SERIKALI imesema kuwa haina takwimu za watoto waliokeketwa nchini kutokana na vitendo hivyo kufanyika kwa siri.
Pia imesema kuwa haina takwimu ya watu waliopelekwa mahakamani kutokana na wale ambao wamehusika na ukeketaji .
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamisi Kigwangalla ,alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Gidarya (Chadema).
Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ina takwimu za watoto waliokeketwa pamoja na takwimu za watu waliopelekwa mahakamani kutokana na vitendo vya ukeketaji.
Awali katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na ukatili ambao wanafanyiwa watoto wa kike kwa kukeketwa.
“Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa ukeketaji wa watoto wa kike, takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kitaifa.
“Je Serikali ina mpango gani madhubuti wa kukomesha ukatili huu wa kijinsia pamoja na kutoa semina elekezi kuhusu madhara yanayotokana na ukeketaji wa watoto wa kike hususani katika wilaya za Hanang’, Simanjiro, Kiteto na Mbulu,” alihoji mbunge huyo.
Akijibu maswali hayo, Dk. Kigwangalla alisema vitendo vya ukeketaji vinafanywa kwa siri zaidi, hivyo Serikali haina takwimu za watoto waliokeketwa wala waliopelekwa mahakamani.
Hata hivyo, alisema Serikali inatoa makatazo ya kuwakeketa watoto wa kike kwani kwa kufanya hivyo ni kuwanyanyasa kijinsia watoto wa kike.