27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

TRA, ZRB WAKUBALIANA MKATABA WA MAFUNZO

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


HIVI karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetiliana saini ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Chuo chake cha Kodi cha ITA na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kuwajengea uwezo wa kazi watumishi wa Bodi hiyo ya Zanzibar.

Katika makubaliano hayo, kutakuwa na kozi mbalimbali 64 ambazo watumishi hao watafundisha na lengo ni kuwajengea uwezo pamoja na kuwaongezea ujuzi ili kuimarisha utendaji wao wa kazi.

Mamlaka hizo zimepewa jukumu la kisheria la kuhakikisha zinakusanya mapato na kodi mbalimbali za Serikali ili kuiwezesha kufanya shughuli za kimaendeleo katika jamii yake.

Ili kuweza kumudu kazi za ukusanyaji mapato na kodi mbalimbali katika kiwango kinachostahili, inahitajika elimu ya mara kwa mara kwa watumishi ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kwa kufuata sheria.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwa na tija kwa taasisi hizo kutokana na kuwa kila jambo lenye kulenga mafanikio ni lazima liandaliwe mkakati wa kuhakikisha unafanikisha kile kinacholengwa.

Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, anasema baada ya kusaini makubaliano hayo mafunzo kwa watumishi hao wa Bodi ya Zanzibar yataanza mwezi  huu na  kwamba yataendelea hadi Juni.

Anasema mafunzo kwa watumishi wa mamlaka za mapato ni moja ya mikakati waliyoiweka ili kuhakikisha wanawajengea uwezo katika utendaji wa kazi na kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa kufuata sheria bila kumuonea mtu yeyote.

Kwa mujibu wa sheria, kila mwenye mapato anastahili kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi wake kwa kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana.

Taasisi hizo ambazo zimejipanga kuhakikisha zinasaidiana katika kufanikisha zoezi zima la ukusanyaji wa mapato, zitakuwa zikitoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa watumishi wake ili pia kuondoa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Naye Kamishna Mkuu wa ZRB, Amour Hamim Bakari, anasema matokeo ya makubaliano hayo yataanza kuonekana katika kipindi kifupi hasa ikizingatiwa kuwa mabadiliko ya teknolojia yanahitaji mafunzo ya kujengewa uwezo katika utendaji kazi.

Anasema maandalizi ya mafunzo ya awali yamekamilika na jana baadhi ya watumishi 13 wa ZRB wameshiriki katika mafunzo hayo ambayo yanaendeshwa na Chuo cha Kodi (ITA) kulingana na makubaliano yaliyowekwa.

Anasema taasisi hizo zinahitaji ushirikiano kutoka kwa kila mtu ili kuziwezesha kukusanya mapato ya Serikali kama zilivyotakiwa kufanya.

Anasema sambamba na wananchi, pia vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kueneza elimu ya kodi kwa wananchi na kuwafanya  washiriki katika kulipa kodi ya Serikali kama  ambavyo sheria na taratibu za nchi zinavyowataka kufanya.

Hili ni jambo zuri na ambalo litaweza kuleta  mafanikio kwa nchi hizi ambazo bado zinapambana kuhakikisha zinapiga hatua katika kupata maendeleo.

Kwa upande wa Tanzania Bara, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ambayo itawezesha kufanikisha lengo la ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha juu.

Baadhi ya mikakati ambayo TRA upande wa bara iliiweka na kuonyesha mafanikio, ni kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi iliyokuwa ikisababisha upotevu wa mapato kwa kiasi kikubwa, biashara za magendo, usisitizaji wa matumizi ya mashine za kielekroniki (EFDs), ikiwa ni pamoja na elimu ya kodi kwa wadau mbalimbali pamoja na taasisi za Serikali.

Pamoja na mikakati  mbalimbali ambayo TRA imeiweka, bado inahitajika ushirikiano kutoka kwa wananchi wazalendo ili kuhakikisha wanafanikisha malengo iliyojiwekea hasa katika zoezi zima la ukusanyaji wa mapato. Uzalendo una nafasi kubwa katika masuala ya kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles