Mwandishi Wetu-Butiama
JAMII imetakiwa kuondokana na dhana kuwa kila kijana anayejiunga na kupata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) ni lazima apate ajira katika katika majeshi yaliyopo nchini.
Badala yake mafunzo hayo yanatakiwa kutumika katika kutatua changamoto za maisha kwa kijana mmoja mmoja na jamii kwa ujumla hatua ambayo itapelekea kuwa na maisha bora kwa vijana hao na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa wilayani hapa na Mkuu wa JKT nchini, Charles Mbuge wakati akihitimisha mafunzo ya vijana 937 wa kidato cha sita waliojiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria katika kikosi 822 KJ Rwamkoma wilayani Butiama.
Mbuge alisema mafunzo yanayotolewa na jeshi hilo yanalenga kuwajenga vijana katika kujiajiri, kujitambua na kuwa wazalendo kwa Taifa lao na kwamba ni wajibu wa jamii kuhakikisha kuwa wanawasaidia vijana hao kujiajiri badala ya kusuburi ajira kutoka katika majeshi.
Alisema mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji mali pamoja na mengine mengi yanayotolewa na jeshi hilo ni suluhisho juu ya suala la ukosefu wa ajira kwa vijana na kwamba vijana wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo pele wanaporudi omitaani baada ya kuhitimu kutoka katika vikosi mbalimbali nchini.
Alisema Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa katika kufanikisha mafunzo hayo huku lengo kubwa ni kutaka vijana kupata mbinu mbalimbali zenye maadili ambazo wanaweza kuzitumia katika kutatua changamoto za maisha katika jamii na kwamba mafunzo hayo yakitumika vema yatakuwa ni chachu ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.
” Nichukue fursa hii kuishukuru serikali kuendelea kufadhili mafunzo haya na jamii pia inatakiwa itambue kuwa serikali inafanya jambo kubwa na la muhimu sana kwa ustawi wa vijana wetu na taifa letu kwa ujumla kwahiyo badala ya kutaka vijana wapate ajira katika majeshi yetu ni vema tukawapa nafasi watumie mafunzo haya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo katika jamii,” alisema Mbuge
Pia aliitaka jamii kuondoka na dhana kuwa mafunzo yanayotolewa na JKT ni mateso na manyanyaso badala yake jamii ihamasishe vijana waweze kujiunga na mafunzo hayo kwani zaidi na kufundishwa uzalendo lakini pia vijana wanapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kama vile ujasiriamali na uzalishaji mali.
Alisema kuwa mafunzo kwa vijana yanayotolewa na JKT yanalenga kuwasaidia vijana hao kukabiliana na changamoto za kimaisha huku wakiwa wazalendo zaidi na kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika suala zima la ulinzi wa taifa.
Akisoma risala ya wahitimu,mmoja wa wahitimu hao, Mariam Haruna aliliomba jeshi hilo kuongeza muda wa kwa vijana wahitimu wa kidato cha sita kutoka miezi miwili hadi miezi sita kwa maelezo kuwa mafunzo yanayotolewa jeshini hapo ni mazuri lakini muda ni mfupi sana.
Aliishukuru serikali kwa kugharamia mafunzo hayo na kwamba katika kipindi cha mafunzo wamejifunza mambo mengi yenye faida kwao na kwmaba mafunzo hayo yamewafanya kuwa wazalendo zaidi na wenye kujitambua tofauti na ilivyokuwa awali.