30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Samaki ajabu aonekana Kilwa

samaki

NA EVANS MAGEGE

SAMAKI mkubwa na wa ajabu ambaye aina yake hajatambulika mara moja ameonekana katika fukwe ya Bahari ya Hindi katika eneo la Kilwa Masoko, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa watu waliomshuhudia samaki huyo ambaye ana ukubwa wa kontena na urefu wa futi 25 wanasema ameonekana akiwa tayari amekufa.

Mkuu wa Wilaya la Kilwa, Christopher Ngubiagai ambaye ni miongoni mwa watu waliofika kumuona samaki huyo aliliambia gazeti hili kuwa inavyoonekana samaki huyo alinasa katika pwani hiyo usiku wa kuamia jana.

Ngubiagai alisema, taarifa ya awali aliyopewa na wataalamu wa masuala ya uvuvi imeonyesha kuwa samaki huyo alinasa akiwa hai na alikufa saa chache baada ya kukosa maji.

Alisema wataalamu hao wamemwambia kuwa samaki huyo inawezekana alipotea njia wakati anapita katika mkondo wa kina kirefu cha maji ambao hutumiwa na samaki wakubwa kupita badala yake akajikuta amenasa katika sehemu ambayo maji yanakupwa.

“ Wataalamu wameniambia kuwa Samaki huyu katokea bahari kuu na kafuata mkondo unaotenganisha Kilwa Masoko na Kilwa Kisiwani ambapo kunamkondo wenye kina kirefu na huo mkondo inaonekana samaki hawa wakubwa huwa wanapita mara nyingi, yani ni kama njia yao fulani kwa kipindi fulani wanasafiri kutoka huko chini, Beira na Maputo wanapanda mpaka Mogadishu na wanashuka kuelekea sehemu mbalimbali za Bahari ya Hindi.

“ Sasa alivyopita samaki huyu akakuta kuna  ile maji kupwa na kujaa, inawezekana maji kuwa machache yalimkwamisha kurudi kwenye maji mengi, pia mwili wa samaki huyu haujajeruhiwa sehemu yeyote, ukiangalia macho yake mwili wake pua yake hakuonyeshi kajeruhiwa,” alisema Ngubiagai.

Akizungumzia ukubwa wa samaki huyo, Ngubiagai alisema kuwa amemshuhudia kwa macho samaki huyo na ukubwa alionao ni sawa na kontena la kubebea mizigo lenye urefu wa futi 25 (kutokea mkiani hadi mdomoni) na upana wake unafika futi kati ya 9 hadi 10.,” alisema.

Akisimulia ukubwa wake alisema, mtu akisimama ng’ambo ya kwanza hawezi kuona ng’ambo ya pili na wataalamu wa masuala ya uvuvi wamemwambia tukio kama hilo halijawahi kutokea katika eneo hilo.

“ Wataalamu wameniambia kuwa inawezekana samaki huyu alipotea njia wakati anapita katika eneo hilo au ni kupungua kwa kina cha maji aliyoyakuta ndio akapotea lakini vilevile kiumbe huyu ni kati ya wale viumbe adimu maana ukubwa wake, aina yake bado haijabainika rasmi ni samaki wa aina gani, kama ni nyangumi ni wa aina gani.

“ Kwa ujumla wataalamu wangu bado hawajatafsiri kama ni samaki wa aina fulani au ni nyangumi kwa sababu ana matezi kama kawaida, mkia, macho, mdomo mkubwa sana ambao haujachongoka kukata kama papa,” alisema

Alisema hata wataalamu wa uvuvi wanamshangaa samaki huyo kwa sababu hana sifa za nyangumi na wamesema inawezekana ni aina ya samaki wakubwa ambao ni tofauti baharini na imekuwa ngumu kumfananisha na papa au nyangumi.

“ Bado wanamfanyia uchunguzi, unajua amekwama usiku kwa hiyo mpaka asubuhi alikufa,” alisema.

Alipoulizwa  kama wananchi wameruhusiwa kumtumia kama kitoweo, Ngubiagai alisema ngozi ya samaki huyo ni ngumu zaidi ya tembo na wananchi wamejaribu kutumia visu, mapanga na shoka lakini vimeshindwa kukata.

“Ngozi yake ni ngumu na sehemu moja tu ilipasuka na anatoa damu nyingi sana sasa nadhani labda ni samaki anayezaa sijui anataga kwa sababu kamwaga damu nyingi sana pale kwenye eneo ambalo amenasa,” alisema.

Alisema kwa mantiki hiyo, amewakataza wananchi kukata au kuchukuwa nyama  ya  samaki huyo kwa sasa hadi hapo wataalamu wa uvuvi watakapothibitisha kuwa nyama hiyo iko salama kwa matumizi ya binadamu.

Mwaka 2014 mzoga wa samaki mkubwa aina ya nyangumi ulionekana  katika Bahari ya Hindi karibu kabisa na ufukwe wa mji wa Msangamkuu uliopo mjini Mtwara.

Tukio kama hilo lilitokea mwaka 2012 ambapo mzoga wa samaki aina ya  nyangumi ulikutwa katika ufukwe wa pwani ya Coco Beach,  jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles