NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM
SERIKALI imetumia zaidi ya Sh bilioni 65 kukarabati shule kongwe 60 zilizoko maeneo mbalimbali nchini.
Shule hizo ni kati ya 88 ambazo miundombinu yake ni chakavu, zinazotarajiwa kukarabatiwa hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2019/20.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe, alisema hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2019/20 shule zote 88 zitakuwa zimekarabatiwa.
Sylvia alitembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd kwa lengo la kuelezea shughuli zilizofanywa na Serikali katika wizara hiyo hadi sasa.
“Lengo la Serikali ni kukarabati shule zote kwa asilimia 100 ili zirudi kwenye hadhi yake, tunaboresha mfumo mzima wa utoaji elimu, mwanafunzi asome katika mazingira mazuri na mwalimu afundishe katika mazingira mazuri,” alisema Sylvia.
Alisema ukarabati wa shule hizo umefanywa kwa kutumia wakandarasi na nguvu kazi (Force Account) na kati ya shule hizo wizara imekarabati shule 43 kwa Sh bilioni 46,6 wakati Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imekarabati shule 17 kwa Sh bilioni 19.
Kwa mujibu wa Sylvia, miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa katika shule hizo ni pamoja na madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu, ofisi na mifumo ya majitaka na umeme.
WALIMU
Alisema wakufunzi zaidi ya 700 kutoka vyuo 35 vya ualimu wamepatiwa mafunzo kuboresha ufundishaji wa walimu waweze kuendana na mazingira ya sasa ili watoto waweze kuelewa.
“Unakuta mwalimu amefundishwa kufundisha watoto 40, lakini anakwenda kukutana na watoto 200 darasani, hivyo kunahitajika mbinu za ziada.
“Tutakapomwandaa mkufunzi atakayeweza kumfundisha mwalimu sawasawa, ufundishaji utakuwa bora zaidi,” alisema.
Sylvia alisema kupitia mkakati huo mkazo umewekwa katika masomo magumu kama ya hesabu na lugha na kwamba walimu pia wanafundishwa kutambua vipaji na vipawa mbalimbali walivyonavyo watoto na kuweza kuvikuza.
Alisema ukarabati huo pia unahusisha vyuo vya ualimu na kwamba hadi sasa vingi vimeboreshwa na vingine vimejengwa upya.
Akizungumzia maadili ya walimu, alisema wako kwenye mchakato wa kuunda chombo kipya kitakachosimamia taaluma na maadili ya ualimu.
“Mwalimu aliyepitia mafunzo sawasawa hawezi kufanya kinyume na maadili yake, ndiyo maana akikosea anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Sylvia.
Alisema pia wamewajengea uwezo wadhibiti ubora kwa kuwajengea ofisi na kuwapatia usafiri wa magari na pikipiki, waweze kufuatilia maendeleo ya shule kwa ufanisi.
Sylvia alisema mwaka 2018/19 wametumia Sh bilioni 15.2 kujenga ofisi 100 ambapo wastani wa gharama kwa ofisi moja ni Sh milioni 152 kwa kutumia nguvu kazi.
“Katika mwaka huu wa fedha (2019/20) zitajengwa ofisi 55 na wale wa sekondari tunawapatia magari na waratibu kata tunawapatia pikipiki kufanikisha shughuli zao,” alisema.