Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayechezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, sasa yupo fiti kurejea dimbani baada ya kupona majeraha ya nyama za paja yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Mchezaji huyo bora wa Mazembe msimu uliopita, anatarajia kushuka dimbani Julai 20 mwaka huu akiwa na kikosi cha Taifa Stars kuivaa Msumbiji katika mechi ya raundi ya pili ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), huku pia akitarajia kuichezea Mazembe Julai 26 mwaka huu, itakapochuana na Zamalek kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa kutoka Mazembe zinaeleza kuwa Samatta yupo fiti kurejea dimbani sambamba na kiungo mwingine, Mghana Gladson Awako, ambao wote wamepona majeraha yao yaliyokuwa yakiwasumbua, huku kocha wao mkuu, Mfaransa Patrice Carteron, akifurahishwa na kurejea kwao.
“Mbwana Samatta na Gladson Awako wako vizuri hivi sasa na wanaweza kuendelea na majukumu yao ya uwanjani…” alisema daktari wa timu hiyo, Cesar Kabila.
Samatta anayechezea timu hiyo na Mtanzania mwingine Thomas Ulimwengu, kwa sasa wapo mapumzikoni nchini na watajiunga na Mazembe kabla ya Alhamisi hii kambi ya timu hiyo itakapoanza.