Na JOACHIM MABULA,
KUKOSA hamu ya ngono ni tatizo ambalo wengi huona aibu kulizungumzia ingawa ni kitu kinachowanyima raha wanawake wengi. Inakadiliwa kuwa asilimia 40 ya wanawake hupatwa na tatizo hili katika maisha yao, hata hivyo tatizo hili huwapata zaidi wanawake wenye umri kati ya miaka 45 na 65.
Wataalamu wengi wa afya huwaambia wanawake wenye tatizo hili kuwa wana matatizo ya homoni. Kuwa na homoni za kutosha katika mwili ni muhimu kwa tendo la ndoa. Homoni iitwayo istrojeni huhamasisha damu kwenda kwenye uke na kusaidia kulainisha uke wakati homoni iitwayo testosteroni huchochea hamu ya ngono. Hata hivyo, hamu ya ngono kwa wanawake ni kitu chenye utata mwingi kwa maana msongo wa mawazo, mkazo, afya yake na uhusiano aliopo huchangia kuwa na hamu au kutokuwa na hamu ya tendo la ndoa.
Wanawake wengi mwanzo wanakuwa wanafanya ngono mara tano kwa wiki na baadae hamu hupotea na kuanza kufanya ngono mara moja kwa mwezi tena kwa kujilazimisha. Tatizo hili linaweza kuanza kwa mwanamke kukosa msisimko (raha ya tendo), kutofikia kileleni au kufika kileleni na kushindwa kuendelea na tendo la ndoa baada ya mzunguko mmoja.
Wanawake walio katika hatari ya kupata tatizo hili
Wanawake ambao waliwahi kupatwa na tatizo la kupungua hamu ya kujamiiana hapo mwanzo wanaweza kupatwa na tatizo hili kwa mara ya pili. Wale ambao wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa mayai yao ya uzazi kutokana na sababu mbalimbali kama magonjwa au uzazi wa mpango. Wanawake ambao waliofika umri wa kukoma hedhi mara nyingi huanzia kati ya miaka 45 na 55 ingawa kuna wachache huanza kabla ya umri huo.
Matatizo ya homoni si chanzo pekee cha kukosa hamu ya ngono. Sababu zingine ni pamoja na:
Mzunguko mbovu au kukosa kabisa hedhi
Ikiwa mwanamke ana mzunguko wa kati ya siku 24 hadi 34 ni dalili kuwa ovari na homoni zake zinafanya kazi vizuri. Mzunguko mbovu wa hedhi au kutopata kabisa hedhi huwa ni ishara kuwa homoni za mwanake haziko vizuri. Kukosa hedhi kwa zaidi ya miezi sita ni ishara kwamba hakuna uwiano mzuri wa homoni ya istrojeni. Tatizo hili linaweza kuathiri tendo la ndoa hivyo ni vyema kumuona daktari kwa msaada zaidi.
Kukoma hedhi (Menopause)
Baada ya hedhi kukoma, ovari za mwanamke huacha kutengeneza homoni, hivyo kiasi cha homoni ya istrojeni na istrojeni hupungua na wakati mwingine huisha kabisa. Wanawake wengi katika kipindi hiki hupatwa na shida ya uke kukauka (kukosa ute wa kutosha) na kupungua hamu ya tendo la ndoa. Kupungua kwa homoni ya istrojeni husababisha nyama ya uke kuwa nyembamba na kukauka hivyo kusababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Ikiwa tendo la ndoa litasababisha maumivu kwa mwanamke hatataka kufanya tendo hilo mara kwa mara na jinsi anavyofanya mara chache ndivyo tatizo linavyozidi kukua. Wakati mwingine tatizo la uke kukauka linaweza kutatuliwa kwa kupaka mafuta ya kulainisha uke au mafuta ya nazi. Matumizi ya virutubishi vya homoni ya testosterone yanaweza kusaidia na kuongeza hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake waliokaribia kukoma hedhi na wale waliokoma, ingawa virutubisho hivi huweza kusababisha chunusi, kuota nywele mwilini na huongeza kiwango cha lehemu (cholesterol) kitu ambacho kinaweza kusababisha matatizo ya moyo.
Matatizo ya kihisia
Kuwa na wasiwasi, msongo wa mawazo na mikazo katika maisha ambayo huchangiwa na matatizo ya uchumi, matatizo katika uhusiano kama ugomvi, kutoelewana, kutoaminiana huathiri mwili na kufanya homoni muhimu kwa ajili ya tendo la ndoa kutotengenezwa kwa kiwango cha kutosha. Pia mzunguko wa damu katika tupu ya mwanamke hupungua na hivyo kusababisha maumivu wakati wa kujamiiana. Historia ya kubakwa au kupata maumivu wakati wa kujamiiana hapo awali kutokana na mwanamke kutokuwa tayari au kutotayarishwa vyema husababisha uke kuwa mdogo kuruhusu uume kupita, tatizo ambalo kitaalamu huitwa vaginismus.
Matumizi ya vilevi
Matumizi ya dawa za kulevya na unywaji pombe kupita kiasi hupunguza hamu ya tendo la ndoa, ingawa kuna baadhi ya watu huamini kuwa unywaji pombe kali huongeza hamu ya kujamiiana au kupunguza uzito. Pombe kali au kilevi cha aina yoyote vikitumiwa kupita kiasi hupunguza hamu ya kujamiiana na pombe huongeza uzito na kusababisha utapiamlo hasa kitambi.
Maradhi
Magonjwa kama kisukari, magonjwa ya mifupa (arthritis), magonjwa ya moyo, saratani ya aina yoyote ile, matatizo ya kupungua kwa homoni ya tezi la koo (hypothyroidism) ambayo hutokea zaidi kwa wanawake kuliko wanaume husababisha kupungua hamu ya tendo la ndoa.
Vilevile madhara ya dawa mbalimbali kama za kushusha shinikizo la damu na za saratani.
Ujauzito, kujifungua na kunyonyesha
Mwanamke anaweza kukosa hamu ya tendo la ndoa kutokana na mabadiliko katika mfumo wa homoni au vichocheo wakati wa ujauzito. Pia kutokana na mabadiliko ya maumbile ya wanawake wakati huo na kufanya mwanamke kutojiamini kufanya tendo la ndoa.
Mwanamke akijifungua na kuanza kunyonyesha homoni ya prolactin huwa katika kiwango cha juu. Homoni hii hufanya kazi ya kumfanya mtu kuridhika baada ya ngono/tendo la ndoa, hushirikiana na homoni/kichocheo nyingine iitwayo dopamine inayofanya mtu kufikia kilele wakati wa tendo la ndoa. Hata hivyo, homoni ya prolactin inaweza kuongezeka wakati mtu akiwa kwenye usingizi mzito hasa wakati wa alfajiri, baada ya kufanya mazoezi, kula, baada ya tendo la kujamiana, baada ya upasuaji mdogo na hata baada ya kupata degedege. Sababu zingine za kuongezeka kiwango cha homoni hii ni kuwa na saratani ya ubongo.
Vidonge vya uzazi wa mpango
Vidonge vingi vya uzazi wa mpango hugandisha homoni ya testosteroni kwenye mwili na huweza kusababisha kupungua kwa hamu ya ngono kwa baadhi ya wanawake. Ikiwa una hofu juu ya njia ya uzazi ya mpango yenye homoni ni vyema kuzungumza na daktari juu ya njia nyingine isiyokuwa na homoni. Usiache tu kutumia vidonge vya uzazi wa mpango kwa kuhisi ndio sababu ya wewe kutopata hamu ya tendo la ndoa bila kuzungumza na mtaalamu wa afya.
Mambo Mengine
Uharibifu wa neva inayohusika na kuongeza msisimko wakati wa kujamiana (pudendal nerve) wakati wa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi kwa mwanamke mwenye matatizo ya uzazi au katika mfuko wa kizazi. Uchovu mwingi baada ya majukumu ya kulea mtoto/watoto, kazi na kumhudumia mume wake. Matumizi ya vifaa vya kieletroniki kupita kiasi hasa uraibu wa mitandao ya kijamii kama Facebook & Instagram.
Kupenda kuchat au kutumia intaneti kupita kiasi na hivyo kusababisha msisimko kupotea kati ya wenza wawili mwishowe kupungua uwezo au hamu ya kujamiiana.
Ikiwa unapata hedhi katika mpangilio mzuri, husikii maumivu ukifanya tendo la ndoa na hautumii njia yoyote ya uzazi wa mpango yenye homoni basi tatizo lako la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa linaweza lisiwe tatizo la homoni moja kwa moja. Ni vyema kumuona daktari kwa msaada zaidi.