22.2 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia kuongoza mkutano Baraza la Amani na Usalama Afrika

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Tanzania imetajwa kuwa kitovu cha harakati za ukombozi barani Afrika katika masula ya amani, ulinzi na usalama.

Pia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika litakalofanyika Mei 25, 2024 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akizungumza na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 22,2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema mkutano huo utakaofanyika Mei, 24-25 kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere.

“Kwa miaka mingi tangu tumepata uhuru imekuwa ndio kitovu cha harakati za ukombozi barani Afrika, wapigania uhuru wa nchi nyingi za Afrika wakati wanatafuta uhuru na ukombozi wa nchi zao waliitumia Tanzania kama sehemu ya kujipanga.

“ Nchi yetu ilitoa sapoti kubwa katika harakati hizo, Tanzania inaheshimika sana duniani na barani Afrika kwa mchango wake mkubwa wa ukombozi Barani Afrika,” amesema.

Amesema kuna vyama vya ukombozi hasa Kusini mwa Afrika ambavyo vilianzishwa Dar es Salaam matokeo yake baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika wamekuwa wakizungumza Kiswahili kwa sababu wameishi kwa miaka mingi.

Amesema baada ya ukombozi kupatikana kazi ya Tanzania iligeuka katika kulinda uhuru, amani, ulinzi na usalama wa bara la Afrika kwa sababu hakuna faida ya kuwa nchi huru bila kuwa na usalama.

Makamba amesema dhima ya Tanzania ikabadilika na ikawa mstari wa mbele katika harakati za kulinda usalama wa bara la Afrika.

“Ukiangalia nchi za Afrika zinazoongoza katika kusaidia jitihada za kupatikana amani barani Afrika hasa ukanda huu ni Tanzania na mazungumzo mengi ya kutafuta amani, ya kusuluhisha yamefanyika hapa, viongozi wetu wote kuanzia Julius Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Magufuli na Rais Samia wameshiriki kama wasuluhishi wa migogoro ya nchi mbalimbali Afrika.

“Kama Tanzania, jukumu hili ni heshima na ni wajibu, ndio moja ya chanzo cha sifa yetu kama nchi kuwa hatuko nyuma katika harakati za kutafuta amani na usalama barani Afrika kama ambayo hatukuwa nyuma wakati wa kutatuta uhuru na ukombozi wa bara la Afrika,”ameeleza.

Amesema shughuli itakayofanyika Mei 25, mwaka huu ni mahala pake kwa sababu Tanzania ni kiongozi wa harakati wa kuleta amani na usalama barani Afrika.

Akizungumzia kuhusu Baraza hilo Makanba amesema Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Afrika tangu kuanzishwa kwake.

Ameongeza kuwa kulifanyika mabadiliko ya umoja huo na kuundwa chombo kikuu cha kusimamia amani na usalama Barani Afrika linalojulikana kama Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.

“ Baada ya kundwa kile chombo muundo wake ni kuwa na wajumbe 15 ambao wanateuliwa kwa mzunguko kila baada ya muda, nchi hizo kwa wakati wote zinakuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya kukabiliana na migogoro isitokee Afrika.

“Kuzuia ,kusuluhisha migogoro hiyo inapojitokeza na ndio chombo cha Umoja wa Afrika ambacho kila mwezi huwa na Mwenyekiti wa baraza hilo na Mei, mwaka huu, Mwenyekiti atakuwa Tanzania chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Amesema Mei, mwaka huu una historia mahususi kwa sababu chombo hicho kilianzishwa na kukaa kwa mara ya kwanza Mei 25, mwaka 2004 sasa ikifika Mei 25, mwaka huu kitakuwa kimetimiza miaka 20 tangu Baraza hilo lianzishwe.

“Viongozi wa kamisheni ya Afrika na viongozi wakuu waliamua kutokana na umuhimu wa Umoja wa Afrika, kutokana na dhima muhimu ya kulinda na kuleta amani barani Afrika na kutokana na umuhimu wa chombo hiki na kazi kubwa iliyofanya kwa miaka 20 iliyopita, umuhimu wa kuwa na chombo imara basi tuadhimishe miaka 20 ya kunzishwa kwa baraza hilo Tanzania wakati uenyekiti ukiwa Tanzania,”amefafanua.

Amesema uenyekiti ukiwa Tanzania maana yake kuanzia katika ngazi ya mabalozi kazi yake ni kufuatilia masuala ya amani katika Bara la Afrika.

“Ni jambo la heshima kubwa kwa sababu Tanzania sasa ni mjumbe wa baraza hili kwa sababu ilichaguliwa Machi, mwaka 2022 na ilichaguliwa kwa mara ya pili Machi, mwaka huu, sisi ni wajumbe mpaka mwaka 2026,” amesema Makamba.

Amesema Rais Dk. Samia aliridhia kufanya sherehe kubwa ya miaka 20 ya baraza hilo kwa kuwaalika viongozi kadhaa wakiwemo marais wastaafu na kamisheni.

Makamba amesema katika kusherehekea miaka hiyo walikuwa na dhima tofauti ikiwa masuala ya usuluhishi, misaada na mahitaji ya kibinadamu, nafasi ya wanawake na vijana katika ulinzi na usalama na kusaidia misheni za amani.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo miaka 20 ya Baraza la Amani la Usalama Barani Afrika ni “chombo cha maamuzi, miogo miwili ya Afrika ya amani na usalama tunayoitaka’ na jambo hilo linafanyika pamoja na Kamisheni ya Umoja wa Afrika”.

Baadhi ya wanaotarajia kushiriki ni Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, viongozi wastaafu Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Burundi, Joachim Chisano(Msumbiji) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Vilevile katika baraza hilo kutakuwa na muhadhara, mazungumzo , majadiliano na jopo ya kujadili kuhusu hali ya ulinzi na usalama barani Afrika kwa miaka 20 iliyopita na muelekeo kwa miaka 20 ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles