Na WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
RAIS Samia Suluhu Hassan, amewakabidhi wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars, hati za viwanja baada ya kufurahishwa kitendo cha kutwaa ubingwa wa michuano ya COSAFA.
Rais Samia ametoa hati hizo leo Oktoba 27,2021 wakati wa hafla ya kuwapongeza na chakula cha mchana iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika halfa hiyo, Rais Samia amesema amefanya hivyo kwa kutambua mchango wa Twiga Stars katika michezo na kulitangaza vizuri Taifa.
“Nilikuwa nawafuatilia katika mashindano ya COSAFA, nimefurahishwa na kiwango mlichokionesha hadi kutwaa kombe hili ambalo leo mmekuja kulikabidhisha.
“Nilijiambia kuna haja ya kukaa pamoja kupata chakula cha mchana na kuambizana. Niseme kwamba watoto wangu wa Twiga Stars imenifanya mama yenu nitembee kifua mbele,” ameeleza Rais Samia.
Amesema timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri na kuleta makombe lakini haitangazwi kama ilivyo ya wanaume, hivyo ameamua kulipiza.
“Huko nyuma nilikuwa nalia nasema kuna timu hapa ilicheza Taifa Stars wakaifunga timu gani na kuingia sijui nusu fainali kina Hassani, Wakurugenzi na kina Karia wakasimama wachezaji wakabandikwa viwanja wote vya kujenga nyumba zao.
“Lakini wale ambao walikuwa wameleta makombe ndani,kombe kabisa hili hapa, sio nusu fainali hapana, sasa leo ‘narevange’. Kuna vijisenti vya mafuta vitapitapita kwa wachezaji pamoja na makocha wao.
“Nawapatia watoto wangu viwanja vya kujenga nyumba zao, bahati mbaya au nzuri, viwanja vyote vitakuwa kule mama yenu ninapokaa, najua baadhi yenu itakuwa shida kujenga Dodoma lakini leo pokeeni viwanja nitajua nini cha kufanya.
“Nawapa viwanja kwa sababu, nilisema siku ile maneno yangu yakageuzwa juu chini, nilisema vijana hawa wana maisha baada ya wao kuacha kucheza, watafika mahali watachoka, muda mwingi wameutumia katika kucheza, lazima tuwajengee ‘future’ yao.
Aidha amewataka wachezaji hao kuzingatia nidhamu katika kazi yao kwani ndiyo msingi mkubwa wakufanya vizuri.
Pia amewataka mawakala wa soka kuwatangaza wachezaji hao ili waweze kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi na kupata mchanganyiko wa uzoefu katika kikosi hicho.
Tofauti na Twiga Stars, Rais Samia amewapongeza watanashati na warembo ambao ni watu wenye uziwi, pamoja na timu za kriketi na karate kutokana na kufanya vizuri katika mashindano yao.