25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANANDOA HATIANI KWA KUFICHA MENO YA TEMBO

Na Kulwa Mzee

-Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewatia hatiani Peter Kabi na mkewe Leonidia Kabi, waliokutwa na meno ya tembo yenye thamani zaidi ya Sh bilioni mbili wakiwa wameyaficha katika jeneza huku wakilifunika kwa Bendera ya Taifa.

Washtakiwa hao walihukumiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka na utetezi wa washtakiwa wenyewe.

Shahidi alisema katika ushahidi huo, mshtakiwa Polisi Malisa haukumgusa popote wala hakuna namna ya kumuunganisha katika kesi hiyo hivyo hajapatikana na hatia.

Baada ya Shahidi kuwatia hatiani Peter na mkewe, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliomba alete ushahidi wa ziada ili washtakiwa wapewe adhabu stahiki iwapo mahakama itaona inafaa.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, mahakama imeridhia na kuiahirisha kesi hadi Februari 13, mwaka huu ambapo itasikiliza ushahidi wa ziada na kuwapa adhabu washtakiwa hao.

Washtakiwa wanadaiwa kuwaua tembo 93 kwa sababu katika meno waliyokutwa nayo ndani ya nyumba yao Kimara, mazima yalikuwa 158 ambayo ukigawa kwa mbili ni sawa na tembo 79, kwa kuwa tembo mmoja ana meno mawili.

Pia kutokana na vipande vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa vipande vya chini (base) 24 ambapo ukigawa kwa mbili ni sawa na tembo 12 waliuawa ambao kwa pamoja wana thamani ya Dola 1,395,000 za Marekani sawa na Sh 2,206,611,000.

Hata hivyo, katika utetezi wao, washtakiwa walikana nyara hizo hawazielewi na kwamba maelezo ya onyo waliyoyatoa polisi yalichukuliwa baada ya wao kuteswa na kulazimishwa kukubali.

Hakimu Shahidi alisema maelezo hayo ya onyo ni halali na kilichoandikwa kilikuwa sahihi na kwamba wakati chumba kilipofunguliwa na polisi kilichokutwa na nyara Leonidia alipoteza fahamu.

Alisema mshtakiwa huyo alizimia kwa sababu alikuwa anajua uwepo wa nyara hizo katika nyumba yao.

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kuendesha biashara ya nyara za Serikali na kukutwa na nyara hizo kinyume cha sheria.

Wanadaiwa Oktoba 27, 2012 katika maeneo ya Kimara Stop Over, Dar es Salaam kwa pamoja washtakiwa hao  waliendesha vitendo vya uhalifu kwa   kupanga, kukusanya na kuuza vipande 210 vya meno ya tembo na vipande vitano vya mifupa ya tembo.

Alidai kuwa vipande hivyo vya meno ya tembo vilikuwa na uzito wa kilo 450.6 vyenye thamani ya Dola 1,380,000 za Marekani.

Kwa upande wa vipande vitano vya mifupa ya tembo vilikuwa na thamani ya Dola 30,000 za Marekani na kwamba vyote vilikuwa na thamani ya Dola 1,410,000 za Marekani ambayo ni sawa na Sh 2,206,611,000.

Wakili huyo aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao walijihusisha na biashara hiyo bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles