25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yasaini mkataba ujenzi wa matenki ya mafuta bandarini

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania (TPA), imesaini na mkataba kwa ajili ya ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta.

Mkataba huo umehusisha muunganiko wa kampuni za M/S China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd. na M/S WUHUAN Engineering Co. Ltd ya China.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini Februari 26,2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, amesema wanatarajia kuwapo kwa uhakika wa mafuta nchini kutokana na ujenzi wa matanki hayo, gati la kupokea na kupakua mafuta pia inaweza kupunguza mfumuko wa bei na kuleta nafuu.

“Hii inatokana na ukweli kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunasababisha kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bidhaa nyingine kwa maana hiyo matanki haya yatakuwa na unafuu kwa wananchi,” amesema Mbossa.

Amesema mradi huo utaondoa tatizo la upotevu wa mafuta katika bandari hiyo na kupunguza malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara wa mafuta na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

“Kwa kuwa mafuta yote yatapokelewa na kupimwa vizuri yakiwa sehemu moja na kuwa chini ya TPA kabla ya kuyasambaza, hali hii itaimarisha udhibiti wa mapato ya serikali kwa kuzuia mianya ya ukwepaji kodi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na bidhaa za mafuta zinazoingia nchini,” ameeleza.

Amesema kuwapo kwa mradi huo kutaimarisha hifadhi ya mafuta na kuondoa changamoto ya sasa ambapo uwezo wa kuhifadhi mafuta nchini ni wa siku 15 kwa kutumia matenki ya kampuni binafsi.

Ameongeza kuwa mradi huo utachochea mashirika yanayoshughulika na mafuta kuanzisha Kituo cha Usambazaji Mafuta (Hub) kwenda nchi za jirani kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo cha soko la biashara ya mafuta.

Mbossa amesema ujenzi huo unakwenda kupunguza gharama za meli kukaa bandarini ambapo zimekuwa zikisubiri kushusha bidhaa hizo takribani siku saba hadi 10, huku meli moja hushusha mafuta kwa siku 10 hadi 12 na gharama za kusubiri ni dola za Kimarekani 25 kwa siku.

Amesema hatua iliyofikia inaenda kuondoa ucheleweshwaji wa upakuaji mafuta pamoja na upotevu wa mafuta zaidi ya asilimia moja ulikuwa ukitokea.

Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameagiza usimamizi na utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia muda wa mkataba na kukamilika kwa wakati ili kuondokana usumbufu usiyo wa lazima.

“Leo Tanzania imeweka historia kwa kusaini mradi huu namna mradi huu ulivyochukua muda zaidi ya miaka 10 hadi kufanikiwa leo,”amesema Profesa Mbarawa.

Akifafanua kuhusu mradi huo amesema yatajengwa matenki yenye mita za ujazo wa 420,000 pamoja na miundombinu yake na kwamba matenki sita yenye uwezo wa mita za ujazo wa 30,000 ni kwa ajili ya dizeli na matenki matano yenye uwezo wa mita za ujazo 30,000 m3 kwa ajili ya petrol.

Amesema pia matenki matatu yenye uwezo wa mita za ujazo 30,000 kwa ajili ya mafuta ya ndege na tanki moja kwa ajili ya huduma za bandarini hapo.

Ameeleza kuwa serikali ina mpango wa kujenga gati ya kupokea meli za mafuta eneo la Kigamboni kurahisisha upokeaji na usambazajii wa huduma hiyo nchini.

Kwa upande wake Mwenyeki wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, ameipongeza juhudi hizo za serikali kutekeleza mradi huo na kuhimiza matumizi sahihi ya fedha za mradi na kumtaka mkandarasi kuzingatia muda wa kukamilisha mradi huo ili kuepuka hasara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles