31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaja na mkakati mpya soko la korosho

Leonard Mangoha, Dar es salaam

SERIKALI imekuja na mkakati mpya wa ununuzi wa zao la korosho kwa njia ya mnada wa wazi kupitia  mtandao ambao utaanza kutumika katika mwaka wa mavuno 2019/2020.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema uamuzi wa kutumia mfumo huo umetokana na uzoefu walioupata wakati wa ununuzi wa zao hilo msimu uliopita.

Hasunga alisema kutokana na uzoefu walioupata msimu uliopita wameamua katika msimu wa mavuno ya zao hilo wa 2019/202 kuendesha minada ya wazi ambayo ina tofauti kidogo na ile ya siku za nyuma.

Kupitia utaratibu huo alisema kila mwananchi anaweza kushiriki na kuona kinachotokea katika mnada husika na itaendeshwa nchi nzima na duniani kote kupitia mtandao

“Kwa sababu itakuwa inafanyika Tanzania lakini wanunuzi wanaweza kushiriki wakiwa sehemu yoyote duniani…Jambo la pili, tunakuja na utaratibu mpya wa kuhakikisha viwanda vyetu kwanza vinapewa kipaumbele cha kununua malighafi zile zitakazotumika katika kuongeza thamani.

“Kama sote tunavyojua viwanda vyetu kwa muda mrefu vilikuwa vinashindwa kufanya ubanguaji kwa sababu vilikuwa vinashindwa kushindana katika bei, lakini la pili walikuwa hawana vifaa au storage facilities (miundombinu ya kuhifadhi) kwamba wanunue mzigo Ruvuma halafu wautunze kwenye maghala na tatu walikuwa hawana fedha za kutosha kununua mzigo wa mwaka mzima.

Waziri Hasunga alisema Septemba 30 mwaka huu watakuwa na mkutano wa wadau wote wa korosho nchini utakaofanyika Dar es Salaam ambapo watawaeleza taratibu zote na namna watakavyoendesha na kusimamia minada hiyo.

Alisema mtu ama kampuni yoyote iliyopo ndani, iliyopo nje ya nchi, anayetaka kushiriki minada hiyo atalazimika kujisajili kupitia mfumo wa kompyuta wa Wizara ya Kilimo.

“Wanajisajili kwamba mimi mwaka huu nitashirki katika minada ya kununua korosho na wataonesha kiasi cha korosho ambacho anakihitaji kwa tani, bei hataonesha. hadi sasa kuna makampuni mengi ya nje yameonesha nia ya kuja kununua korosho zetu, milango iko wazi waje kujisajili.

“Ile  platform (mfumo) itakuwa ni soko la bidhaa, maana yake tutakapoendesha kama kuna korosho ziko Lindi, Mtwara au ziko Mkuranga zote zitatengenezewa kitu tunaita ‘catalogy’ ambazo zinaonesha aina gani ya korosho ziko katika hayo maghala na ile catalog  ndiyo tutakayoitangaza,” alisema Waziri Hasunga.

Alisema wanafikiria minada hiyo ifanyike mara mbili kwa wiki  katika kipindi cha msimu na kwamba jambo hilo watalipeleka kwa wadau.

“Lakini pia tumetoa nafasi katika huo mfumo wakulima kuwa na bei yao ambayo kama bei (ya mnunuzi) haijafika kiwango hiki sisi mzigo wetu hatuuzi. Bei hiyo watu wengine hawataijua ila wakulima kupitia chama chao cha msingi watakuwa wametuambia,” alisema Hasunga.

Alisema wakati minada hiyo inafanyika wataweka televisheni maeneo mbalimbali ya wakulima wa korosho nchi nzima ili kuwawezesha wakulima kuangalia minada inavyoendeshwa.

Hasunga aliongeza kuwa kwa kutumia mfumo huo waamini wanunuzi watakuwa na bei nzuri kwa sababu watakuwa wanashindana dunia nzima kwa uwazi na wakulima watakuwa wanaona kinachoendelea sokoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles