32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SARAKASI ZA UUNDAJI SERIKALI ZAENDELEA ITALIA

ROME, ITALIA


WAZIRI Mkuu mteule wa Italia, Carlo Cottarelli, ameonana na ofisi ya rais kwa mashauriano baada ya kukosa ushirikiano kutoka vyama vikubwa juu ya uundaji wa Serikali.

Hali hiyo imeleta athari katika masoko ya fedha na mitaji, sekta ambayo tayari imeathirika tangu Uchaguzi Mkuu wa Machi 4 ushindwe kutoa mshindi.

Cottarelli ambaye aliteuliwa na Rais Sergio Mattarella mapema wiki hii kuunda Serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mpya, amefanya mazungumzo na rais huyo katika Ikulu ya Quirinale mjini Roma.

Hakusema chochote wakati alipokuwa akiingia makazi ya rais, na wala ofisi ya rais haijatoa maelezo ya kina kuhusu mazungumzo baina ya viongozi hao.

Cottarelli alikabidhiwa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya Julai mwaka huu, lakini ameshindwa kupata ushirikiano kutoka vyama vikubwa.

Badala yake vyama hivyo vinamtaka Rais Mattarella kulivunja Bunge na kuitisha Uchaguzi Mkuu mpya mara moja, wakipendekeza ufanyike Julai 29, ikiwa ni chini ya miezi isiyotimia minne tangu uchaguzi wa Machi, ambao haukutoa mshindi wa wazi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Italia vinazungumzia uwezekano wa kupatikana mwafaka kati ya rais na vyama vyenye misimamo mikali ya kizalendo na vinavyopinga Umoja wa Ulaya.

Tofauti kubwa iliibuka baada ya hatua ya Rais Mattarella kukataa pendekezo la vyama hivyo vya Vuguvugu la Nyota Tano na League, la Paolo Savona kuwa waziri wa uchumi.

Savona mwenye umri wa miaka 81, anajulikana kwa msimamo mkali dhidi ya ushiriki wa Italia katika ukanda wa sarafu ya Euro.

Kiongozi wa Vuguvugu la Nyota Tano, Luigi di Maio, alisema wako tayari kuzungumza na pande zote kupata suluhisho la mgogoro unaoigubika nchi.

Wakati Cottarelli akijaribu kuunda Serikali yake ya mpito, zipo taarifa kuwa maofisa wa Vuguvugu la Nyota Tano na chama cha League wanajaribu kukubaliana juu ya mtu mpya wanayeweza kumpendekeza katika wadhifa wa waziri wa fedha badala ya Savona aliyeleta mtafaruku.

Taarifa hizo zimedai vyama hivyo vinatafakari kukishirikisha katika Serikali chama kingine chenye sera kali za mrengo wa kulia cha ‘Ndugu wa Italia’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles