Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
KAMATI ya Maafa inatarajia kuikabidhi Serikali taarifa ya maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera Septemba 10, mwaka jana ili kuanza ukararabati wa miundombinu iliyoharibiwa wakati wa tukio hilo.
Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu 17 na zaidi ya 200 wakijeruhiwa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema kuwa tayari wameandaa utaratibu wa kuikagua taarifa hiyo ili kumalizia kazi ya kukarabati maeneo yaliyoharibiwa.
Alisema kazi waliyopewa kama wizara ni kuhakikisha fedha zilizopatikana zinatumika kurekebisha miundombinu ya Serikali ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama vile shule, hospitali na miundombinu ya barabara.
Alipoulizwa kuhusu utaratibu utakaotumika kwa wale watakaokuwa tayari kutoa michango yao kwa waathirika, Waziri Mhagama alisema kazi waliyopewa ni kutumia fedha zilizopo kwa miundombinu ya Serikali.