23.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yapiga marufuku tozo kinyume na sheria kwa wachimbaji wa madini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku Halmashauri zote nchini kutoza tozo kwa wachimbaji wa madini ambazo hazikubaliana na Sheria Mama. Aidha, kliniki ya kutatua changamoto za wachimbaji wa madini imepangwa kuanza Julai 3, 2024, kote nchini.

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, alitoa tangazo hilo leo, Juni 26, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA). Dk. Kiruswa alisema kuwa tozo yoyote inayotozwa katika sekta ya madini lazima iwekwe kulingana na Sheria Mama.

“Ni marufuku kwa halmashauri zote nchini kutoza tozo ambazo ni kinyume na Sheria Mama. Tozo zote lazima ziendane na Sheria Mama ili kuwasaidia wachimbaji wa madini,” alisema Dk. Kiruswa. Aliongeza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameelekeza sheria na wizara zote kuhakikisha zinaendana na kusaidia sekta ya madini.

Dk. Kiruswa pia alitangaza kuanzishwa kwa kliniki ya kusikiliza na kutatua changamoto za wadau wa sekta ya madini kuanzia Julai 3, 2024. Kliniki hii itafanyika kwa kushirikiana na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde. “Tutashughulikia changamoto zote tutakazoweza kutatua papo hapo, na zile za kisheria na kimfumo tutashirikiana na wadau husika,” alisisitiza.

Wizara ya Madini iko katika mchakato wa kufanya marekebisho ya kanuni mbalimbali za sekta ya madini. Katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2024/25, kiasi kikubwa cha bajeti kimeelekezwa kwenye shughuli za utafiti ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija.

“Tafiti zitatusaidia kujua madini tuliyonayo, aina zake, maeneo yalipo, na ubora wake. Hii itasaidia kugawa leseni kwa ufanisi zaidi,” alisema Dk. Kiruswa.

Dk. Kiruswa pia aliagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa ripoti za utafiti kwa umma badala ya kuzifungia kwenye makabati. Aidha, aliahidi ushirikiano wa hali na mali kwa wachimbaji na kuwasihi kuwa vinara wa kufuata sheria na kanuni za madini.

Dkt Kiruswa alitoa wito kwa wachimbaji kuwa mabalozi wa mfano katika kufuata taratibu na kupambana na utoroshaji wa madini. Alisisitiza kuwa utoroshaji wa madini unakosesha taifa mapato muhimu.

Pia, aliagiza Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwa na wawakilishi wa wachimbaji (LEMAS) katika shughuli zao au mikutano.

Kwa upande wake, Rais wa FEMATA, John Bina, aliwataka wachimbaji wadogo kuwa na subira na kuipa muda Serikali kushughulikia changamoto zao. “Sisi kama Shirikisho tunaandaa makongamano na mikutano kwa ajili ya kuishauri Serikali na viongozi wetu,” alisema Bina.

Mkutano wa FEMATA unaendelea sambamba na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji pamoja na kongamano la wachimbaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles