31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi wapiga kambi Chadema

chademaNa WAANDISHI WETU

– DAR ES SALAAM

NI mwendo wa doria. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya askari polisi kulazimika kupiga kambi katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zilizopo Mtaa wa Ufipa, Dar es Salaam.

Polisi hao tangu jana asubuhi walikuwa wakifanya doria katika eneo hilo huku wengine wakizingira ofisi za chama hicho wakiwa wamevaa kiraia.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilituma timu ya waandishi ambao kutwa nzima ya jana waliwashuhudia askari polisi wakiwa nje ya ofisi za chama hicho na wengine wakiwa ndani ya magari ya doria.

Hatua hiyo ilionekana kuzua taharuki kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa juu wa chama hicho ambao walijikuta wakishindwa kufanya kikao cha dharura cha Kamati Kuu kwa hofu ya kuzuka vurugu.

Ilipotimu saa tano asubuhi, timu ya walinzi wa Chadema ‘Red Brigade’ waliongezeka na kusimama nje ya ofisi za makao makuu huku wakionekana kuwa tayari kwa lolote, ikiwamo kujihami kwa kuwalinda viongozi wao; mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye ambao waliwasili katika ofisi hizo kwa ajili ya kikao.

Kikao hicho kilikuwa ni cha mwandelezo baada ya kile cha juzi kushindwa kumalizika na baadhi ya viongozi wa chama hicho kukamatwa na polisi.

Pamoja na hali hiyo, ilipotimu saa 9 alasiri, viongozi hao wakiongozwa na Lowassa walitoka nje na kuelezwa kuwa kikao kimeshindwa kufanyika kwa kuwa hali ya usalama si nzuri, hasa baada ya kuonekana askari kanzu wakiingia ndani ya ofisi hiyo na wengine kujifanya ni wanachama wa chama hicho.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu, Dk. Vicent Mashinji, walilazimika kuondoka mapema na kwenda katika kikao cha pamoja kati yao na viongozi wa dini ili kutafuta mwafaka, kuhusu Operesheni Ukuta inayotarajiwa kufanyika kesho licha ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi.

Kikao hicho cha viongozi wa dini kilichofanyika katika Hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine kilijadili kwa kina mkwamo wa kutafuta suluhu kati ya viongozi wa Chadema na Serikali kuhusu kuzuiwa maandamano ya kesho.

MTANZANIA ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji ili kupata ufafanuzi kuhusu kuzingirwa kwa ofisi zao na maofisa wa polisi, alikiri kutokea kwa hali hiyo.

“Ni kweli tumeahirisha mkutano wetu wa Kamati Kuu mpaka hapo baadaye, Ofisi zetu za Makao makuu zilizingirwa na askari wa kila aina, wengine walivaa baraghashia, kanzu na kila aina ya nguo kwa lengo la kuvunja na kutawanya mkutano wetu wa ndani, tumeuahirisha mpaka wakati mwingine, tutawajulisha.

“Askari hao wamekuwa wakipiga kambi katika ofisi zetu kwa muda wa wiki sasa, lakini kadiri siku zinavyokwenda idadi yao inazidi kuongezeka kama ilivyokuwa leo (jana),” alisema Dk. Mashinji.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa wajumbe wa Kamati Kuu walikutana ili kujadili mambo mbalimbali ikiwamo suala la maandamano yanayotarajiwa kufanyika nchi nzima kuanzia kesho.

 

VIONGOZI WA DINI

Viongozi wa dini nchini wameendelea kukuna vichwa kutafuta suluhu kati ya Serikali na vyama vya siasa vinavyojiandaa na Operesheni Ukuta iliyopangwa kufanyika kote nchini kesho.

Viongozi hao walijichimbia jana Hoteli ya Courtyard katika kikao cha siri ambacho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, Katibu Mkuu wake, Mashinji na mawaziri wakuu wa zamani; Sumaye na Lowassa.

Taarifa za ndani zinasema kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana aliwasili hotelini hapo saa nne asubuhi, lakini aliondoka punde baada ya kupokea simu ambayo inadaiwa alipigiwa na Rais Dk. John Magufuli.

Kikao hicho kilichoanza saa mbili asubuhi hadi saa tisa alasiri ni cha tatu kufanyika, ambacho mbali kuhudhuriwa na viongozi dini, pia kilihudhuriwa na vyama vitano vyenye uwakilishi bungeni huku agenda kuu ikiwa ni hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kuwa ulimalizika salama na kukubaliana na kwamba watatoa taarifa rasmi ya kikao hicho leo kwa umma.

“Kikao chetu tunamshukuru Mungu tumemaliza salama na kwa pamoja tumeweza kukubaliana mambo mbalimbali, ikiwamo ya hali ya kisiasa nchini, wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge pamoja na Operesheni Ukuta, ambayo tutayazungumza kwa waandishi wa habari kesho (leo) ili Watanzania waweze kuyajua,” alisema Sheikh Alhad.

Pamoja na mambo mengine, alisema kwa sasa hali ni nzuri na wanaamini mkutano huo utaweza kurudisha hali ya utulivu, umoja na mshikamano kwa wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, dini au kabila.
KAULI YA MASAJU

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa mkutano huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, aliliambia MTANZANIA kuwa Serikali iwaache wafanye mambo kwa wakati wanaoona unafaa.

Dk. Shoo alikuwa akizungumzia kauli iliyotolewa juzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akiwataka viongozi wa dini kuliombea taifa lisiingie kwenye uvunjifu wa amani kutokana na Operesheni Ukuta na kwamba huu si wakati mwafaka wa kukaa meza ya majadiliano.

“Sisi tunafanya vitu kwa wakati tunaoona unafaa, siyo yeye atuamuru cha kufanya, namuomba ayaache haya mambo hivi hivi kwani tunaujua wajibu wetu kwa Serikali na wananchi ambao ni waumini wetu.

“Kwa sasa haya mambo tuyaache yabaki kama yalivyo, sisi tunazungumza kuhusu masuala hayo hayo na tumefikia mahali pazuri, mtayasikia kesho (leo), bado kikao hakijaisha,” alisema Dk. Shoo.

 Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta na Esther Mbussi, Dar es Salaam

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles