33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

SARATANI YA BEGA ILIVYOMUANZA MARIAM HADI KIFO CHAKE

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


“HUYU ni mwanangu wa saba na wa mwisho katika uzao wangu, naamini atakuja kuwa mkombozi katika maisha yetu, alipozaliwa hakuwa na tatizo lolote kiafya.

“Lakini kuna siku moja nilimtuma dukani aende kununua kiberiti wakati anarudi nyumbani alianguka ghafla na kujikuta amekaa kitako, tangu wakati huo alianza kuhisi maumivu makali ya bega ambayo yaliongezeka siku hadi siku.

Ni mazungumzo kati ya MTANZANIA na Bernadeta Raymond  yaliyofanyika ndani ya wodi ‘Wing 4B’ iliyopo jengo jipya la MOI Phase III katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu, Ubongo na Uti wa mgongo Muhimbili (MOI.

Bernadeta alilazwa wodini humo akimuuguza mwanawe  Mariam Sandali (17) kabla ya kupewa rufaa kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa matibabu zaidi hata hivyo alifariki dunia.

Bernadeta anasema kwa zaidi ya mwaka mmoja, enzi za uhai wake, Mariam alilazimika kulala kitandani muda mrefu huku akikabiliana na maumivu makali yaliyotokana na uvimbe mkubwa uliokuwa umeota katika sehemu ya bega lake la kulia.

Anasema hali hiyo ilimsababishia mwanawe kushindwa kuhudhuria masomo ya kidato cha pili katika Shule ya Sekondari King David mkoani humo tangu Machi, 2017.

“Walimu wake walikuwa wanakuja nyumbani kumsalimia, ana uwezo mkubwa darasani alikuwa anashika nafasi ya nne kwenda juu na ana uwezo kuzungumza lugha ya Kichina, alikuwa akizungumza na walimu wake.

Januari 21, mwaka huu, mwili wa Mariam ulipumzishwa  katika nyumba yake ya milele huko nyumbani kwao Masasi mkoani Mtwara.

 

Daktari

Julius Mwaiselage ni Mkurugenzi wa ORCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, anasema kifo hicho kilitokana na ugonjwa wa saratani ya bega.

“Kwa kuwa walichelewa kumleta hospitalini, tulipomfanyia uchunguzi tulibaini ugonjwa ulikuwa umefika hatua ya nne na tayari ulikuwa umesambaa katika mifupa, mapafu na mbavu,” anasema.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye ndiye aliagiza Mariam kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu, anasema taarifa za kifo hicho zimemsikitisha mno.

“Inasikitisha, walijitokeza wakati wa dakika za mwisho, msaada wetu haukuweza kuokoa maisha yake, tutaongeza jitihada zaidi kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuwahi hospitalini kwa uchunguzi wa awali.

“Pia kuzingatia ushauri na maelekezo wanayopewa na madaktari ikiwamo kuzingatia matibabu na si kwenda nyumbani kukaa na mgonjwa,” anasema.

 

Chanzo chake

MTANZANIA limefika na kufanya mazungumzo ya kina na madaktari bingwa wa saratani wa ORCI kuhusu ugonjwa huo ambao wanaeleza kwa kina juu ya tatizo hilo.

Dk. Mark Mseti anasema saratani ni jina lililotungwa na wataalamu likiwa na mkusanyiko wa kundi la magonjwa mengi yanayofanana kwenye njia kuu mbili.

“Kwanza ni kule kukosekana kwa udhibiti wa kuzaliana kwa seli au chembechembe hai za mwili, pili ni kutodhibitiwa kwa chembechembe hai zinazozaliana kwa wingi ambazo husafiri kutoka zilipozaliwa kwenda sehemu mbalimbali za mwili,” anasema.

Anasema chembechembe hizo huendelea kuota na kusambaa zaidi katika sehemu zingine za mwili kwa sababu zinakosa udhibiti.

“Sasa itategemea seli hizo zitaenda kuzaliana kwa wingi katika sehemu gani ya mwili… inaweza kuwa begani au sehemu yoyote ya mwili, ikizaliana begani ndipo tunasema saratani ya bega,” anasema.

Anaongeza: “Yaani saratani hupewa majina kulingana na mahala ambapo imetokea katika mwili wa binadamu.

 

Zipo zaidi ya aina 200

“Aina hizo hutokana na majina ambayo hupewa kulingana na mahala (sehemu ya mwilini) ambapo saratani imejitokeza,” anabainisha Dk. Crispin Kahesa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani katika taasisi hiyo.

 

Takwimu za dunia

 

Dk. Kahesa anasema mwaka 2000 takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilibainisha kuwapo kwa wagonjwa wapya milioni 10 duniani.

“Hivi sasa idadi imeongezeka na kufikia wagonjwa zaidi ya milioni 14, kati yao wagonjwa milioni 8.5 hufariki dunia kila mwaka,” anasema.

Anasema saratani ya mapafu, tezidume na njia ya mfumo wa chakula ndizo zinazotesa zaidi wanaume huku saratani ya matiti, shingo ya kizazi na utumbo mkubwa zikiwatesa zaidi wanawake.

 

Hali ilivyo Tanzania

Dk. Kahesa anasema saratani ni ugonjwa unaotajwa kuathiri zaidi nchi zilizopo katika uchumi wa kati na chini kuliko zile zilizopo katika uchumi wa juu.

Anasema kila mwaka zaidi ya watu 50,000 nchini hupata magonjwa ya saratani na kwamba hiyo ni idadi kubwa.

“Changamoto iliyopo ni kwamba kati ya hao ni asilimia 12 pekee ndiyo wanaokwenda hospitalini kufuata matibabu.

“Hapa ORCI tunaona wagonjwa wapatao 6,000 kwa mwaka, ni idadi ndogo, hali hii inachangiwa na sababu kadhaa… bahati mbaya Waafrika, Watanzania tuna mila na tamaduni nyingi.

“Ukiwauliza wagonjwa wengi utabaini wengi wao waliokuja hospitalini tayari walikuwa wamezunguka huku na huko kutafuta matibabu.

“Wapo ambao walianza kuwaeleza marafiki, ndugu na jamaa, wengi huona ni ugonjwa wa ajabu, wanashauriwa kununua dawa na kuanza kujitibu wenyewe majumbani.

“Wapo wanaokwenda kwenye maombezi, wengine kwa waganga wa kienyeji, wanasema safari ya matibabu ya saratani Tanzania ni ndefu… hadi aje afike kwetu (hospitalini) ugonjwa unakuwa umeshasambaa na upo katika hatua ya mwisho, ambayo ni ngumu kuutibu na wapo ambao hukata tamaa na kukaa nyumbani,” anabainisha.

 

Visababishi

Anasema zipo sababu nyingi zinazochangia hali hii ikiwamo ulaji usiofaa, matumizi ya pombe, kutokufanya mazoezi na hali ya umasikini.

“Matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku nayo inatajwa kuwa kisababishi, lakini mtindo wetu wa maisha umebadilika, zamani sisi tulikuwa tunalima zao hilo lakini hatutumii bidhaa zake.

“Leo hii zinatumika nchini hasa na kundi la vijana ambao tunawategemea kwa sababu ni nguvu kazi ya Taifa, lakini utaona hata matangazo yanatengenezwa kuwavutia,” anasema.

Anasema sigara ni miongoni mwa chanzo kikuu cha saratani na kwamba vipo pia visababishi vingine kama vile uchafuzi wa hali ya hewa na maji.

“Hatuli vyakula bora vya asili, wengi leo wanapenda kula vyakula vilivyo na kemikali nyingi lakini pia umri nao ni miongoni mwa visababishi vya magonjwa haya.

“Jinsi umri unavyosonga mbele, ndivyo mtu anakuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani, kwa sababu unapovuta sigara leo kwa kawaida athari yake huwezi kuipata papo hapo, itakuchukua miaka kadhaa,” anasema.

Anasema hilo linaweza kuthibitika kwa kuangalia orodha ya wagonjwa wao, kwamba wengi wanaofika kliniki huwa na umri wa zaidi ya miaka 50.

 

Watoto hatarini

Dk. Kahesa anasema jamii inapaswa kuwa makini katika malezi ya watoto kwa kuhakikisha wanakula vyakula bora  na si bora vyakula.

“Wapatie vya asili zaidi na si vya viwandani, leo hii wengi ukiwatazama utaona wana miili na uzito mkubwa kuliko umri wao, ni hatari ikiwa hatutachukua hatua, tutajikuta wakiugua magonjwa mengi ikiwamo ya saratani maishani mwao.

“Hata vijana wapo ambao ukiwatazama utaona wamezeeka lakini kumbe bado, tuzingatie chakula na vinywaji tunavyokunywa kwani tunaweza kupata athari katika miili yetu, lazima tuielimishe jamii.

“Wagonjwa wengi wanaokuja kwetu ni wanawake na wengi wana saratani ya shingo ya kizazi, utaona katika jengo letu la ghorofa tatu, ghorofa mbili zinatumika kuwahudumia wao pekee.

“Kina baba si wengi wanaokuja hospitalini, hata kuja kufanya uchunguzi wa awali tuliliona hilo kwamba bado wana mwamko mdogo, tukaanzisha kliniki maalumu kwa ajili yao na sasa wameanza kuitikia wito,” anasema.

 

Uchunguzi

Dk. Mseti anasema ili kufanya uchunguzi vipo vipimo mbalimbali ambavyo hutumika kikiwamo cha damu (full blood picture) katika kufanya uchunguzi pamoja na mashine nyinginezo kikiwamo cha ‘tumor marker’, Ct Scan, MRI, Borne scan na Pet Scan.

“Kipimo cha Pet Scan kwa sasa bado hatuna, lakini tayari serikali imedhamiria kukinunua na kitafungwa hapa, ni kipimo muhimu mno katika kufanya uchunguzi, hivi sasa tunalazimika kuwapa rufaa wagonjwa kwenda nje ya nchi kufanya kipimo hiki ambacho hutumia gharama kubwa,” anabainisha.

 

Matibabu

Dk. Mseti anasema hutegemea na hatua ya mgonjwa na kwamba kabla ya kumpatia matibabu dhidi ya saratani inayomsumbua, huwa wanajadiliana naye njia ipi hasa anaona inafaa kwa matibabu yake.

“Tiba ya awali kabisa ni upasuaji ndiyo maana tunahimiza watu wafanye uchunguzi wa awali kwa sababu mtu akichelewa inabidi tutumie ama tiba ya mionzi, chermo therapy (dripu), hormonal therapy (vichocheo) na immune therapy kumtibu,” anasema.

 

Hatua zaidi

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa Yasiyokuwa ya Kuambukiza (NCDs) wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mariam Kalomo anasema  saratani ni miongoni mwa magonjwa yaliyowekwa katika kundi hilo la magonjwa.

“Kwa kuwa hivi sasa kasi ya magonjwa haya ni kubwa ukilinganisha na magonwja ya kuambukiza, wizara tumeweka mikakati ya kukabiliana nayo,” anasema.

Anataja mikakati hiyo kuwa ni kuanzisha jamvi la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali zikiwamo wizara na taasisi nyinginezo ili kuweka nguvu ya pamoja.

“Tunaona Wizara ya Afya peke yetu hatuwezi kuyakabili, tutaungana na wizara nyingine ikiwamo ya Kilimo kwa sababu moja ya chanzo cha saratani ni matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku.

“Pia tutaungana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili wanapotaka kujenga barabara wahakikishe wanasimamia vema kunakuwa na sehemu maalumu za watembea kwa miguu ili watu waweze kufanya mazoezi.

“Watoto ni kundi pekee, wakipewa mafunzo ni rahisi kujenga utamaduni wa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi na kuepuka visababishi vinginevyo vinavyoweza kusababisha kupata magonjwa haya hivyo, tutashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika hili,” anabainisha.

 

Kozi maalumu

Anasema wizara ipo mbioni pia kuanzisha kozi maalum ya uuguzi ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambao watahudumia wagonjwa wa saratani pekee.

“Hii ni katika kuhakikisha wagonjwa hawa wanapata huduma bora inayohitajika, pia itaanzishwa kozi maalumu ya utoaji huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani.

“Pia tumepanga kuanzisha kanzi data ya Taifa itakayo kusanya takwimu zote za wagonjwa wa saratani nchi nzima tofauti na ilivyo sasa, kila hospitali inahifadhi takwimu zake yenyewe,” anabainisha.

 

Kuhusu maadhimisho

Dk. Kahesa anasema Februari, 4 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Saratani Duniani na kwamba ORCI wamepanga kufanya uchunguzi wa awali.

“Tunahimiza watu wajitokeze, tutafanya bila malipo uchunguzi huo ili wale watakaokutwa na dalili za awali waanze kupata matibabu mapema,” anatoa rai.

 

MWISHO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles