31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia awapa viwanja Twiga Stars

Na WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital

RAIS  Samia Suluhu Hassan,  amewakabidhi wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars, hati za viwanja baada ya kufurahishwa  kitendo cha kutwaa ubingwa wa michuano ya COSAFA.

Rais Samia ametoa hati hizo leo Oktoba 27,2021 wakati wa hafla ya kuwapongeza na chakula cha mchana iliyofanyika  Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi hati ya kiwanja mchezaji wa Twiga Stars, Fatuma Issa leo Ikulu, Dar es Salaam

Akizungumza katika halfa hiyo, Rais Samia amesema amefanya hivyo kwa kutambua mchango wa Twiga Stars katika michezo na kulitangaza vizuri Taifa.

“Nilikuwa nawafuatilia katika mashindano ya COSAFA, nimefurahishwa na kiwango mlichokionesha hadi kutwaa kombe hili ambalo leo mmekuja kulikabidhisha.

Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea Kombe la Ubingwa wa Cosafa kutoka kwa nahodha wa timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars Amina Ali Bilali leo Oktoba 27, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam

“Nilijiambia kuna haja ya kukaa pamoja kupata chakula cha mchana na kuambizana. Niseme kwamba watoto wangu wa Twiga Stars imenifanya mama yenu nitembee kifua mbele,” ameeleza Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza na baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars mara baada ya kupokea Kombe la Ubingwa wa Cosafa kutoka kwa wachezajia wa timu ya hiyo leo Oktoba 27, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema  timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri na kuleta makombe lakini haitangazwi kama ilivyo ya wanaume, hivyo ameamua kulipiza.

“Huko nyuma nilikuwa nalia nasema kuna timu hapa ilicheza Taifa Stars wakaifunga timu  gani na kuingia sijui  nusu fainali kina Hassani, Wakurugenzi na kina Karia wakasimama wachezaji wakabandikwa viwanja wote vya kujenga nyumba zao.

“Lakini wale ambao walikuwa wameleta  makombe ndani,kombe kabisa hili hapa, sio nusu fainali hapana, sasa leo  ‘narevange’. Kuna vijisenti vya mafuta vitapitapita  kwa wachezaji pamoja na makocha wao.

“Nawapatia watoto wangu viwanja vya kujenga nyumba zao, bahati mbaya au nzuri, viwanja vyote vitakuwa kule mama yenu ninapokaa, najua baadhi yenu itakuwa shida kujenga Dodoma lakini leo pokeeni viwanja nitajua nini cha kufanya.

Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars mara baada ya kupokea Kombe la Ubingwa wa Cosafa kutoka kwa wachezajia wa timu ya hiyo leo

“Nawapa viwanja kwa sababu, nilisema siku ile maneno yangu yakageuzwa juu chini, nilisema vijana hawa wana maisha baada ya wao kuacha kucheza, watafika mahali watachoka, muda mwingi wameutumia katika kucheza, lazima tuwajengee ‘future’ yao.

Aidha amewataka wachezaji hao kuzingatia nidhamu katika kazi yao  kwani ndiyo msingi mkubwa wakufanya vizuri.

Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza na viongozi na wachezaji wa timu ya Taifa ya  Wanawake Twiga Stars mara baada ya kupokea Kombe la Ubingwa wa Cosafa kwa timu  hiyo leo Oktoba 27, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Pia amewataka mawakala wa soka kuwatangaza wachezaji hao ili waweze kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi na  kupata mchanganyiko wa uzoefu katika kikosi hicho.

Tofauti na Twiga Stars, Rais Samia amewapongeza watanashati na warembo ambao ni watu wenye uziwi, pamoja na timu za kriketi na karate kutokana na kufanya vizuri katika mashindano yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles