28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

KOCHA YANGA ABWAGA MANYANGA LIGI KUU


MOHAMED KASARA-DAR ES SALAAM     |

KOCHA mpya wa timu ya Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera, amesema kikosi chake hakina nafasi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, badala yake kitajikita kufanya vizuri katika michezo ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha huyo anaamini Yanga haina ubavu wa kufukuzana na vinara, Simba ambao imewazidi kwa pointi 17 katika mbio hizo, hivyo ameushauri uongozi wa klabu hiyo kukitumia kikosi B katika michezo miwili ya Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar.

Yanga ipo nafasi ya tatu, baada ya kucheza michezo 24, ikishinda michezo 13, sare tisa, ikipoteza michezo miwili, na kujikusanyia pointi 48, ikiruhusu kufungwa mabao 14 na kufunga mabao 40, wakati Simba, ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa, inaongoza msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza michezo 27 na kujikusanyia pointi 65.

Simba inahitaji pointi mbili ili iweze kutangazwa mabingwa wa soka msimu wa 2017/18 na imebakisha michezo mitatu dhidi ya Singida United, utakaopigwa Jumapili Uwanja wa Namfua, Kagera Sugar na kumaliza dhidi ya Majimaji katika Uwanja wa Majimaji, Songea.

Zahera ametoa ombi hilo wakati timu hiyo ikianza vibaya katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuchapwa mabao 4-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Yanga, ambayo iliwasili jana mchana kutoka Algeria, kesho inatarajia kushuka dimbani kuumana na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Timu hiyo pia itakuwa na kibarua kingine cha kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, kabla ya kucheza mchezo wa pili wa makundi dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Mei 16, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua nchini jana, Zahera aliwashauri viongozi wa Yanga kuacha kukimbizana na Simba kwenye ligi, badala yake waweke mkazo zaidi kwenye michezo ijayo ya Kombe la Shirikisho.

“Hatuna nafasi kwenye ligi, hivyo tunatakiwa kuweka nguvu zote kwenye michezo ya Kombe la Shirikisho, nimewaomba viongozi wapeleke kikosi B katika michezo yetu ya ligi ili nibaki na kikosi cha kwanza nikiandae kwaajili ya mchezo dhidi ya Rayon.

“Tunatakiwa kujiandaa vema ili tusipoteze mchezo huo, ukiangalia ratiba ya ligi imekaa vibaya kwetu, tumefika leo (jana), kesho (leo), tunatakiwa kwenda Mbeya, baadaye tuna mchezo Morogoro kabla ya kuivaa Rayon, ndiyo maana nimewaomba wakubwa tuwaze zaidi Kombe la Shirikisho.”

Akizungumzia kipigo cha Algeria, Zahera alisema kikosi chake kilipoteza mchezo huo kutokana na kukosa wachezaji wazoefu.

“Tulikosa wachezaji wenye uzoefu katika kikosi changu, hivyo uwanjani tulikuwa na watoto watano, wenzetu walitumia mwanya huo kutuadhibu.

“Kwenye mpira uzoefu ni jambo la msingi, vijana walijitahidi kucheza kwenye majukumu waliyopewa, lakini walikosa umakini,” alisema Zahera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles