23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza kuandaliwa mkutano wa wadau wa sekta ya uvuvi Mara

Mwandishi Wetu -Musoma

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewaagiza makatibu wakuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mkutano wa pamoja utakaohusisha wadau wa sekta ya uvuvi mkoani Mara.

Bashungwa alitoa agizo hilo jana mjini hapa, baada ya kufanya ziara ya siku moja na kukagua viwanda ambavyo vimesimama uzalishaji, kikiwepo kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki cha Prime Catch.

Alisema sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika kufanikisha lengo la Serikali la uchumi wa viwanda, hivyo ni wajibu wa viongozi kuhakikisha wanakutana na wadau wa sekta hiyo ili kujadili na kupata ufumbuzi wa pamoja namna ya kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Bashungwa alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ni namna ya kurudisha viwanda vilivyosimamisha uzalishaji, kuanza kuzalisha kutokana na ukweli kwamba rasilimali samaki ipo ya kutosha.

Alisema lengo la Serikali la uchumi wa viwanda pia linakusudia kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia sekta ya viwanda.

Bashungwa alisema Serikali ina imani kubwa ikikutana na wawekezaji pamoja na wadau wote wa uvuvi, kila upande utajua matatizo yake na hatimaye kupata namna ya kuondokana nayo ili kuondoa vikwazo ambavyo vinazuia sekta hiyo kushiriki kikamilfu katika sera ya Tanzania ya viwanda.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alimwambia waziri huyo kuwa uwepo wa viwanda mkoani Mara ambavyo havifanyi kazi, unasababisha mkoa huo kushindwa kukua kiuchumi kutokana na kukosekana kwa mchango wa viwanda hivyo katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla.

Alisema Manispaa ya Musoma zaidi ya viwanda vitatu hivi sasa havifanyi kazi.

Malima alisema mbali na kuzuia uchumi wa mkoa kukua, lakini pia hali hiyo inasababisha zaidi ya watu 2,000 kukosa ajira na kwamba umefika wakati sasa Serikali kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinaanza kazi kwa masilahi ya wananchi na Tanzania kwa ujumla.

Alisema Serikali ya mkoa imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kuwa inaboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ili uwekezaji uweze kufanyika kwa uhakika.

Alitolea mfano suala la uvuvi haramu ambalo lilisababisha upungufu mkubwa wa samaki ndani ya Ziwa Victoria, hivyo kusababisha viwanda vya samaki kusitisha uzalishaji na kwamba baada ya kuanza kupambana nalo, hivi sasa samaki wameongezeka ziwani.

Alitoa mfano wa kiwanda kimoja cha kusindika samaki ambacho kutokana na uhaba wa samaki kilikuwa kinasindika tani tatu kwa siku, lakini baada ya operesheni endelevu ya kupambana na uvuvi haramu, kwa sasa kinasindika zaidi hadi tani 40 za samaki kwa siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles