24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Septemba Mosi kijeshi

Kanali Ngemela RubingaNa MAULI MUYENJWA – DAR ES SALAAM

NDEGE za kijeshi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zitaruka angani kesho Septemba Mosi, kuadhimisha miaka 52 ya kuanzishwa kwa jeshi hilo.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Ngemela Rubinga, alipokuwa akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ratiba ya maadhimisho ya siku hiyo mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kanali Rubinga, ndege hizo zitarushwa kwa ajili ya kutoa heshima kwa Watanzania ambao ndio waajiri wa JWTZ.

“Miaka 52 ni mingi na tunajivunia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kulinda amani katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Kwa hiyo, siku hiyo ndege zitaruka kuwaonyesha wananchi jinsi jeshi lao lilivyo pamoja nao.

“Pamoja na kurusha ndege hizo, siku hiyo pia tutaiadhimisha kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali kama sehemu ya kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikisisitiza kufanya usafi.

“Pia, siku hiyo tutachangia damu katika hospitali mbalimbali na madaktari wetu watakuwa wakitoa ushauri kwa wagonjwa kuhusiana na magonjwa mbalimbali.

“Kwa wale wasiofahamu, maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa wiki moja iliyopita, lakini Septemba mosi ndiyo kilele chake ambapo shughuli nyingi zitafanywa ikiwa ni pamoja na magwaride yatakayofanyika katika kambi zetu kama sehemu ya kukumbushana masuala mbalimbali,” alisema.

Naye Makonda alipokuwa akipokea ratiba hiyo, alisema wananchi wasiogope pindi watakaposikia milio ya ndege za kijeshi bali wazishangilie ndege zao kwani siku hiyo ni ya amani.

“Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka na tunaamini wananchi wanajua hivyo, kwani ni sherehe muhimu na kuna kila sababu ya kujivunia jeshi letu la JWTZ kwa mafanikio waliyoyapata kwa miaka 52.

“Katika utekelezaji wa jambo hilo, wakuu wa wilaya hapa Dar es Salaam wameshajipanga kwa ajili ya kujumuika na jeshi kufanya usafi na kama kuna wananchi au taasisi zozote zitakazotaka kuunga mkono kufanya usafi siku hiyo, zifike ofisini kwangu ili wapangiwe maeneo,” alisema Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles