27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Balozi Mussa ampongeza Rais Samia kwa Uteuzi unaozingatia Jinsia

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Dar es Salaam – Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wake unaozingatia jinsia, ambao umepelekea wanawake kuwa asilimia 24 ya wanadiplomasia nchini.

Pongezi hizo zilitolewa Juni 24, 2024, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Katika Diplomasia, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022 na Baraza la Umoja wa Mataifa.

“Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi kwa kuwachagua katika nafasi mbalimbali,” alisema Balozi Mussa.

Aliongeza kuwa, katika maadhimisho hayo walihudhuria wanadiplomasia mashuhuri kama vile Balozi Getrude Mongera, Balozi Amina Salum Alli, na Balozi Riberata Mulamula, pamoja na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alieleza kuwa maadhimisho hayo ni jitihada za serikali zote za Muungano katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi katika nyanja za maamuzi.

“Serikali zote mbili zimetambua umuhimu wa wanawake kwa kuwachagua katika sekta mbalimbali, ikiwemo mawaziri, ambapo sasa kwa Zanzibar wanawake waliopo katika nafasi za maamuzi ni asilimia 33,” alisema Pembe.

Akizungumzia kuhusu uchumi, Pembe alisema serikali zote zimeweka miundombinu ya kuwainua wanawake, ikiwemo kuwapa mikopo isiyokuwa na riba. “Wanawake wamepewa kipaumbele kila sehemu. Kwenye siasa tunae Jemedari wetu Rais Dkt Samia. Kwenye uchumi, elimu, na afya, serikali imeweka mazingira mazuri kuhakikisha mwanamke anapata nafasi,” aliongeza.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma.

Siku ya Wanawake Katika Diplomasia huadhimishwa Juni 24 kila mwaka na ilianzishwa ili kutambua na kuthamini juhudi za wanawake ambao wamejitolea maisha yao katika nyanja za diplomasia na uongozi wa kimataifa. Wanawake wamekuwa na msaada mkubwa katika kujenga madaraja kati ya mataifa, kukuza ushirikiano wa kimataifa, na kutafuta suluhisho la migogoro kwa njia ya amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles