Benjamin Masene -Mwanza
SERIKALI imewaonya wakurugenzi au mamlaka za ajira nchini kuacha mara moja mwenendo wa kuwakubalia watumishi waliojiendeleza kielimu tofauti na taaluma yao waliyoajiriwa awali bila kufuata taratibu za utumishi, huku Mkoa wa Mwanza ukitajwa miongoni mwa mikoa isiyowasilisha kikamilifu taarifa za watumishi wake kwa Tume ya Utumishi wa Umma.
Kauli hiyo hiyo imetolewa juzi na Katibu wa tume hiyo, Nyakimura Muhoji na kusisitizwa zaidi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa wakati wa mkutano wa watendaji wote wa taasisi za umma katika Mkoa wa Mwanza.
Dk. Mwanjelwa ambaye ameambatana na makamishna wa tume ambao ni Balozi mstaafu John Haule, Khadija Mbarak, Alhaji Yahya Mbila na wengine, wapo katika ziara kwa baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kukutana na watumishi wote wa umma kujifunza na kubadilishana uzoefu wa utendaji katika uendeshaji na usimamizi wa masuala ya rasilimali watu katika utumishi wa umma.
Alisema licha ya Serikali kuwa na utaratibu wa kuwaendeleza kielimu watumishi na wengine kujigharamia wenyewe, lakini tatizo lililopo ni watumishi hao kwenda kusoma taaluma nyingine tofauti na ile aliyoajiriwa nayo, na baada ya kurejea kituo chake cha kazi, hutaka kubadilishiwa kitengo na baadhi ya wakurugenzi na mamlaka za ajira hufanya hivyo bila kufuata sheria na taratibu za utumishi.
Dk. Mwanjelwa alisema kitendo hicho kimesababisha kuwapo na shida sana ndani ya tume na baadhi ya watumishi kufuatilia hadi makao makuu.
Aliwataka wakurugenzi na mamlaka za ajira kuwa makini juu ya matumizi ya rasilimali watu.
“Serikali haizuii mtu kujiendeleza kielimu wala kubadili taaluma yake isipokuwa tatizo lipo namna watumishi na waajiri wanapofanya uamuzi bila kuzingatia sheria.
“Sasa hapo kuna suala la mshahara kupanda, cheo na mambo mengine, ndiyo hayo yanapofuatiliwa na kukuta utaratibu haufuatwi, hivyo hayo ni matumizi ya rasilimali watu mabaya, kuanzia sasa sheria zitachukuliwa kwa wahusika,” alisema.
Dk. Mwanjelwa alisema katika ziara hiyo amebaini licha ya watumishi wa umma ni wasomi, lakini bado kuna udhaifu mkubwa katika suala la kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa.
“Baadhi yao hawajitambui na hawajui sheria zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao,” alisema Dk. Mwanjelwa.
Alisema ameshangazwa na watendaji wa umma hawazingatii taratibu za ajira mpya, watumishi wapya kutopewa mafunzo elekezi, kutowathibitisha kazini kwa wakati baada ya kumaliza kipindi cha majaribio, watumishi kutopewa mgawanyo wa majukumu yao.
Dk. Mwanjelwa alisema hali hiyo inasababishwa na watumishi wengi kutojua sheria, kanuni na taratibu zilizopo na hatimaye kukiuka maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa kutowathibitisha kazini mtumishi mpya ni kumnyima haki zake jambo linalosababisha malalamiko yasiyo na tija na kupunguza ari ya utendaji kazi.
“Hili ninalokwenda kulisema linawahusu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Katibu Tawala, hili lenu, naomba mlione namna ya kufanya, katika kipindi cha mwaka 2017/2018 hali ya uwasilishaji wa taarifa tume kutoka taasisi zilizopo chini ya mkoa wenu haziridhishi kabisa,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Katibu Tawala, Christopher Kadio, walisema wataalamu na maofisa utumishi ndio wanaowashauri vibaya na kusababisha hali hiyo kujitokeza na waliahidi kuyafanyia kazi mapunguifu yaliyojitokeza.