24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Butiku: Rais tembo hatufai

jbutiku

Na JONAS MUSHI

DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema kutokana na miiko iliyowekwa na mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julias Nyerere, mtu yeyote anayekuwa rais wa nchi lazima atambue watu wote ni sawa na “usiwe wewe ni rais tembo.”

Hayo aliyasema jana wakati akiwasilisha mada ya miiko ya uongozi katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya TANU ya mwaka 1954 imani ya chama ilikuwa binadamu wote ni sawa, kila mtu anastahili heshima na kwamba kila raia ni sehemu ya Taifa.

Alisema nchi ambayo mwalimu aliijenga ilikuwa na misingi ya “binadamu wote ni ndugu zangu” na kwamba msimamo kama huo aliuweka hata alipotoka nje ya mipaka ya Tanzania.

“Tunachosema ni kwamba miiko ilikuwa inasema ukitaka kuwa rais utambue na uwe na imani kuwa watu wote ni sawa usiwe wewe ni tembo,” alisema Butiku na kuongeza:

“Lazima utambue kuwa unatokana nao (watu) na lazima kiongozi huyo atambue kuwa anaongoza watu hivyo anapaswa kuwaongoza kwa heshima.”

Akizungumzia miiko ya uongozi, Butiku alikumbusha hoja ya kutenga siasa na biashara ambayo alisema imeonekana kupuuzwa na viongozi katika miaka ya hivi karibuni.

Alisema miiko ya uongozi ilikuwa  ni pamoja na kiongozi lazima awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika shughuli zozote za ubepari.

Katika hilo aliwataka viongozi kuchagua ama kuwa kuwatumikia watu au kutafuta utajiri.

“Katika siasa za hivi sasa wanasiasa wote wanajitahidi sana kukataa kanuni hii na wamekuwa wakibabaisha. Msibabaishe,” alisisitiza Butiku.

 

Mbali na Butiku, naye Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mkama wakati akiwasilisha mada ya miiko ya uongozi alibainisha kuwa viongozi lazima wapatikane kwa haki na uwazi.

Alionya kuwa ni hatari kwa viongozi kupatikana kwa njia za vitisho, ujanja, ulaghai na rushwa na kwamba kufanya hivyo ni kupoteza sifa za uongozi.

“Asili ya uongozi ni watu na viongozi lazima wapatikane kwa haki na uwazi na si kwa njia za ujanja ujanja, vitisho, ulaghai na rushwa na inapokuwa hivyo tunapoteza sifa ya uongozi,” alisema Mkama.

Pamoja na hilo Mkama alipongeza kauli mbiu inayotumiwa na Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi tu’ akisema kiongozi lazima afanye kazi kwa kufuata utaratibu wa kisiasa uliowekwa.

“Watu wamekuwa wakitafsiri siasa vibaya lakini ukweli ni kwamba siasa ni namna ya kutengeneza utaratibu wa maisha na maamuzi ya kisiasa ndio yanayoijenga jamii,” alisisitiza.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philip Mangula, akiwasilisha mada ya ‘Viongozi na Maadili’ alisema kwa kiasi kikubwa chama chake kimekuwa kikizingatia maadili ya viongozi.

Alisema kwa sasa chama hicho chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli kinahakikisha kinatokomeza rushwa serikalini na katika chama hasa wakati wa uchaguzi.

“Katika mkutano Mkuu wa mwaka 2012 ambao ndio ulinichagua kuwa makamu mwenyekiti na nikapata uenyekiti wa kamati ya maadili, tuliazimia kuchukua hatua haraka kwa viongozi wala rushwa na ndio kazi anayofanya Rais Magufuli,” alisema Mangula.

Mangula ambaye amepewa jina la utani la ‘Mzee wa mafaili’ kutokana na timu yake kujihusisha na uchunguzi wa masula yote yanayohusu maadili hasa kwa wanachama wanaotaka uongozi kupitia  CCM, alisema mafaili bado yanaendelea kurekodiwa na mwisho yatafunguliwa kwa kila atayetaka uongozi.

Alionya kuwa wapo watu ambao wameshaanza kutoa zawadi na misaada bila kuzingatia taratibu za chama kwa lengo la kutengeneza mazingira ya kupata uongozi katika uchaguzi ujao na kusisitiza kwamba “safari hii imekula kwao.”

Kauli hiyo ya Mangula inafanana na ile aliyoitoa Rais Magufuli Julai mwaka huu baada ya kukabidhiwa mikoba ya Uenyekiti wa chama hicho mjini Dodoma.

Rais Magufuli alitangaza kufanya mapinduzi makubwa ya kimfumo ndani ya CCM ikiwa ni pamoja na kukomesha uongozi unaopatikana kwa njia ya rushwa.

Magufuli ambaye amekuwa akijinasibu kupambana na rushwa na ufisadi alikitaja waziwazi chama hicho kama moja ya taasisi zinazotajwa kuongoza kwa rushwa licha ya kukatazwa katika ahadi ya tatu ya CCM pamoja na kifungu cha 18 cha Katiba ya CCM.

“Niligombea urais niliyaona huko Iringa wakati wa kutafuta wadhamini, Wilaya yote ilikuwa imenunuliwa ilibidi nisafiri kwenda ndani huko vijijini. Fedha imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi…ukitaka urais kiasi fulani, ubunge kiasi fulani, diwani kiasi fulani. Tumekuwa tukipoteza sehemu zingine kuchagua wenye pesa badala ya anayekubalika,” alikaririwa Magufuli.

Alisema amedhamiria kukomesha jambo hilo na kwamba mtu atakayetoa rushwa hatachaguliwa wala kupitishwa kwa mujibu wa kanuni ambazo alikabidhiwa jana na Mwenyekiti mstaafu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles