Andrew Msechu, Dar es Saam
KONGAMANO la Pili wa wadau wa Sekta na Gesi na Mafuta uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam umeonesha namna vyanzo hivyo vya nishati vinavyoendelea kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani, kuja kuwekeza katika sekta hiyo.
Kongamano hilo lililowakutanisha zaidi ya watu 340 kutoka nchi 75 duniani, zikiwemo kampuni kubwa za mafuta na gesi limeibua namna rasilimali hizo zinavyoweza kutumiwa kuimarisha uchumi wa nchi, japokuwa bado kuna malalamiko kuhusu namna mifumo ya utoaji wa nishati ya gesi inavyocheleweshwa.
Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Godfrey Simbeye anasema tayari wapo wawekezaji katika bidhaa zinazoweza kuzalishwa kutokana na gesi ikiwemo mbolea, lakini inaonekana Serikali bado ni kikwazo kutokana na kuchelewesha baadhi ya maamuzi.
Anasema hadi sasa uwekezaji katika utengenezaji wa mbolea inayotokana na gesi umekwama kwa sababu Serikali imekuwa ikisita kutangaza bei ya gesi yake kwa ajili ya shughuli za uzalishaji hasa wa mbolea.
Anasema ili kuharakisha na kuondoa kikwazo kwa wawekezaji, Serikali inahitaji kufanya maamuzi ya haraka kuhusu bei nya gesi ili kuruhusu kuendelea kwa uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na gesi hapa hapa nchini.
“Tunataka maamuzi ya haraka ili tujue kuwa bei ya gesi ni kiasi gani ili na viwanda navyo vijue gharama zake za uzalishaji na vianze kuzalisha hasa vile vya mbolea. Bado tunasumbuliwa na hawa wawekezaji wakitaka kujua iwapo Serikali imeshaamua bei ili waendelee na shughuli zao lakini suala hilo bado, hivyo tunataka maamuzi ya haraka,” anasema.
Anasisitiza kuwa kuchelewa kutangazwa bei ya gesi kunachelewesha uwekezaji huo na kuzuia kuanza kwa viwanda hasa vya mbolea, bidhaa muhimu kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini hasa ikizingatiwa kuwa mbolea inayotumika nchini kwa sasa inaagizwa kutoka nje.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba anasema kwa sasa wanafikiria kuanzisha mradi mpya wa kupeleka gesi kwenye vituo vya biashara vinavyowakutanisha wafanyabiashara wengi kama ilivyo katika soko la samaki la feri jijini Dar es Salaam na katika maeneo ya makazi.
Anasema kwa sasa, mipango iliyopo ya uwekezaji katika eneo hilo ni kuangalia sehemu yoyote yenye kamkusanyiko ka watu wengi kwa pamoja kisha kuwawekea mabomba kwa ajili ya kuwasambazia Gesi ya Asili (CNG) katika mabomba katika maeneo ya biashara na makazi.
Anasema mradi huo utasambazwa katika miji yote mikubwa kwa kuangalia vituo vyote vya biashara vinavyohitaji nishati ya gesi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao kwa gharama nafuu na kuepuka matumizi ya kuni na mkaa.
Alisema upo pia mpango wa kukaribisha wawekezaji binafsi ambao ni wasambazaji binafsi watakaokuw awakitumia magari kusambaza katika vituo, watakaofanya kazi kwa ubia katika wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, Ubungo na Kigamboni.
Anasema katika kuhakikisha uwekezaji wao unafanikiwa, kwa sasa wanafanya utafiti katika mikoa saba ambayo wanataka kuifanya ya mfano hasa wakizingatuia masuala ya uwezo wa watumiaji na masoko, ambayo ni Mwanza, Dodoma, Tanga, Arusha, Morogoro, Kilimanjaro na Mbeya ambayo itaisha Desemba mwaka huu.
“Kwa miaka miwili ijayo tunatarajia tutakuwa tumeanza vizuri katika mkoa wa Dodoma, ambapo tunaona tutaweza kufanya biashara vizuri kwa kuwa utakuwa mji wa kisasa uliopangiliwa kisasa zaidi, kwa hiyo itakuwa ni rahisi kwetu kupita na kupitisha mabomba maeneo yote,” anasema.
Anaelezaa kuwa katika mji huo itakuwa rahisi kusambaza gesi kutokana na miundombinu yake kuwa ya kisasa zaidi tofauti na ilivyo Dar es Salaam ambayo kutokana na mpango miji wake maeneo mengi ukitaka kupita lazima ubomoe baadhi ya ameneo, suala lilaokuwa gumu kutokana na kuhitajika malipo ya fidia katika baadhi ya maeneo.
Anasema anaamini kazi hiyo kwa Dodoma itakuwa ni nyepesi na kuanzia mwaka ujao wa fedha, 2019/20 wataelekeza nguvu zao huko baada ya utafiti wao wanaoendeela kuufanya kukamilika Desemba mwaka huu.
Akizungumzia maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais-Mazingira, January Makamba anasema mafanikio katika sekta hiyo yanategemea uwezo was Serikali kujua gharama za miradi, ili kuweza kukokotoa faida ya rasilimali hizo kwa taifa.
Makamba anaema uwezo huo ndio utakaoainisha faida inayoweza kupatikana na kunufaisha taifa, kutokana na uvunaji wa rasilimali hizo kuwa jambo jipya katika nchi za Afrika, ambazo kutokana na teknolojia duni kampuni nyingi zinazowekeza zinatoka katika mataifa ya ulaya.
“Bara la Afrika kwa sasa linaonesha linaelekea kwa kasi katika uchumi wa mafuta na gesi. Tatizo linaloonekana ni suala la gharama za miradi hii ya utafiti na uchimbaji, ambazo kama serikali zisipokuwa makini kuzijua inaweza isiwe na manufaa kwa wananchi,” anasema.
Anaongeza kuwa suala la kubaini gharama halisi za miradi zinazotumiwa na wawekezaji ambao ndio wenye teknolojia ya uchimbaji na miradi mikubwa inayohitajika ndiyo nyenzo muhimu ya kukokotoa namna ya kupata faida.
Makamba anasema Serikali imekuwa ikiendelea kufanya mabadiliko ya sheria na kuweka mipango na mikakati ya kwa ajili ya kuhakikisha matumizi ya rasilimali ya gesi na mafuta yanakua na manufaa kwa taifa
Anafafanuakwamba soko la mafuta na gesi duniani linakua kwa kasi hivyo ni vyema kujipanga vizuri na kwamba kasi ya maendeleo duniani pia inaathiri soko hilo, ikiwamo mwenendo wa siasa na uchumi katika mataifa yote ambao unaathiriwa pakubwa na ukuaji wa soko hilo.
“Pamoja na mwelekeo wa soko kupanda na kushuka katika vipindi tofauti, mwelekeo ni mzuri kwa nchi za Afrika na kwa nchi yetu pia, hivyo suala la muhimu ni sisi kujiandaa tu ipasavyo,” anasema.
Makamba anasema kuwa kwa sasa, ukiacha vyanzo vingine taifa linategemea mafuta na gesi kuzalisha asilimia 53 ya nishati yake, ambayo lazima ihusishe sekta binafsi na kwamba pamoja na kuzalisha nishati, mipango inaendelea kwa ajili ya kutumia gesi asilia kuzalisha mbolea kwa ajili ya matumizi ya kilimo.
“Kwa sasa asilimia 95 ya mbolea inaagizwa nje, kwa hiyo iwapo mipango hiyo itakamilika tutaweza kuzalisha mbolea ya kutosha hapa hapa nchini na kusaidia kukuza uchumi wetu,” anasema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi nchini (ATOGS), Abdulsamat Abdulrahim anasema kupitia kongamano hilo, wadau wote waliokusanyika wanaibua namna eneo hilo lilivyo muhimu na kuonesha fursa mpya ya uwekeaji kwa wawekezaji wakubwa duniani.
“Kuna zaidi ya mashirika na kampuni 75 kutoka maeneo mbalimbali duniani ambao wengine wamekuja na ndege zao binafsi. Wote wenye miradi mikubwa ya mafuta na gesi wako hapa, hivyo Watanzania tunatakiwa tuitendee nchi haki, tujitokeze na sisi nankuchangamkia hizo fursa,” anasema.
Abdulrahim ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Pietro Fiorentini Tanzania anasema ujio wa wawekezaji hao ni ishara ya umuhimu wa Tanzania katika jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa mafuta na gesi duniani, suala linalohitaji ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi ili kuinua uchumi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu anasema Serikali imeweka mazingira mazuri kuhakikisha wadau wote wapya wa masuala ya nishati wanaojitoleza wanapokelewa.
Anasema kwa sasa wanategemea karibu asilimia 50 ya nishati kutoka katika vyanzo vya mafuta na gesi, hasa katika gesi inayotoka Songosongo na Mnazi Bay.
Waziri wa Nishati, Medard Kalemani anasema ni lazima Watanzania watambue kuwa uwekezaji katika sekta hizo unahitaji teknolojia kubwa na uwezo mkubwa wa mtaji. “Kupata mafuta siyo jambo dogo. Unaweza ukatafuta mafuta kwa miaka 20 na usipate.”
Hata hivyo, anasema Serikali imeendelea kufanya jitihada za makusudi katika kuwawezesha Watanzania kunufaika na sekta hiyo na kuweka mfumo wa será inayowapa kipaumbele wazawa kushiriki katika uwekezaji.
Pia, anasema Serikali imeweka mfumo wa kisheria unaoweka mazingira rafiki kwa watanzania kuweza kushiriki katika uwekezaji.
“Mathalani, kwenye Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, tumeweka kipengele mahsusi kinachomtaka mwekezaji wa nje amshirikishe Mtanzania kwa hisa zisizopungua asilimia 25,” anafafanua.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Hamisi Mwinyimvua, anasema Serikali imepata fursa ya kunadi fursa za uwekezaji kwa wadau walioshiriki kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Tumeeleza utayari wetu wa kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji kwenye sekta hizi muhimu za mafuta na gesi. Pia, tumeweza kubadilishana mawazo na uzoefu. Ni matarajio yetu kupokea maombi mengi zaidi ya uwekezaji, hali ambayo italinufaisha Taifa,” anasema.