25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YADANGANYWA, YAJENGA DODOMA BADALA YA SINGIDA

 Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM


 

TANZANIA ni nchi ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii kutokana na wanyama, mandhari, fukwe, misitu na milima yake.

Watalii kutoka nchi mbalimbali duniani wamekuwa wakivutiwa na vivutio hivi vinavyopatikana katika mikoa mbalimbali ya nchi. Mwasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere aliona uwezo wa maliasili kusaidia maendeleo ya nchi na kutenga robo ya nchi kuwa chini ya hifadhi ya wanyama mbalimbali na sasa imekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii.

Utalii ni sekta inayoipatia Taifa pato kubwa  kutokana na kuwa na vivutio vingi vinavyopatikana nchini kama mbuga za wanyama, nyumba za makumbusho, mambo ya kale kupanda Mlima Kilimanjaro, Olduvai Gorge na vinginevyo.

Sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa na inaaminika kwamba ingeweza kufikia asilimia 30 ya pato hilo kama kungekuwa na mkakati wa pamoja wa kutangaza fursa zilizopo na kuhimiza utalii wa ndani  na inalenga kuzidisha mara nane mapato yake ifikapo mwaka 2025.

Moja ya nyenzo za kufanikisha utalii duniani ni urahisi kwa mtalii kulifikia eneo la kuvutio kwa wakati na kwa gharama nafuu na kuimarisha miundombinu ya usafiri na huduma nyingine.

 Kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii nchini, kuna baadhi ya maeneo yamesahaulika kuwa nayo ni sehemu ya utalii ambayo yangeweza kuliingizia Taifa pato kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Akizungumza na MTANZANIA,  Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka (CCM), akitolea ufafanuzi juu ya maeneo ambayo yanafaa kufanywa kuwa vivutio vya utalii  ambavyo vinapatikana katika  jimbo lake vingeweza kuchangia Pato la Taifa  kwa kiasi kikubwa  kama vilivyo vivutio vingine nchini na kubadilisha sura ya nchi.

 Anasema Mkoa wa Singida ni mkoa uliogawanywa katika wilaya tofauti tofauti na una sehemu kuu mbili ambazo zinapatikana  katika Wilaya ya Manyoni na zingefaa kwa ajili ya utalii ambazo hazitambuliki  kwa jamii kama sehemu nyingine.

“Sehemu yenye sifa ya kwanza ni sehemu pekee inayopatikana alama ambayo inaonesha katikati ya reli ya kati  kutoka Dar es Salaam  na Mwanza ipo juu ya jiwe  lililowekwa na Wajerumani  katika Kijiji cha Sukamahela, Kata ya Solyia,” anasema Mtuka.

Anasema pamoja na kuwapo kwa alama hiyo, Watanzania wengi bado hawajatambua kuwa kile ni kivutio muhimu na fahari kwa nchi.

Anasema watu wengi wanaotumia usafiri wa barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, wamekuwa wakishuhudia alama hiyo lakini bado hawaelewi ina  maana gani na hawatambui kuwa ni kivutio, hivyo inatakiwa liwekwe bango kuashiria umuhimu huo.

Mtuka anasema katika alama hiyo hakuna kibao chochote kilicho na maandishi ya kuelezea historia ya alama  hiyo na hivyo watu bado hawajatambua  umuhimu wa alama hiyo.

Anasema sifa ya pili ya utalii katika wilaya hiyo ndipo ambapo  kinapatikana kitovu cha nchi ya Tanzania yaani ndio katikati  hasa ya nchi, ni kitovu  kilichopo katika Kijiji cha Chinsinjisa,  Kata ya Sasilo Tarafa ya Nkonko.

Anasema sehemu hiyo ilipimwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kubainika kuwa hapo ndipo  katikati ya nchi.

“ Watu wanashinda kutofautisha sehemu hizo mbili  ambazo ni  kwenye alama moja inayoonyesha  katikati ya Reli ya Kati na  kuna sehemu ambayo  inaonyesha katikati ya nchi na ambazo ni sehemu mbili tofauti kwa sababu vimesahaulika kuwa navyo ni sehemu ya utalii,” anasema.

Anasema wilaya hiyo  ikiwa inakaliwa na kabila la Wagogo na inasemekana  ndio wilaya  ambayo Wajerumani walibainisha  kuwepo katikati ya  Tanzania  kwa kutokea upande wa Mashariki au Magharibi au Kaskazini na hata Kusini mwa Tanzania.

Anasema kutokana na kuwa vivutio hivyo na vinginevyo ni utalii mkubwa,  vinahitajika kutangazwa na kuvithamini.

 “Ili kukuza utalii wa ndani na kuwafanya wenyeji  na wageni wafaidike, ni lazima kuwe na mikakati mizuri inayolenga pia kuongeza pato la Taifa katika maeneo hayo,” anasema.

 Mtuka anasema ili kutangaza zaidi vivutio hivyo, wanatakiwa kuanza kutoa historia ya maeneo hayo shuleni  kama ilivyo  kwa vituo vingine kama historia ya Mkwawa ma Kinjekitile Ngwale.

Anasema sekta ya utalii iendelee kubuni huduma mbalimbali za kukuza  utalii nchini na kuongeza  pato la Taifa na kukuza uchumi.

Pamoja  na  changamoto nyingi zinazoikabili sekta hiyo,Mtuka anaamini wakiweka mikakati mizuri  watanufaika na maeneo hayo.

Anasema anaishauri Serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga minara katika maeneo hayo.

 Mtuka anasema anawakaribisha wawekezaji kujenga hoteli kwa ajili ya kufikia watalii wanapokuwa wanakuja kutembelea vivutio hivyo. Hivi sasa hakuna utalii wowote unaofanyika katika maeneo hayo.

Mtuka anasema kama vituo vikifanikiwa kuboreshwa, vitafungua fursa kwa Watanzania kwa kufanya biashara katika maeneo hayo na ajira zitapatikana kwa vijana kutokana na kuwepo watalii wengi.

Anasema  kwa sasa wanatakiwa kutoa elimu kwa wanachi kuhusiana na vivutio hivyo  ili wawe na uelewa na kutangaza utalii katika mataifa mengine.

Anasema  kwa kutambua umuhimu wa biashara ya utalii, Serikali na wananchi kwa ujumla wana wajibu wa kutangaza rasilimali hizo zilizohifadhiwa  kwa faida ya uchumi  wa nchi.

Anasema ukuzaji viwanda kwa lengo la kuifanya nchi itimize malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, utachangiwa pamoja na utalii na sekta nyingine.

 Kwanini Dodoma na si Singida?

Maelezo hayo ya Mbunge  Mtuka yanazaa mkanganyiko wa ajenda kuwa Taifa limedanganywa kwa kuaminishwa kuwa ni Dodoma na si Singida na hivyo Serikali ya Awamu ya Tano inajikusanya kuhamia Dodoma kwa hali na mali na wala si Singida,  kwani inaamini kuwa pale Dodoma ndio katikati ya nchi? Nani amepotosha ukweli huo na kwanini? Je nchi iendelee kuheshimu kile ambacho kimethibitishwa kitaalamu kuwa si sahihi? Ni Mkoa wa Singida wilayani Manyoni, Kijiji cha Chinsinjisa, Kata ya Sasilo Tarafa ya Nkonko na wala si Chimwaga mjini Dodoma kuwa ni katikati ya nchi.

 Mbunge Mtuka  alipoulizwa kuhusu kupotoshwa ukweli na kunyang’anywa  fursa  mkoani mwake  na kupewa Dodoma, alionesha  kuwa na sintofahamu  na kujibu kisiasa zaidi.

Anasema katikati ya nchi iwe Singida na si Dodoma  kwani ukiweka ramani ya Tanzania, vipimo vya ‘survey’ vinaonesha  pini  hiyo inaangukia katika Wilaya ya  Manyoni.

“Kutoka  Dodoma hadi Manyoni ni km 126 ni karibu na  ikumbukwe   kuwa mikoa  hiyo inaitwa  mikoa ya katikati ya nchi  kwa ujumla wake na ninaamini  kuwa kutokana  na ukaribu huu, Dodoma  ikipanuka  na Manyoni itapanuka, ni sawa  na Dar es Salaam na Bagamoyo na hivyo watu wamejenga  na wamewekeza,” anasema .

Mtuka anasema  Dodoma ndiyo sehemu nzuri  kwa ujenzi wa makao makuu ya nchi  kwa sababu Manyoni  maeneo yake mengi ni mapori  na vilima na si  nzuri kwa kujenga  na wakijenga makao makuu eneo ni finyu.

Anasema anaungana na  kukubali maamuzi ya  Serikali  kuwa makao makuu iwe Dodoma kwa sababu haoni tofauti ya  mkoa huo na wilaya hiyo.

Anasema kujenga  minara  katika vituo hivyo viwili  kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo ni  kidogo  na hazitoshi kuendeleza minara  hiyo na fedha inatolewa kwa ajili ya  miradi  ni kidogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles