Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
SERIKALI imeboresha mgawo wa fedha utakaowezesha upatikanaji wa dawa zikiwamo za shinikizo la damu katika ngazi zote za kutolea huduma za afya kuanzia hospitali hadi vituo vya afya.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, wakati akijibu swali la Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali haijui kuwa wazee wengi wanaosumbuliwa na magonjwa ya shinikizo la damu wanaishi vijijini ambako kuna zahanati pekee na si hospitali.
Pia alitaka kujua lini Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha dawa za aina mbalimbali za shinikizo la damu zinazowekwa katika zahanati zilizopo vijijini ambako ndiko kuna wazee wengi zinakuwepo.
Akijibu swali hilo, Kigwangalla, alisema: “Serikali inatambua uwepo wa wazee wengi sehemu za vijijini wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya utu uzima ikiwemo shinikizo la damu.”
Pia alisema Serikali inao mwongozo wa utoaji tiba za dawa ulioambatanishwa na orodha ya Taifa ya dawa muhimu.
“Orodha hiyo imebainisha dawa mbalimbali zinazotumika katika
ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma za afya ikiwamo vituo vya afya na zahanati,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema vituo vya kutolea huduma za afya vinayo mamlaka ya kuagiza dawa nyingine zozote za kutibu shinikizo la damu huku akisema wizara hiyo haizuii kituo chochote kuagiza dawa za kutibu shinikizo la damu.
Katika swali la nyongeza, Gama, aliitaka Serikali kueleza lini itatoa huduma ya matibabu bure kwa wazee ili waondokane na adha ya kupata huduma hiyo wanaposumbuliwa na magonjwa mbalimbali pia alitaka kujua
mpango wa Serikali wa kuwapa wazee pensheni ili waweze kujikimu hususani katika masuala ya matibabu.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla, alisema kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Taifa, wazee wanatibiwa bure na kuhusu pensheni alisema Serikali kupitia takwimu za mwaka 2012 inaendelea na mchakato ili kupata idadi ya wazee watakaohudumiwa na mpango huo.