Na Shomari Binda, Musoma
WAKALA wa Maji Vijijini( Ruwasa) Wilaya ya Musoma, imesema miradi mbalimbali inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata maji, huku ikiiandikia barua TANROADS kutokana na changamoto za kupitisha mabomba katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kijiji cha Wanyere Kata ya Suguti, Meneja wa Ruwasa,Edward Sironga,amesema yapo maeneo ambayo mabomba yanapita barabarani na tayari wamewasiliana na TANROADS ili kukamilisha miradi hiyo.
Amesema Kata ya Suguti kuna mradi wa maji wa kuwafikishia wananchi majumbani lakini bado baadhi maeneo hajafikiwa kutokana na changamoto ya kupitisha mabomba barabarani.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, tumepewa zaidi ya bilioni nane kutekeleza miradi ya maji.
‘Tunamshukuru pia Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa jitihada zake za kuwafikishia wananchi huduma,”amesema Sironga.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Suguti wameshukuru kwa kufikishiwa huduma ya maji wakati kipindi cha nyuma waliyafuata zaidi ya kilometa 15.