24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali yaua watu saba Simanjiro

BEATRICE MOSSES – MANYARA

WATU saba wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa linatoka Kijiji cha Namalulu, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kupinduka.

Akithibitisha kutokea ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga, alisema tukio hilo lilitokea juzi.

Chanzo cha ajali hiyo kimeeleza dereva alishindwa kulimudu kutokana na eneo la Namalulu kuwa na kona nyingi, vumbi na milima hivyo lilikwenda moja kwa moja ndani ya korongo.

“Gari hili lenye namba za usajili T 870 AHG aina ya Mitsubishi Fuso lilikuwa linaendeshwa na mtu aliyejulikana kwa jina  moja la Rashidi, lilikuwa linatoka Arusha kwenda mnadani Simanjiro lilikuwa limebeba bidhaa mbalimbali kwa ajili ya mnada na abiria.

 “Idadi kwa ujumla hatukuweza kupata kwa haraka haraka, lakini lilikuwa na abiria wa kutosha.

“Lilipofika katika maeneo ya Namalulu, Kata ya Naberela, Wilaya ya Simanjiro ni barabara ya vumbi, kona na milima, inaonekana gari ilimshinda dereva kwa sababu inaonekana iliacha njia na kwenda korongoni na kupinduka.

“Watu watano walifariki papo hapo, wengine wawili walifariki wakati wanapatiwa matibabu kituo cha afya cha Orkesment na majeruhi 18 wanaendelea na matibabu.

“Katika majeruhi hao, 7 walikuwa na hali mbaya walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Selian kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Senga.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Leapa Olekaraa (31), Aloyce Temba (32), mkazi wa Arusha, Moses Mgonja (31), mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro, Germana Gerard (36), mkazi wa Arusha na Anna Kileo (46), mkazi wa Sanya Juu, Kilimanjaro.

“Miili ya marehemu imehifadhiwa zahanati ya Orkesment, mpaka asubuhi ya leo (jana), walitambuliwa na ndugu zao ni mili mitatu tu.

“Juhudi za kumpata dereva zinaendelea kwa sababu alitoroka baada ya ajali, nina hakika mpaka jioni atakuwa amepatikana kwa sababu tunamtafuta mmiliki wa gari ambaye tunaamini atatusaidia zaidi.

“Tumekuwa tukisema siku zote magari ya minadani ni ya mizigo sio magari ya abiria, kisheria ni magari yasiyopaswa kubeba abiria kwa usalama wa watu wetu.

“Jiografia ya mkoa wetu ni ngumu kidogo na hasa kwa Wilaya ya Simanjiro ni kubwa takribani ya mara mbili ya Mkoa wa Kilimanjaro, sehemu kubwa ni barabara za vumbi.

“Sehemu hazina makazi ya watu, ni hifadhi za wanyama, barabara za kona na milima kwa hiyo ni hatari,” alisema Kamanda Senga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles