Na MOHAMED MHARIZO-DAR ES SALAAM
MGOMBEA wa nafasi ya urais katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shija Richard, amesema iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, atahakikisha anajenga kituo cha kuendeleza vipaji (academy) mkoani Dodoma.
Mgombea huyo aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa kampeni yake, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa TFF utakaofanyika Jumamosi mjini Dodoma, ambapo alisema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kutambua vipaji ili viendelezwe kwa ajili ya maendeleo ya soka la Tanzania.
“Wanafunzi wenye vipaji vya mpira wanatakiwa kuwekwa kwenye shule maalumu (academy) ili kupata muda wa kutosha kuendeleza vipaji vyao, lakini pia kuwa na miundo mbinu rafiki karibu nao.
“Kama taasisi, tutaweka malengo ya kuwa na vituo hivyo vya michezo katika kanda sita; Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,” alisema Shija.
Alisema katika kipindi cha miaka 20 ijayo, huo utakuwa mkakati wake na kwamba, ataialika Serikali, mashirika ya umma na taasisi za watu binafsi kujenga ‘academy’ hizo kwenye kanda hizo ili kuwa na mfumo uliosambaa kwa usawa nchi nzima katika kuendeleza vipaji.
“Mchezaji wa mpira wa miguu anatakiwa kuandaliwa kuanzia miaka sita, katika umri huo watoto wa Kitanzania wanakuwa shuleni, kunatakiwa kuwepo mpango wa kuwatambua wachezaji wakiwa wadogo, kwa kuwa michezo imerudi shuleni tutaweka mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa walimu wa michezo ili waweze kuwapa wanafunzi mafunzo stahili,” alisema.
Pia alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais wa TFF, atahakikisha anatengeneza fursa, uwezeshaji na furaha kupitia mchezo huo ili wadau waweze kuupenda zaidi kama ilivyokuwa kipindi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo alipokuwa kocha wa Taifa Stars.