24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yadhamiria kulinda, kuimarisha afya za Watanzania

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kulinda na kuimarisha afya za Watanzania hasa  kipindi hiki cha kuelekea kutimiza dira ya kuutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030.

Ametoa kauli hiyo leo Novemba 26, 2021 wakati akifungua Kongamano la Kisayansi la Kitaifa Kuhusu VVU na UKIMWI katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mbeya Modern Highland, jijini Mbeya.

Kaulimbiu ya Kongamano hilo inasema “Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi walioshiriki katika Kongamano la Kisayansi la
Kitaifa kuhusu VVU na UKIMWI katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, kutoka kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Ummy Nderiananga, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Godwin Mollel na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji  wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko kwenye ukumbi wa Mbeya Modern Highland Hotel, Jijini Mbeya, Novemba 26, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Amesema kuwa kaulimbiu ya kongamano hilo inaakisi dhamira ya Serikali ya kulinda na kuimarisha afya za Watanzania.

“Hivyo basi, nitoe rai kwa jamii kutafakari upya nafasi waliyonayo na kupinga kwa nguvu zote masuala yote na tabia zinazochangia maambukizi mapya ikiwemo unyanyapaa, ukatili wa kijinsia, mila zinazochangia maambukizi, ngono katika umri mdogo, kuporomoka kwa maadili na tabia nyinginezo hatarishi.

“Kaulimbiu hii, imekuja wakati muafaka ambapo kama Taifa tunahitaji kuihamasisha jamii na mtu mmoja mmoja kuzingatia usawa na kutoa mchango wake katika kufikia azma ya kutokomeza maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana wetu ambao kwa mujibu wa Takwimu wanachangia kiwango kikubwa cha maambukizi mapya,” amesema Waziri Mkuu.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi cha DREAMS kinachohamasisha mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya UKIMWI jijini Mbeya, wakati  alipofungua Kongamano la Kisayansi la Kitaifa kuhusu VVU na UKIMWI katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, kwenye ukumbi wa Mbeya Modern Highland Hotel, Jijini Mbeya Novemba 26, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali ikiwamo sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu.

Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI pamoja na kutafuta vyanzo vya uhakika zaidi vya kutunisha mfuko huo.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kwa niaba ya Serikali kuwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI nchini.

“Ninawahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kupambana na tatizo hili la UKIMWI,”

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Ummy Nderiananga, amesema kuwa wadau wote walioshiriki katika kongamano hilo watumie ujuzi na maarifa waliyopata katika kuboresha kazi zao, pia taasisi zinazojihusisha na masuala ya VVU na UKIMWI ziongeze nguvu kwa kundi la wenye ulemavu.


Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kisayansi la Kitaifa kuhusu VVU na UKIMWI katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao alipofungua kongamano hilo kwenye ukumbi wa Mbeya Modern Highland Hotel, Jijini Mbeya, leo Novemba 26,2021 kwenye ukumbi wa Mbeya Modern Highland Hotel, Jijini Mbeya Novemba 26, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
 
 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko, amesema kongamano hilo ni fursa ya kuweza kutafakari walikotoka ili waweze kuendelea kutekeleza afua za VVU na UKIMWI.

Amesema kongamano hilo linawapa fursa nzuri ya kupata takwimu zinazowasaidia kuboresha utendaji kazi  ambapo ametoa mfano mwaka 2016/17 walifanya tafiti na kubaini wanaume wako nyuma katika suala zima la upimaji hivyo wanatakiwa wahamasishwe  ili nao wajitokeze kwa wingi kupima.

Naye, Mwakilishi wa Mratibu Mkazi wa PEPFAR Tanzania, Dk. Hiltruda Temba ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira ya dhati ya kutokomeza VVU na UKIMWI nchini pamoja na kuendelea kutoa kipaumbele katika huduma muhimu za kinga pamoja na utekelezaji mzuri wa afua za UKIMWI.

Pia, Dk. Hiltruda amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kufikia malengo ya kuwa na asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya watu wanaofahamu hali zao za maambukizi ya VVU wanapata tiba na asilimia 95 ya waliotumia dawa za ARV wamefanikiwa kupunguza kiasi cha maambukizi.

Dk. Hiltruda amesema PEPFAR na wadau wengine wa maendeleo wanaahidi kuendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo yake ya kimkakati kama yalivyoainishwa kwenye mkakati wa nne wa Taifa wa VVU na UKIMWI.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles