24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS UHURU KENYATTA, VIONGOZI WENZAKO WAMEKUSIKIA?

Na Leah Mwainyekule      |           


Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya; Salaam!

Sikuwahi kufikiri kama ingekuja kutokea siku kama ya leo, ya mimi kuamua kukuandikia waraka huu nikiwa na imani kwamba kuna uwezekano mkubwa wa waraka wangu huu kusomwa na wewe na hata na viongozi wenzako. Nikisema viongozi wenzako, namaanisha wale marais wenzako wa nchi za Afrika waliokula viapo kama wewe, wenye wafuasi kama wewe na wenye wapinzani wakubwa kama wewe.

Mheshimiwa Rais, kutokana na ujirani wa nchi zetu, nadhani si ajabu kwa mimi kupenda kufuatilia masuala ya nchi unayoiongoza, kama ambavyo hupenda kufuatilia masuala ya ndani ya nchi nyingine yoyote iliyotuzunguka.

Hata hivyo, dunia kwa sasa ni eneo huru lenye kuwezesha watu kutoka hata nchi za mbali kufuatilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kutoa maoni yao, hata kama ukweli ni kwamba hawayajui yale wanayoyazungumza. Nina imani sitaonekana kuwa mtu wa kutoyajua ninayoyazungumza, maana nimejaribu kukufuatilia kwa miezi kadhaa sasa.

Mheshimiwa Rais, mahakama nchini Kenya ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka jana, niliduwaa.   Niliduwaa kwakuwa sikutaraji kwamba kitu kama hicho kingeweza kutokea katika ukanda wetu huu; lakini ilitokea. Ilipotokea, ulionekana kutopendezwa kabisa na uamuzi ule na ulizungumza maneno makali dhidi ya wale majaji waliopitisha hukumu ile.

Hayakuwa maneno mazuri. Yalikuwa maneno ya kuonesha kama vile unajiona utashinda tu tena uchaguzi wa marudio na ukishinda, ‘utashughulika’ na wale waliosababisha kuwapo kwa uchaguzi wa marudio, kwa maana ya majaji walioipitisha hukumu ile ya kihistoria. Ni kweli, hazikuwa kauli nzuri.

Wakati wengine tukiendelea kufuatilia uchaguzi wa marudio, hapa katikati kulikuwa na majibizano ya hapa na pale kati yako wewe na wapinzani wako wa kisiasa. Taifa la Kenya liligawanyika – kama inavyotarajiwa kuwa katika uchaguzi wowote ule – lakini bahati mbaya, Taifa la Kenya liligawanyika si kwa sababu ya siasa tu, bali kwa sababu pia ya makabila. Ilikuwa kama vile wafuasi wako wote walitarajiwa kuwa wale wa kabila lako tu. Sisi wengine tuliokuwa tukitazama kwa mbali tulikuwa tunajiuliza endapo chaguzi zenu ni za kuchagua machifu wa makabila yenu, au Rais wa nchi.

Mheshimiwa Rais, nilifuatilia kwa karibu sana matukio yaliyokuwa yakitokea kuelekea ‘kuapishwa’ kwa mpinzani wako mkuu, Raila Odinga, kuwa “Rais wa wananchi wa Kenya.” Si mimi tu, bali nadhani wengi wetu tulikuwa tukitarajia siku hiyo Kenya ingebadilika na kupewa jina jingine. Tulitarajia – pengine hata Raila mwenyewe ndivyo alivyowaza – kwamba siku hiyo huyo bwana atakamatwa, atapigwa, ataswekwa ndani na kufunguliwa kesi ya uhaini.

Tulitarajia kwamba hayo yatatokea na yakitokea, dunia nzima itakuwa ikiangalia na kuripoti hatua kwa hatua kwa jicho lao wenyewe na “Jumuia ya Kimataifa” kuishutumu Kenya kwa “kunyanyasa wapinzani na kuminya demokrasia na uhuru wa kujieleza.” Lakini matarajio yetu yalitumbukia nyongo baada ya kuona hali ilikuwa shwari na polisi walikuwa wakifanya kazi yao hasa ya kulinda usalama wa raia na mali zake, badala ya kumzonga zonga. Siku ile, nilianza kukutazama kwa jicho la tofauti.

Nilikutazama kwa jicho la tofauti kwa sababu ulitukomesha kwelikweli. Jicho langu likakuheshimu ghafla na kuanza kuyasahau yale mengine ya nyuma uliyokuwa ukiyafanya, kama vile kuwatukana wapinzani na kuwasakama majaji. Jicho hili la heshima likajiuliza: wa wapi viongozi wengine wa Afrika wa kuiga mfano huu na kuona kwamba si kila kitu kinajibiwa kwa marungu na mabomu ya kutolea machozi? Wakati mwingine kunyamaza na kuacha mpinzani wako ajiapishe kinyume cha Katiba ya nchi, kunakufanya wewe uliyekaa kimya uonekane una busara zaidi.

Mheshimiwa Rais, kilichonifanya niandike hasa waraka huu leo, ni ile hotuba yako uliyoitoa katika Bunge la Kenya. Kusema kweli kabisa sikuisikiliza, lakini niliwasikia watu wakiizungumzia na vyombo vya habari vilivyoripoti. Niliamua kutafuta taarifa yenye hotuba hiyo na kuisoma. Nilipokuwa naisoma, nilikuwa kama nakuona unavyozungumza na kutikisa kichwa, huku sura yako ikionesha kumaanisha kwako yale uliyoyasema. Hotuba ile Mheshimiwa, nayo ilinishangaza.

Ndiyo, ilinishangaza kwa sababu kuu moja: uliomba msamaha!!! Ni wapi ulishawahi kuona kiongozi – mkuu wa nchi – akasimama mbele ya wawakilishi wa wananchi na kuomba radhi kwa yale ambayo ama aliyafanya au aliyasema? Uliona wapi? Binafsi nimewahi kuona, lakini si katika maisha halisia. Actually nilikuwa naangalia tamthiliya moja iitwayo Designated Survivor ambayo ina mhusika aliye Rais wa Marekani, ambaye aliomba radhi kwa Taifa lake kutokana na matamshi binafsi aliyoyatamka. Yalikuwa maigizo.

Lakini wewe Mheshimiwa Rais, hukuwa unaigiza. Uliomba radhi kwa kuwaumiza wananchi wako, uliomba radhi kwa kuathiri Umoja wa Kenya. Uliomba usamehewe na uliomba waungane nawe kuyatibu majeraha hayo. Ulisema kwamba Wakenya mnatakiwa kubadilika ili watoto wenu wakue ndani ya Kenya iliyo tofauti kabisa. Kwamba mnatakiwa kuonesha mifano halisi kwamba ninyi ni raia halisi wa Kenya na kwamba mnatakiwa kuyafanya hayo kwa ajili ya nchi yenu na si kwa ajili yenu wenyewe.

Mheshimiwa Rais, sisi wananchi wa Bara la Afrika kwa kweli hatujazoea kuona mkuu wa nchi akisimama na kuzungumza namna hiyo. Sisi Waafrika tumeshazoea kuona watu wakikaripiwa na kuonywa kwamba Serikali si ya mchezo mchezo.

Mheshimiwa Rais, kwenye hotuba yako umesema kwamba endapo hamtafanya kazi pamoja kuijenga Kenya yenye umoja na amani, mnaweza kujikuta mnaiangamiza nchi na hiyo dhambi itawatafuna.

Umetamka pia kwenye hotuba yako kwamba mwaka uliopita umewafundisha kwamba endapo hamtaweka ukomo kwenye ushindani wa kisiasa unaobana wengine, basi Kenya ndiyo itakayofika ukomo. Kwamba wakati wa kampeni mligeuza siasa kuwa mapambano ya maadui walioshindikana, badala ya mijadala ya afya kati ya waliokuwa wakipingana….mbona wenzako Afrika ndicho tulichokizoea Mheshimiwa? Wakati wa kampeni ndio wakati ambao watu hujifunza matusi mapya. Wakati wa kampeni watu hubadilika na kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya wapinzani wao, bila hata kujali kwamba huyo anayemnenea mabaya ana umri wa kuweza kuwa mzazi wake!

Umezungumza, Mheshimiwa, kwamba mnatakiwa kuomba radhi kutokana na matamshi yenu, hasira zenu, na chuki zenu ambazo Wakenya waliwasikia mkitamka. Kwamba kila kiongozi wa nchi hiyo anatakiwa kuwakumbusha wana wenu kwamba mnao uwezo wa kuwa na Kenya inayozungumza kwa utaratibu, inayokosoa kwa utaratibu na inayoheshimu ushindani kwa njia ya kistaarabu… Mheshimiwa, hakuna kutukanana? Hakuna kusimangana? Hakuna kutishana? Hakuna kupotezana? Wenzio Waafrika mbona tulishayazoea hayo? Mabadiliko yatawezekana kweli.

Mheshimiwa Rais, hayo ndio maisha ya Waafrika wengi, na yameshazoeleka. Ulivyoamua kusimama mbele ya kadamnasi na kuomba radhi, sisi tunashangaa. Viongozi wenzako wa Afrika wanayajua uliyoyasema? Wamekusikiliza? Wamejaribu hata kufuatilia taarifa za hotuba yako? Najaribu kuwaza ni kitu gani wanachokiwaza wao kama kweli wamekusikia. Wamekuonaje? Shujaa ama msaliti? Wamekusikiliza kweli?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles