Na Veronica Simba – TSC
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde amewaagiza Wakurugenzi wa Wilaya kote nchini, kuhakikisha wanawapatia ofisi zenye hadhi, watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika maeneo yao.
Ametoa maagizo hayo leo, Januari 25, 2021 mjini Morogoro wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume.
Naibu Waziri ametoa maagizo hayo baada ya kuelezwa changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume husika, ambapo mojawapo ni ya ukosefu wa ofisi zenye hadhi kwa watumishi wa TSC hususani zilizoko katika baadhi ya Wilaya nchini.
“Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanawapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume, ofisi ambazo zinaendana na hadhi ya utumishi wa umma,” amesema Silinde.
Aidha, ameitaka Tume kuhakikisha inawawezesha Walimu kujitambua na kuelewa sheria, kanuni, taratibu, haki na wajibu wao.
Vilevile, ameipongeza Tume kwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa moyo wa uzalendo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili. Pamoja na kutoa pongezi, ameitaka Tume kuendelea kutoa huduma bora kwa Walimu.
“Sote tunafahamu kuwa tunapotoa huduma bora kwa Mwalimu inamwezesha kutekeleza majukumu yake shuleni kwa ufanisi hatimaye kuinua kiwango cha elimu nchini.”
Naibu Waziri ameihakikishia Tume kuwa ushirikiano uliopo katika utendaji kazi kati ya Tume na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni endelevu.
Aidha, ameongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kusisitiza kila Wilaya kuhakikisha kazi za kushughulikia masuala ya kiutumishi ya Walimu zinatekelezwa kwa ushirikiano ili kuleta tija na ufanisi katika suala zima la kuwahudumia walimu.
Awali, akiwasilisha hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Tume, Profesa Willy Komba alibainisha changamoto kadhaa zinazoikabili, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na jengo la Ofisi za Tume Makao Makuu na Wilaya.
Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya waajiri kutokuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kushughulikia masuala ya kinidhamu ya Walimu.
“Mfano kuchelewa kuwasilisha mashtaka kwa Mamlaka ya Nidhamu, kuchukua jukumu la kutoa adhabu kinyume cha utaratibu na kuwaondoa Walimu kwenye mfumo wa malipo kabla ya mchakato wa mashauri kuanza na kukamilika,” amefafanua Profesa Komba.
Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa pia na Kaimu Katibu wa Tume, Moses Chitama, Menejimenti ya Tume pamoja na wawakilishi mbalimbali kutoka wilaya zote nchini.
Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali, Tanzania Bara.
Naibu Waziri David Silinde ndiye amepewa wajibu wa kusimamia Taasisi hii pamoja na nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.