumbua kwa muda mrefu katika Ligi Kuu.

Katika mchezo huo Azam inawategemea zaidi washambuliaji wake, Obrey Chirwa, Donald Ngoma, kutokana na kukutana mara nyingi na Simba wakati walipokuwa wanakipiga Yanga.

Licha ya hayo, makocha wote wawili wanaonekana kuwa na mbinu na uzoefu katika kukabiliana na michezo mikubwa na mechi zao zimekuwa hazitabiriki hata kama mmoja wao ametoka kuboronga.

Ikumbukwe timu hizo mara ya mwisho zilikutana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu na Simba kuchapwa mabao 2-1, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika msimu wa Ligi Kuu uliopita, mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu Uwanja wa Azam Complex kabla ya Simba kushinda bao 1-0, Uwanja wa Taifa.

Mchezo wa leo ni mara ya kwanza vikosi hivyo kukutana msimu huu, kutokana na Simba kubanwa na ratiba za michuano ya kimataifa.

Mashabiki wa Simba wanatarajia kuonekana kwa wingi kushuhudia mchezo huo kama walivyofanya katika mechi zilizopita wakiamini kikosi chao kitaendeleza ushindi.

Kwa matokeo ya  Kombe la Mapinduzi, mchezo huo utakuwa wa kulipa kisasi kwa Simba kwa sababu  Azam ndiyo iliyoinyima ubingwa wa michuano hiyo, hali iliyochangiwa na kukosekana kwa nyota wake wa kikosi cha kwanza.

Hivyo basi katika mchezo wa leo, kila mmoja atashusha kikosi kamili, swali ni  je, Azam wataendeleza ubabe? Makocha wa timu zote wanaamini mchezo huo utakuwa mgumu na dakika 90 ndizo zitakazoamua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles