23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RC APIGA MARUFUKU UFYATUAJI  MATOFALI KANDO YA MITO

Na Ashura Kazinja –  Morogoro


MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, amepiga marufuku  uchimbaji wa  mchanga, kilimo, ufyatuaji wa matofali na shughuli nyingine zote za  kibinadamu zinazofanyika kandokando ya mito  na vyanzo vingine vya maji.

Shughuli hizo ni pamoja na ufyatuaji matofali, kilimo cha mbogamboga pamoja na mahindi.

Akizindua  mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa usimamizi wa Mazingira Kanda ya Mashariki yaliyoandaliwa na Baraza la Mazingira (NEMC), Kebwe alisema amechukua hatua hiyo ili kunusuru hali ya mazingira mkoani hapa.

Alisema kilimo endelevu na cha uhifadhi ndicho kilimo kinachoshauriwa kwa Mkoa wa Morogoro katika maeneo yote ambayo yanalimwa na yanafaa kwa kilimo.

“Wananchi waheshimu kulima umbali wa mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kupanda miti inayosaidia kuhifadhi mazingira ambayo imethibitishwa kuwa haina athari kwa vyanzo hivyo vya maji.

 “Ufyatuaji wa matofali pamoja na kilimo aidha cha mbogamboga au cha mazao makubwa kama mahindi, vitunguu, mchicha, kandokando ya mito, vitu hivi tumevipiga marufuku ili kulinda mazingira pamoja na kilimo,” alisema Kebwe.

Kwa upande wake Mratibu wa Mazingira Kanda ya Mashariki, Jafari Chungege, alielezea changamoto za mazingira zinazowakabili kuwa ni uchimbaji wa madini katika vyanzo vya maji, mmong’onyoko wa kingo za bahari, uvamizi wa vyanzo vya maji na utupaji taka ovyo ambazo zimekuwa  zikiharibu mazingira kwa wingi.

Naye Ofisa Mazingira Mkuu wa Baraza la Hifadhi na  Usimamizi wa Mazingira, Glory Kombe, alisema mifuko ya plastiki  ni hatari zaidi kwani huingiliana na mfumo wa udongo ambapo husababisha kutokuotesha zao la aina yoyote, huku moshi wa mifuko hiyo ikiwa ni sumu inayosababisha kansa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles