Mohamed Kassara – Dar es Salaam
BAADA ya kuchapwa na Yanga katika mchezo wa watani jadi, kikosi cha Simba leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya Singida United, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba itashuka kuikabili Singida ikiwa na hasira za kutunguliwa bao 1-0 na Yanga, katika mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye uwanja huo.
Wekundu hao wa Msimbazi, licha ya kichapo hicho wanaendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo, wakiwa na pointi 68, baada ya kucheza michezo 27, wakishinda 22, sare mbili na kupoteza mitatu.
Singida wanayokutana nayo, inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20, ikiwa na pointi 12, baada ya kucheza michezo 27, ikishinda miwili, sare sita na kupoteza 19.
Itaikabili Simba ikiwa na mwenendo mbovu kwani katika michezo yake mitano iliyopita imevuna pointi moja pekee.
Simba inajivunjia rekodi nzuri ya kuvuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida, mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 28, mwaka jana Uwanja wa Liti, Singida.
Rekodi za jumla zinaonyesha kuwa tangu Singida irejee Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, haijawahi kupata ushindi mbele ya Simba, katika michezo mitano ambayo timu hizo zimewahi kukutana.
Msimu wa 2017/18, Simba ilivuna pointi zote sita dhidi ya Singida, baada ya kushinda michezo miwili, ikianza kushinda mabao 4-0, mzunguko wa kwanza kabla ya kutakata bao 1-0 mzunguko wa pili.
Msimu uliopita, Simba ilishinda mabao 3-0, mzunguko wa kwanza, kabla ya kutakata mabao 2-0 mzunguko wa pili.
Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ameahidi kurejeshea furaha mashabiki wa timu hiyo iliyopotea, baada ya kipigo cha Yanga.
“Tunaahidi kurudisha furaha miyoni mwenu, “aliandika Kegere katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamiii wa Instagram.
Naye, Kocha Mkuu wa Singida United, Ramadhan Nsanzurwimo alisema wamejiandaa kikamilifu kukabiliana na hasira za Simba, lakini akisisitiza kuwa wao wanahitaji zaidi ushindi, hivyo watapambana kwa jasho na damu kufanikisha hilo.