WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amesema Serikali imejipanga kuandaa mashamba ya mbegu bora za pamba ili kumaliza tatizo la mbegu kutoota linalowakabili wakulima za zao hilo.
Alikuwa akizungumza na wadau wa pamba katika kikao cha kuchajadili maandalizi ya msimu ujao wa kilimo Jijini Mwanza.
Dk. Tizeba alisema Serikali imeamua kulifuatiliwa tatizo la mbegu za pamba kutokana na kukwamisha ufanisi wa kilimo kwa sababu ya mbegu zisizoota.
“Serikali bado inafanyia kazi suala la upatakanaji wa mbegu bora za pamba kwa vile wazalishaji wameshindwa kufikia robo ya mahitaji kwa wakulima.
“Mfano Kanda ya Magharibi ambayo inahitaji tani 21,000 mpaka sasa wameweza kuzalisha tani 350, hivyo serikali tumejipanga kuandaa mashamba kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora mwakani mkulima apate mbegu hizo kwa urahisi na kwa wakati,” alisema Dk. Tizeba.
Aliiagiza Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania ( TOSCI), kufikia Oktoba 5 mwaka huu iwe imeanza ugawaji wa mbegu za pamba zilizo tayari kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo kwa maeneo ya Biharamulo, Kombe, Geita na Chato na kuhakikisha baada ya wiki tatu iwe imekamilika.
Waziri alisema katika kuendeleza zao la pamba Serikali imetenga Sh bilioni 5 kwa ajili ya pamba, fedha ambazo zitatolewa kwa wakulima bure kupitia fedha hizo za Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza zao la Pamba( CDTF).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pamba, James Shimbe, alisema katika msimu wa kilimo mwaka 2016/2017, wakulima wanatarajia kulima zaidi ya hekta 400,000 kwa Kanda ya Magharibi.
Alisema CDTF inatarajia kuagiza chupa 500,000 za viuatilifu zenye uwezo wa kuhudumia ekari 166,666 kwa kunyunyuzia mara tatu kwa kila ekari kutokana na uwezo wa fedha wa mfuko huo kushuka katika msimu huu.
Alisema bodi hiyo ilielekeza makampuni yaliyonunua pamba msimu huu kuhifadhi tani 21,000 za mbegu za kupanda kutoka maeneo ambayo hayana ugonjwa wa mnyauko fuzari kutokana na ukosefu wa mbegu bora za kutosha katika kuhakikisha eneo hilo linahudumiwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania, John Msemwa, alisema hadi kufikia Septemba 10, mwaka huu zilikuwa zimekwisha kuchukuliwa sampuli 239 ambazo ni tani 138.3 za mbegu zisizo na manyoya.
Alisema zenye manyoya ni tani 5836.7 kutoka kwa wachambuzi 13 na kampuni moja kwa ajili ya upimaji ambao unaendelea kujua ubora wa mbegu hizo.
Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (TACOGA), Lucas Hazina, alisema wakulima wamejipanga kulima zao hilo kwa wingi kuinua uchumi wa nchini.