Na Ashura Kazinja – Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, amepiga marufuku uchimbaji wa mchanga, kilimo, ufyatuaji wa matofali na shughuli nyingine zote za kibinadamu zinazofanyika kandokando ya mito na vyanzo vingine vya maji.
Shughuli hizo ni pamoja na ufyatuaji matofali, kilimo cha mbogamboga pamoja na mahindi.
Akizindua mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa usimamizi wa Mazingira Kanda ya Mashariki yaliyoandaliwa na Baraza la Mazingira (NEMC), Kebwe alisema amechukua hatua hiyo ili kunusuru hali ya mazingira mkoani hapa.
Alisema kilimo endelevu na cha uhifadhi ndicho kilimo kinachoshauriwa kwa Mkoa wa Morogoro katika maeneo yote ambayo yanalimwa na yanafaa kwa kilimo.
“Wananchi waheshimu kulima umbali wa mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kupanda miti inayosaidia kuhifadhi mazingira ambayo imethibitishwa kuwa haina athari kwa vyanzo hivyo vya maji.
“Ufyatuaji wa matofali pamoja na kilimo aidha cha mbogamboga au cha mazao makubwa kama mahindi, vitunguu, mchicha, kandokando ya mito, vitu hivi tumevipiga marufuku ili kulinda mazingira pamoja na kilimo,” alisema Kebwe.
Kwa upande wake Mratibu wa Mazingira Kanda ya Mashariki, Jafari Chungege, alielezea changamoto za mazingira zinazowakabili kuwa ni uchimbaji wa madini katika vyanzo vya maji, mmong’onyoko wa kingo za bahari, uvamizi wa vyanzo vya maji na utupaji taka ovyo ambazo zimekuwa zikiharibu mazingira kwa wingi.
Naye Ofisa Mazingira Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Glory Kombe, alisema mifuko ya plastiki ni hatari zaidi kwani huingiliana na mfumo wa udongo ambapo husababisha kutokuotesha zao la aina yoyote, huku moshi wa mifuko hiyo ikiwa ni sumu inayosababisha kansa.