Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
MAADHIMISHO ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yamefikia tamati leo Desemba 9, 2021, huku sherehe yake ikifanyika kwa aina tofauti.
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi kutoka nchi mbalimbali, zimefanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam zikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan.
Pamoja na viongozi mbalimbali, Watanzania hasa wakazi wa Dar es Salaam hawakuwa nyuma katika kuhudhuria kilele cha maadhimisho hayo baada ya kujaza Uwanja wa Uhuru na wengine kuamua kwenda kusimama katika pembezoni mwa majukwaa ya Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mageti ya Uwanja wa Uhuru yalifunguliwa tangu saa 11:00 Alfajiri na hadi hufikia saa 3:30 asubuhi majukwaa yote yalikuwa yamejaa, hivyo wasimamizi kuamua kuwaruhusu watu waingie uwanja wa mkapa na kusimama maeneo ambayo watakuwa wanaona kinachoendelea.
Rais Samia ndiye alikuwa wa mwisho kuingia uwanjani hapo saa 4:17 asubuhi ambapo aliingia akiwa katika gari maalum lilipambwa na rangi nyekundu zilizoendana na hijabu yake aliyovaa leo Desemba 9.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, aliwasili uwanjani saa:3:30 asubuhi, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi akiwasili saa 3:25.
Marais wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Uhuru Kenyatta(Kenya) ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, Paul Kagame(Rwanda), Filipe Nyusi(Msumbiji) na Azali Assoumani(Comoro),
Rais wa Burundi aliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombanza, DR Congo amewakilishwa na Waziri Mkuu, Jean-Michel Lukonde.
Marais wastaafu ni Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, Dk. Mohammed Shein, Aman Abeid Karumepia walikuwepo marais wastaafu wa nchi nyingine akiwamo Rais Mstaafu wa Malawi, Joyce Banda, Joaquim Chissano rais mstaafu wa Msumbiji, Mstaafu wa Botswana, Ian Khama
Pia Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Dk. Gharib Bilal, Waziri Mkuu wa zamani Fredrick Sumaye.
Maria Nyerere, Fatma Karume wapamba sherehe
Wake wa waasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Maria Nyerere na Fatma Karume, walikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliopamba sherehe hiyo.
Hakuna hotuba, burudani mwanzo mwisho
Katika sherehe ya mwaka huu imekuwa na utofauti na nyingine kwani hakukuwa na hotuba ndefu zaidi ya salamu kwa Watanzania, hii ni kutokana na Rais Samia kuhutubia siku moja kabla ya sherehe hizo.
Sherehe za mwaka huu zimeonekana kupamwa na maonyesho ya shughuli na kazi zinazofanywa na majeshi hasa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), huku kukiwepo burudani za vikundi mbalimbali.
Katika salamu zake, Rais Samia aliwatambulisha wageni na marais waliohudhuria sherehe hizo, huku akisema kutokana na muda hakutakuwa na mambo mengi zaidi ya wageni hao kusimama kwa pamoja na kusalimia Watanzania.
Aidha amewashukuru Watanzania na watu wote walihusika kufanikisha maadhimisho hayo tangu yalipoanza.
Ni sherehe za mwisho kwa Uhuru Kenyata kuhudhiria kama Rais wa Kenya
Rais Samia amesema Uhuru Kenyata wa Kenya amehudhuria sherehe hizo kama mgeni rasmi lakini pia zitakuwa za mwisho kwake kuwepo kama Rais wa Kenya kwa sababu mchakato wa kugombea urais wa Kenya umeanza, hivyo siku nyingine atakuja akiwa ni mstaafu.
Aidha, Rais Samia amesema rais huyo wa Kenya pamoja na kuhudhuria maadhimisho ya Uhuru, amekuja kwa lengo la kufanya ziara Tanzania.
“Rais Uhuru Kenyata wa Kenya yupo hapa kama mgeni rasmi lakini hatazungumza chochote, tutakuwa naye kesho kwa sababu amekuja pia kwa ziara. Ikumbukwe vuguvugu la urais tayari limeanza nchini Kenya, hivyo siku nyingine tutakuwa naye kama mstaafu,” amesema Rais Samia.
Waziri Mkuu ampongeza Rais Samia
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya hayo, amempongeza Rais Samia kwa hotuba yake aliyoitoa jana Desemba 8, 2021 saa 3: 00 usiku na kusema ilikuwa ni chachu kwa Watanzania katika kuendeleza umoja na mshikamano.