Na Michael Mapollu
-Njombe
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amesema umeme wa uhakika kwa wakulima wa nanasi wa Kijiji cha Madeke wilayani Njombe, kutasaidia kwenye uchakati wa mazao hayo badala ya kuwa yanaozea shambani.
Kutokana na hali hiyo, amesema vijiji vyote vilivyopo kwenye Kata ya Mfriga, ambako wakulima wake wanazalisha kwa wingi matunda ya nanasi sasa watakuwa na umeme wa uhakika.
Akizungumza mjini hapa juzi wakati alipopita kukagua ujenzi wa miundombinu ya umeme wa mradi wa Makambako-Songea pamoja na ule wa REA III, Dk. Kalemani alisema kuna vijiji 7,837 ambavyo bado havijapata umeme kwa nchi nzima, lakini kwa sasa Serikali inaanza na vijiji 3,559 vikiwemo vya Jimbo la Lupembe.
“Mkandarasi anayepeleka umeme katika Mkoa wa Njombe, pia atapeleka umeme Madeke-Lupembe, kwa hiyo huu mradi wa REA unakwenda vijiji vyote na utekelezaji wa REA awamu ya tatu utakamilika mwezi Machi, 2019 kwa hiyo wale wanaolima mananasi nawashauri walime kwa sababu umeme tayari utawafikia.
“Umeme upo, watachakata juisi na wasafirishe juisi badala ya mananasi yenyewe na sasa ndiyo tunaongeza nguvu ya umeme huu, kwa sasa wanapeleka umeme wa kv130, huu mradi wa Makambako-Songea wa kv220 utaingizwa kwenye gridi ya taifa ambayo pia itakwenda kwenye hivyo vijiji vya Lupembe,” alisema Kalemani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, alimweleza Naibu Waziri juu ya kilio cha wakulima wa kijiji hicho kuwa wamekuwa wakiyatupa mananasi kufuatia kuharibika kutokana na kushindwa kupata sehemu ya kuyapeleka, lakini endapo umeme ungekuwepo ungesaidia kuanzisha viwanda vidogo.
“Katika maeneo ya Madeke kumekuwa na kilimo cha matunda ya nanasi na parachichi, ni kweli kuna changamoto ya umeme, mazao yanaharibika huko kwa sababu wakulima wenyewe wanavyo viwanda vidogo vidogo wanatumia jenereta, tukiweza kupeleka umeme kule itaweza kusaidia,” alisema Sendeka.
Akizungumzia suala la wakulima wa nanasi wa Kijiji cha Madeke kuhusu kilio chao cha kuanza kazi kwa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Monica Kyuluhya, alisema changamoto anayoifahamu katika hicho kiwanda ni nishati ya umeme.