KILA mtu atakuwa anafahamu namna picha za jela zilivyo kwa kuona mwenyewe kwa macho, kusikia au kuambiwa.
Lakini pia kuna hadithi za uwapo wa maisha ya kifahari katika baadhi ya jela hasa katika mataifa yaliyoendelea, ambazo si ajabu kuwasikia wabongo, au raia wengine wa Afrika wakisema wako radhi kufungwa humo, yote ikiwa kuchoshwa na ugumu wa maisha.
Hata hivyo, jela za aina hizo si nyingi duniani kulinganisha na zile za kawaida au za kutisha.
Wakati hali ikiwa hivyo, nchini India kuna magereza ya aina yake, ambayo hayafanani hata kidogo na jela.
Mfano ni jela ya Sanganer, iliyopo katika Mji wa Jaipur nchini India, wafungwa hupewa mahali pa kulala lakini hawapewi chakula na fedha.
Hiyo inamaanisha kuwa lazima watoke asubuhi kwenda kufanya kazi na kurudi jioni ili wapate kipato kwa ajili ya mahitaji na mkate wa kila siku.
Baadhi ya kazi wanazopata wafungwa hao ni kama vile vibarua, kazi za viwandani, udereva na hata ualimu wa Yoga.
Miongoni mwa simulizi za wafungwa hao ni kuhusu Ramchand na mkewe Sugna.
Mume hupeleka basi la shule na Sugna hufanya kazi katika kiwanda cha nguo mjini humo.
Wawili hao wanaishi jela humo kama mtu na mkewe na kifungo ndicho kilichowakutanisha humo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.
Nyumba yao ipo katika jela ya Sanganer Open mjini Jaipur, ambao ndio mji mkuu wa Jimbo la Magharibi mwa India la Rajasthan.
Jela hii haina maeneo ya kuwazuia kutotoka nje, haina walinzi katika lango lake kuu na wafungwa huruhusiwa na hata kushawishiwa kwenda mjini na kutafuta kazi.
Jela hiyo ambayo imekuwa wazi tangu mwaka 1950 ni nyumbani kwa wafungwa 450 na ni miongoni mwa jela 30 kama hizo katika Jimbo la Rajasthan.
‘’Naenda Sanganer, Smita Chakraburtty, mwanamke anayeoongoza kampeni za kuzifanya jela zionekane kuwa mahali pa kawaida,” anasema.
Amewasilisha ombi lake katika Mahakama ya Juu ya India, ambayo badala yake imeyataka majimbo kufungua taasisi zaidi kama hizo.
Kwa sasa, anahudumu kama kamishna wa magereza katika Jimbo la Rajasthan na hivi majuzi aliorodheshwa katika tuzo ya Agami kwa kazi yake nzuri ya mfumo wa jela nchini humo.
‘’Mfumo wa jela nchini humo unaangazia kuhusu kisa na haujui cha kumfanyia mtu,” anasema Chakrabutty.
Kampeni yake inaendelea kuwa maarufu na majimbo mengine manne nchini India yalifungua jela huru mwaka jana.
Katika jela hizo hakuna walinzi, mtu yeyote anaweza kuingia katika jela hiyo na wageni ni wachache mno.
Wafungwa wanapoulizwa kwanini wako jela wanajibu 302 wakielezea kuhusu kifungu cha 302 katika sheria za India ambacho kinasema wahalifu wa mauaji lazima waadhibiwe.
Wanaita jela hizo mashamba huru na kueleza namna ilivyorahisi kuishi hapo na namna wanavyofurahia maisha.
Ili kufika Gereza la Sanganer ni lazima wawe wamehudumia theluthi mbili za vifungo vyao katika jela za kawaida kabla ya kuhamishiwa hapo na wanasema wakilinganisha na jela hizo nyingine, hapo wapo huru.
Kutokana na kunogewa na maisha ya jela, Serikali ya Rajasthan mara nyingi hulazimisha kuwaondoa wafungwa, ambao wanakataa kuondoka baada ya vifungo vyao kuisha.
Wamepata kazi wakiwa hapo, wamepata shule kwa ajili ya watoto wao na hupata hesabu kama nyumbani.
Pamoja na hayo, wafungwa wengi hueleza namna wanavyopata changamoto kutokana na namna ambavyo huko uraiani huwachukulia.
Baadhi ya wanawake wafungwa wanasema ni rahisi kufunga ndoa na wafungwa wenzao kwa kuwa wanaume walio nje ya jela hiyo hawawaelewi vizuri.
Mara nyingine hata kupata kazi inaweza kuwa vigumu, wanasema kuwa watu wanaogopa kuwaajiri wanapotoa vitambulisho vyao.
Lakini bado wanaendelea kuishi maisha ya kawaida. Wananunua pikipiki, simu aina ya smartphone, runinga na hawavai magwanda ya jela na idadi ya watu wanaoishi katika nyumba walizopewa ni chache.
Kila mfungwa hupewa nyumba na serikali katika jela hiyo isipokuwa tu chakula, maji na kipato.
Hivyo basi, kila siku wengi wao huondoka katika jela hizo ili kutafuta kipato.
Wanaume waliopatikana na hatia ya mauaji hufanya kazi kama walinzi, wafanyakazi wa viwandani ama vibarua.
Unaweza kukutana na mfungwa ambaye ni mwalimu wa kufunza yoga na mwingine ambaye ni msimamizi karibu na shule moja.
Sheria iliyopo ni kwamba wafungwa lazima wahesabiwe kila jioni.
Wakati jua linapozama, wawakilishi wa serikali katika jela hiyo husimama mlangoni na mfungwa mmoja aliye na kipaza sauti huanza kuita namba zao moja hadi 450.
Kila mfungwa hutakiwa ahakikishe usafi wa maeneo yake, vinginevyo huweza kurudishwa katika jela ya kawaida.