27.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS ATOA NENO ZITO KWA MAHASIMU WA JK

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


 

dr-john-pombe-magufuliRAIS Dk. John Magufuli, ametaka Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aachwe apumzike.

Dk. Magufuli pia ameshangaa kuhusishwa na kuzuiwa bandarini mizigo ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Salma Kikwete.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema Rais amesikitishwa na kile kilichodaiwa kuwa ni uzushi unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais Kikwete na familia yake kwa kuandika kuwa anahusika kuzuia mizigo ya WAMA bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.

“Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete, tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na mwacheni Rais Kikwete apumzike.

“Rais Kikwete amefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika, narudia mwacheni apumzike, Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa kwa makusudi ili kuwachafua viongozi wastaafu,” alionya Rais Magufuli.

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari (si MTANZANIA),  na mitandao ya kijamii ilichapisha taarifa zinazomhusisha Mwenyekitiwa WAMA Salma Kikwete kwamba ameshindwa kulipia kodi ya mizigo mikubwa iliyoiingiza nchini na hivyo kuwa hatarini kupigwa mnada.

Taarifa hiyo ya Ikulu, ilisistizwa kwamba si kweli mizigo hiyo ilizuiliwa na Rais Dk. Magufuli na wala Rais hajawahi kutoa agizo lolote kuhusu mizigo hiyo kuzuiwa.

“Tunapenda kuutarifu umma kuwa taarifa hizo si za kweli na ni uzushi, kwani Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Taarifa za kuzuiwa mizigo ya WAMA bandarini ilizua mijadala katika mitandao mbalimbali ya kijamii hasa baada ya kunukuliwa kwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Huduma za Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, ambaye alithibitisha ukweli wa taarifa hizo.

Kayombo alinukuliwa na chombo hicho cha habari akisema kwamba ni kweli kuna mali za WAMA ambazo zinaweza kupigwa mnada endapo hazitalipwa kufikia tarehe ya mnada.

Hata hivyo WAMA ilikanusha kuwapo kwa mali zake zilizozuiliwa bandarini na kusema kuwa mizigo hiyo ilishakombolewa muda mrefu.

Siku chache baada ya taarifa hizo kuripotiwa gazeti jingine la kila siku liliripoti kuwa Mama Salma amekomboa mizigo yake baada ya kulipia kodi.

Inaelezwa kuwa kipindi cha nyuma Taasisi ya WAMA ilikuwa inapata msamaha wa kodi wa mizigo ambayo ilikuwa inaingiza nchini kusaidia wanafunzi yatima wanaosomesha na taasisi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea Rais Dk. Magufuli mara kadhaa amekuwa akitoa kauli ya kuwahakikishia viongozi wasataafu kuwa atawalinda wakati yeye akiwa madarakani.

Moja ya kauli hizo ni ile aliyoitoa Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 23, mwaka huu wakati akikabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo alisema Serikali itawalinda wastaafu nchini wakiongozwa na viongozi wakuu wa umma ili wawe na heshima yao ndani ya jamii.

“Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wewe pumzika kwa raha zako, upo salama watachonga wee lakini mimi kama Rais wa awamu ya tano nipo tayari kuwalinda watumishi wote wastaafu kwa kuthamini mchango wao ndani ya Taifa hili,” alisema Rais Dk Magufuli.

Kauli hiyo amekuwa akiirudia kila wakati hasa pale anapokuwa ameandamana na viongozi wastaafu hasa marais waliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles