Hadija Omary, Lindi
Serikali mkoani Lindi imesema itaendelea kutumia wataalamu wake wa ndani katika kutekeleza miradi midogo ya ujenzi ili kutumia fedha kidogo zinazopatikana badala ya kutumia wakandarasi wenye gharama kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema hayo jana wakati wa ziara yake ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine.
Amesema mkakati uliopo kwa sasa ni kuendelea kuwatumia wataalamu wa ndani wale waliopo katika taasisi za serikali ambao wapo ndani ya mkoa katika kutekeleza miradi midogo na kwamba itatumia wakandarasi kwa miradi mikubwa pekee.
“Kwa kutumia wataalamu wa ujenzi wa ndani fedha nyingi zimekuwa zikiokolewa kutokana na wataalamu hao kutumia fedha kidogo kulingana na mfumo wa matumizi ya fedha hizo,” amesema Zambi.
Ujenzi wa miundombinu katika hospitali hiyo unatarajia kutumia Sh milioni 214 ambapo kwa kuweka kisima cha maji pamoja na matanki yake, wodi ya watoto na matundu ya vyoo.