26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wahenga Aluminium kuendelea kuboresha sekta ya elimu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Aluminium, John Ryoba, amesema ataendelea kutatua changamoto zinazokabili shule mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya ujifunzaji.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Aluminium, John Ryoba (Watano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu. (Wapili kulia) ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam, Hussein Njau.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 20 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Dar es Salaam amesema kila shule ambayo Mungu atamuelekeza kwenda kusaidia atakwenda na kwamba hatarajii kulipwa malipo ya aina yoyote ile.

“Hakuna kitu kikubwa duniani kinachonipa furaha kama kumsaidia mtu mwingine kwa sababu na mimi nilisaidia na watu hadi kufikia hapa nilipo.

“Kidogo nilichonacho najitahidi kugawana na wenzangu, zawadi pekee unayoweza kutoa hapa duniani ni kugusa maisha ya watu,” amesema Ryoba.

Katika mahafali hayo Ryoba ameahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo sambamba na kutoa nafasi mbili kwa wahitimu wa kidato cha nne kwenda kufanya kazi katika kampuni yake.

Naye Mkuu wa shule hiyo Hussein Njau, amesema kiwango cha ufaulu kwa miaka mitatu kimeongezeka kutoka asilimia 66.9 mwaka 2018 hadi asilimia 85.26 mwaka 2020 na kwamba mwaka huu malengo yao ni kufikia asilimia 90.

“Tumekusudia mwaka huu tukapate nafasi za juu kitaifa, wanafunzi wamefanya mitihani mingi zaidi ya ndani na tuna walimu wazuri wenye ushirikiano mkubwa,” amesema Mwalimu Njau.

Amesema pia wamekuwa wakitoa motisha kwa walimu wanaofaulisha kidato cha nne katika masomo mbalimbali ambapo mwanafunzi anapopata alama A mwalimu huzawadiwa Sh 10,000 na alama B huzawadiwa Sh 5,000. Katika mahafali hayo shule hiyo ilitumia zaidi ya Sh milioni 2.7 kuwazawadia walimu.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally, amesema malengo yao ni kuhakikisha jiji hilo linashika nafasi za juu katika mitihani ya kitaifa na kwamba hana mashaka na shule hiyo kutokana na juhudi kubwa wanazofanya.

Aidha amempongeza Ryoba kutokana na juhudi zake za kusaidia sekta ya elimu jijini Dar es Salaam na kuwaomba wadau wengine waige mfano huo.

“Naamini unachokifanya ni kwa nia njema ya kuleta maendeleo, tunapenda sana wadau wanaotusaidia kuboresha sekta ya elimu,” amesema Mwalimu Ally.

Akisoma risala ya wahitimu Kaka Mkuu wa shule hiyo Simon Bwanyire, amewashukuru walimu kwa kuwapatia msingi mzuri na kuahidi kuwa watafanya vema katika mtihani wa taifa.

“Walimu mmetupatia msingi mzuri sasa tunajitambua na kufanya maamuzi sahihi, tunawaahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu,” amesema Bwanyire.

Katika mahafali hayo pia wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma na kwenye maeneo mbalimbali walizawadiwa vyeti vya pongezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles