26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

WAATHIRIKA DAWA ZA KULEVYA KUJENGEWA VITUO ZAIDI

Na AMINA OMARI- TANGA


SERIKALI ipo katika mkakati wa kuweka vituo maalumu vya kutoa tiba ya bure ya dawa ya methadone kwa waathirika wa dawa za kulevya katika mikoa mitano nchini.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Mohamed Bakari, wakati wa uzinduzi wa jengo la kitengo cha afya ya akili kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Mkoa wa Tanga.

Alisema hatua hiyo ni jitihada za Serikali  katika kuhakikisha wanaunganisha nguvu kwenye mapambano ya matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwapa tiba ya uhakika waathirika wa dawa hizo nchini.

Aliitaja mikoa itakayonufaika na huduma hiyo kuwa ni Tanga, Arusha, Mbeya, Dodoma na Kilimanjaro.

“Tunajua kuna jitihada zinazochukuliwa na sekta binafsi ikiwamo uwepo wa sober house, lakini sisi kama Serikali tumeamua kuweka vituo katika

hospitali za rufaa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa pamoja na huduma za afya,” alisema Dk. Bakari.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini ambao ndio wafadhili wa jengo hilo, Ane Maria Kaarstad, alisema Serikali ya nchi hiyo imefurahishwa na juhudi za udhibiti wa dawa za kulevya zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.

Alisema kutokana na gharama kubwa ya tiba ya afya ya akili, waliamua kufadhili ujenzi wa jengo  hilo na kutoa vifaa tiba ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati.

“Kumhudumia mgonjwa wa afya ya akili kunahitaji uwazi na uhuru, hivyo jengo hili litasaidia kutoa huduma kwa haraka zaidi,” alisema balozi huyo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alisema mwaka jana kulikuwa na wagonjwa wa afya ya akili 7,435 waliopatiwa huduma katika vituo mbalimbali mkoani hapa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles