29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rufaa ya kina Mbowe kusikilizwa na wachache

 KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

WASIKILIZAJI kesi wakiwemo wafuasi wa Chadema hawataruhusiwa kuingia mahakamani kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba wakipinga hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 10.

Hayo yalibainishwa jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Lameck Mlacha wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Wakili Salim Msemo huku warufani wakiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.

Jaji Mlacha wakati akiahirisha kesi hiyo, alisema itasikilizwa Mei 13 mbele ya Jaji Ilvin Mgeta na itasikilizwa na warufani na mawakili wa pande zote mbili.

“Hawataruhusiwa wasikilizaji ama wanachama kuingia katika kusikiliza rufani hiyo,” alisema Jaji Mlacha.

Mbowe na wenzake nane Machi 10 walihukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 350 au kutumikia kifungo cha miezi mitano gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili.

Uamuzi wa kuwatia hatiani ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi.

Mbali na Mbowe, wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Ester Matiko.

Wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na aliyewahi kuwa Katibu wa chama hicho kabla ya kuhamia CCM, Dk. Vicent Mashinji.

Hata hivyo viongozi wote kwa nyakati tofauti walifanikiwa kulipa faini na kukwepa kutumikia kifungo hicho.

Katika rufaa yao iliyowasilishwa na Wakili Kibatala wametoa hoja 14 ambazo warufani hao wanapinga hukumu na adhabu dhidi yao.

Warufani wanadai mahakama hiyo ilifanya makosa ya kisheria kufikia maamuzi ya kesi ya msingi bila ya upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo shaka.

Wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kwa kushindwa kufanya uchanganuzi vizuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa.

Warufani wanadai mahakama ilishindwa kuainisha viini vya makosa dhidi ya mashtaka na kuwahukumu ndivyo sivyo na kutozingatia utetezi wa washtakiwa.

“Mahakama ilifanya makosa kwa mujibu wa sheria ya ushahidi wa kielektroniki kupokea kielelezo namba 4 na 5 na kufanya makosa ya kisheria kusikiliza kesi ya msingi huku ikitambua kuwa hati ya mashtaka ina makosa mengi ya kisheria.

“Mahakama imeshindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo au ushiriki wa baadhi ya watuhumiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye shtaka la 2, 3 na 4,” walisema warufani.

Wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kwa kuonyesha mrufani namba 2, 7 na 8 maneno wanayodaiwa kutamka katika shtaka la 11,12,na 13 ni makosa ambayo yalikuwa yanachochea kutendeka kwa kosa la jinai.

Sababu ya mwisho warufani wanadai hakukuwa na maelezo ya awali waliyosomewa washtakiwa kwa mujibu wa sheria na hawakupata haki ya kuwakilishwa hivyo kufanya mwenendo mzima kuwa kinyume na sheria.

Warufani hao wanaomba Mahakama Kuu iamuru hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi ya warufani ifutwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles