24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UFUGAJI HOLELA, WATAKA MBUGA ZA WANYAMA CHACHE

Na Shermarx Ngahemera


TANZANIA ni nchi ya amani kwani watu wake wana utamaduni na shughuli mbalimbali wanaelewana na hivyo kufanya shughuli zao za kiuchumi na maendeleo bila taabu yoyote.

Lakini hali hiyo inatishiwa na mambo ya mahusiano katika mambo mengi na hivyokudai suluhisho kutoka serikalini kwani ndio mhusika mkuu wa matatizo hayo kama utayatazama  kwa kina na wafugaji/ wachungi kwa wanaotazama juu juu.

Ni ukweli kuna kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya  watu na wanyama Tanzania na hivyo wote hawa wanahitaji ardhi ya makazi, malisho na kilimo na hivyo kusababisha mgongano wa maslahi kwa pande zote husika ikiwemo serikali yenyewe. Sheria Iliyounda Mamlaka ya Ngorongoro inatakiwa kubadilishwa kwani ilikuwa kwa watu 9000 mwaka 1959 sasa idadi ya watu ni 90,000 na hivyo sio rahisi kuwalisha bila kazi yoyote.

Kuna tatizo la uhaba wa ardhi ambalo serikali inalikataa na kusisitiza kuwa tatizo ni watu na hasa wachungaji kukosa kuheshimu sheria ambayo wanaivunja kwa kufikiri kuwa eneo lote la nchi ni malisho na hivyo litumike kwa kazi hiyo. Hayo yakiendelea wafugaji wanatumia nguvu na silaha walizojimilikisha kumega mapande makubwa ya ardhi kupitia chama chao cha wafugaji kilicho na matawi nchi nzima. Ukiacha CCM chama chenye mtandao wa kitaifa ni chama hicho.

Serikali nayo inang’ang’ania kuwa maeneo yote yaliyoainishwa kisheria kwa hifadhi ya  wanyama pori yaendelee hivyo na ikiwezekana ipanuliwe mipaka ili eneo la hifadhi liwe kubwa na nchi ifanikiwe kwenye masuala ya utalii. Wananchi  wanatafuta ardhi ya kulima mazao ya chakula na biashara na hivyo kufifisha ari ya watu wanaotafuta maendeleo yao kwani ardhi imesha kuwa haba.

Serikali inajibu hoja kuwa watu wajilaumu wenyewe kwa kuharibu ardhi kwa kukata miti na kufanya nchi kwenye sehemu nyingi iwe nusu jangwa na hivyo kunyemelea maeneo ya hifadhi.

Anasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali  Gaudence Milanzi kuwa migogoro ya ardhi itakwisha tu pale wananchi watakapoheshimu sheria na mazingira na kuondokana na tabia mbaya ya kuchezea vyanzo vya maji , misitu na mbuga rasmi za wanyama. Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA , Dk Kijazi anasema mbuga zilikuwepo kabla ya watu  wanaovamia kwa hiyo wao ni wavunja sheria wasipewe nafasi kwani vurugu zitatawala.

Wafugaji  ambao  kimsingi ni wachungi kwa upande wao wanadai kuwa kikatiba Watanzania wanaruhusiwa kuishi popote na kufanya shughuli zao za kiuchumi na maisha bila bughudha yoyote. Wafugaji/wachungi wanahoji kwa nini wanazuiwa na kubughudhiwa na vyombo vya dola wakati wanajitafutia riziki?

Sheria inataka kutafuta riziki kuwe kwa uhalali na haki na sio kufanya vurugu na kuminya haki za watu wengine  na hivyo kuingia kwenye matatizo.

Matokeo ya vurugu na kutoelewana kunaleta hali ya wasiwasi na chuki kati ya wakulima na wachungi na Mamlaka za hifadhi maeneo mbalimbali na huenda kutafuta suluhisho serikalini wakati yenyewe ni sehemu ya tatizo.

Lakini serikali haini  utata huo na hivyo kukomalia msimamo usio na tija na kutolipa kipaumbele suala hilo hatari kwa usalama na usitawi wanchi yetu. Ni kuonekana kichekesho kuwa nchi hii ya amani na huku watu wanakufa bila sababu yoyote ya msingi kwa kukosa maelewano.

Umuhimu wa usalama

Maisha na usalama wa watu lazima uheshimiwe  na kupewa kipaumbele na hivyo  ni lazima suluhisho la kudumu lipatikane kwa kuzingatia mahitaji ya pande zote zinzohusika.  Serikali lazima ijitathimini kwa kina na kuona kuwa inatumia nguvu  nyingi na ya ziada wakati kinachotakiwa ni kupeana ukweli na kwa mabadiliko ya sera , kufanya mabadiliko ya mtazamo na kuweka mbele mahitaji ya Taifa ya amani, utulivu na maendeleo.

Ni kujidanganya kufikiri Serengeti, Selous, Ruaha , Mikumi na Manyara bado ni zilezile pamoja na mahitaji yake wakati watu wanaozunguka mbuga hizo wameongezeka zaidi ya mara tano au kumi na mahitaji ya kiuchumi yamebadilika katika kila hali na uhalifu unatumika pande zote kujinufaisha.

Wanasiasa nao wamejiingiza kwenye matatizo ya migogoro kwa kuwaambia wananchi wavunje sheria kwa kuvamia mbuga za hifadhi ya wanyama kwa  kuchunga wanyama mbugani huku wakijua wazi ni makosa kufanya hivyo. Mifano ya Simiyu, Maswa na Serengeti imethibitisha changamoto ya wanasiasa kuingilia mambo kimakosa.

Inabidi nchi ifanye tathimini ya kweli kuhusu matatizo ya ardhi kwani uzoefu unaonesha kuwa ardhi Tanzania sio nyingi hivyo kama inavyofikiriwa kwani siku hizi kila mahali ukipataka pana mwenyewe ambaye  sio serikali ingawa ni mapori.

Serikali inabidi itazame kama tunahitaji mbuga zote hizo kama hifadhi ya wanyama wakati nyingi zilizoko kusini ya nchi zinashindwa kujiendesha na kuwa mzigo kwa Shirika la Taifa la Mbuga za Wanyama (TANAPA).

Kwa mtazamo wa wachunguzi wa mambo kuwa wote wanaodai kukosewa kwenye tatizo hilo wanayo haki  kivyao na ni sahihi ukafanyika mkutano wa maridhiano wa pande zote ilikuwekeana mipaka ya kutumia keki ya ardhi katika masuala ya kiuchumi na kuacha kufikiri kuwa mambo yaache yaendelee kama ilivyo  sasa.

Kunahitajika mabadiliko sahihi na  ya kweli na sio kufanya siasa kwenye suala nyeti la  ardhi na uchumi.

Ni makosa makubwa kwa serikali kufanya nchi nzima kuwa malisho ya ng’ombe na hivyo kusababisha kesi zisizoisha za kugombea ardhi. Wafugaji ambao kitabia nimewaita kama wachungi ni dhana ambayo ifanyiwe kazi ili kuendesha ufugaji unaotakikana wa kutumia ufugaji wa kuletewa malisho na sio kutangatanga kutafuta malisho. Wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo kwani tunauza malisho  nchi za mbali kama  Australia kwa nini isiwe hapa nyumbani?

Darubini sekta ya mifugo

Mifugo ni sekta muhimu ya uwekezaji kwa maendeleo ya viwanda na inaweza kuwa ufumbuzi kuongeza pato la taifa na hivyo katika sakata hilo tuone mifugo kama fursa na sio kama balaa kama watu wanavyochukulia kwa makosa.

Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa idadi kubwa ya mifugo katika bara la Afrika ambapo ng’ombe wanafikia zaidi ya milioni 25, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni 8, nguruwe milioni 2.4, na kuku wanafikia milioni 36. Hali hii ni nguvu kubwa na sio unyonge kama inavyofanyika. Mifugo hiyo kwa idadi yake inahitaji malisho yanayoeleweka na sio katika hali ya kubabaisha ya uchungi.

Tanzania ina nafasi nzuri ya kunufaika katika sekta ya mifugo kutokana na uhitaji mkubwa wa bidhaa zinatokana na mifugo kuongezeka kila siku na sio rahisi kupatikana ila katika hali malumu.

Sekta ya mifugo Tanzania kwa kiasi kikubwa inaendeshwa na wakulima wadogo wadogo wasiokwenda shule na kujali sana mila na desturi kwa watu kama Maasai na Wasukuma na hivyo imeajiri mamilioni ya Watanzania. Sekta hii inaweza kuwa chachu ya kuboresha maisha ya wananchi na maendeleo endelevu hasa kipindi hiki ambacho serikali inataka kugeuza nchi kuwa ya viwanda ifikapo 2025. Inakila kitu cha kutoa mchango katika uchumikwani ina bidhaa kuu nane ikiwamo nyama, maziwa, ngozi, kwato, damu, mbolea na mifupa ambayo inaweza kuzalisha bidhaa nyingine ndogo ndogo.

Mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na utafiti wa mifugo ya International Livestock Research Institute (ILRI)  Tanzania, Amos Omore anasema kuwa Mifugo ni sekta yenye nguvu  ya kuleta mabadiliko kama tunahitaji wote  kumaliza njaa na kujenga mifumo endelevu wa chakula.

Anaelezea kuwa dunia nzima, watu bilioni moja huishi kwa kutegemea mifugo hasa wanawake na hutoa ajira kwa vijana. Asilimia15 ya kalori na asilimia 25 ya protini inatokana na wanyama  ambao ni muhimu katika mlo kamili na kuongeza uwezo wa kipato kwa idadi kubwa ya watu masikini.

Kwa mujibu wa Omore ongezeko la thamani ya bidhaa za mifugo ni nzuri hasa kwa kilimo biashara kutokana kwamba bidhaa sita za kimataifa zinatokana na  kilimo ambacho chanzo chake ni wanyama ikiwemo (maziwa, nyama ya nguruwe, nyama, kuku na samaki) ambayo thamani yake inafikia dola za Marekani bilioni 715.

Hata hivyo, ingawa mifugo inachangia asilimia 40 ya Pato la Taifa  katika nchi nyingi ambazo ni maskini zaidi duniani, lakini cha ajabu ni kuwa  zinapata asilimia 4 tu ya misaada ya maendeleo ya kilimo.

Kwa maelezo ya mwakilishi huyu utashangaa kuona kuwa sekta ya mifugo Tanzania  huchangia asilimia 13 ya Pato la Taifa ambacho ni kiwango cha chini sana kimchango ikilinganishwa na nchi zenye mifugo wachache.

“Hii inaweza ikabadilika ikiwa uwekezaji zaidi  utafanyika na kutumia fursa zinazojitokeza,” anasema Omore.

Anasema kufikia mwaka wa 2050, uhitaji wa nyama na maziwa katika soko la dunia inatarajia kuongezeka asilimia 145 na 155, katika kipindi hicho, uzalishaji wa nyama Afrika utaongezeka  sambamba na nchi zilizoendelea na zile za Amerika ya Kusini.

Soko la maziwa litakuwa kubwa katika Afrika hasa katika Afrika Mashariki, kuliko katika kanda nyingine yoyote isipokuwa Asia ya Kusini. Hii inatokana na kuongezeka kwa watu katika maeneo hayo wakati Ulaya na Marekani watu wanapungua.

Hata hivyo anachelea kusema kuwa ongezeko la uzalishaji wa mifugo haitarajiwi kuendana na ongezeko la matumizi ya nyama, maziwa na mayai katika bara la Afrika kutokana kukosekana tija.

“Afrika  itakuwa mwagizaji wa bidhaa za vyakula zinazotokana na wanyama kama uwekezaji hautafanywa, uwekezaji unahitajika ilikuendana na faida zinazotokama na mifugo kwa jamii na ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo ambayo inaweza kuzalisha,” anaelezea Omore.

Suala la malisho

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk  Charles Tizeba anatoa sehemu ya suluhisho ya migogoro ya wachungi na wakulima katika wizara yake kwa kuwapa njia mbadala wafugaji nchini wakati alipokuwa Tanga.

Anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha ukame na kuathiri mifugo, serikali imewataka wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini kujikita katika kilimo cha nyasi za malisho (hay) ili kukabiliana na ukosefu wa malisho msimu wa kiangazi na kuzuia kufanya mifugo kutangatanga  ovyo kutafuta chakula. Majani ya malisho yanatumika wakati wa kiangazi

Ushauri huo ulitolewa juzi na  Dk Tizeba wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuboresha ng’ombe wa maziwa kwa tija na kukuza kipato (ADGG-Tanzania) uliofanyika jijini Tanga.

 

Akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba Dk Tizeba, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alisema kilimo cha nyasi za mifugo kitawawezesha wafugaji nchini kukabiliana na ukosefu wa malisho msimu wa kiangazi.

 

Tizeba  alisema kuwa iwapo mtajikita katika kilimo cha nyasi za malisho, maana yake mtapewa na taaluma ya namna ya kuzihifadhi ili zitumike msimu wa kiangazi, huo utakuwa ni ufumbuzi wa kilio cha ng’ombe kutoa kiwango kidogo cha maziwa wakati wa kiangazi kwani hutokana na lishe duni.

Mratibu wa ADGG-Tanzania, Dk Eliamon Lyatuu alisema malengo ya mradi huo ni kujenga mfumo wa kitaifa wa kukusanya taarifa za uzalishaji ng’ombe wa maziwa nchini na utaendeshwa kwa kutumia teknolojia ya kieletroniki ikiwamo kuweka heleni ng’ombe.

Ofisa Mifugo Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Abdallah Temba alisema mradi huo utawezesha kuunganisha juhudi za wizara kukabiliana na changamoto zinazowakabili wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini na kile kinachoitwa, ‘zero grazing’ ambapo ng’ombe awa mwinyi na kuletewa kilakitu ndani.

Temba alsiema takwimu zilizopo zinaonyesha Tanzania ina ng’ombe 780,000 wa maziwa, ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa za kutokuwa na vinasaba sahihi katika kuzalisha ng’ombe bora na malisho.

Hivi basi kama kwenye ng’ombe wa maziwa imewezekana  kuwa na zero grazing juhudi za malisho kupatikana kirahisi zifanyike ile nao wale wa nyama waweze kupunguza kuzurura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles