26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

WASEMA UKWELI WANAPOTEA, ARDHI INAPANDA THAMANI

Fidel Castro
Fidel Castro

Na FRANK BANKA,

DUNIA imeshuhudia zizimo. Tanzia imewatikisa vilivyo, kuanzia Cuba hadi Afrika. Kila kona amezungumzwa, iwe kwa mazuri ama mabaya. Lakini ukweli utabaki kuwa kuaga dunia kwa Fidel Castro kumedhihirisha kuwa wasema ukweli wanazidi kupotea na ardhi nayo inapanda thamani.

Fidel Castro Ruz amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 na kumwachia madaraka mdogo wake, Raul Castro Ruz, ambaye anatarajiwa kustaafu ifikapo mwaka 2018.

Katika tafakuri yangu juu ya kifo cha Castro, nimelazimika kuamini kuwa watu wanaotunza misingi, wasemaji ukweli wanazidi kupotea ulimwenguni. Wanazidi kutuacha solemba na kujikuta hatuna mahali pengine pa kuwasikiliza. Mbaya zaidi, kila wanavyotuacha na ardhi nayo inapanda thamani.

Umeondoka Fidel Castro, mabepari tu ndio wanaweza kukwita majina yote wanayoyajua. Tena majina ambayo wanaamini kuwa mabaya mno. Ukweli siku zote ni mchungu, hasa kwa mtu ambaye kaamini uongo ndio ukweli katika maisha yake hapa ulimwenguni.

Aghalabu tumekwenda darasani tukafundishwa binadamu ni wakatili, lakini huwa tunasahau kila roho yoyote mbaya ambayo unaweza kuinyoshea kidole kwa binadamu mwenzako au kuisema kwa namna yoyote inahitaji wakati na mazingira roho ya aina hiyo hiyo kuonekana kwako.

Wakati wa uhaia wake, Fidel Castro alipata kutamka maneno mazito kidogo. Castro alisema kuwa kila binadamu ana aina zote za roho, yaani anaweza kuvaa uasi au utu, ni suala la muda tu. Hakufafanua vizuri, lakini alilenga mustakabali wa mataifa na jamii zake kote duniani.

Si hilo peke yake, kuna mengine ambayo yalitamkwa yenye kutafakarisha. Miongoni mwa mwambo hayo ni pamoja na kukumbuka namna Fidel Castro alivyoeleza hilo neno ambalo kwangu lilifunga mwaka.

Baada ya Castro klufariki dunia nimejikuta nikikumbuka matamshi yake na misimamo yake pia. Miongoni mwake ni maneno ambayo yataishi muda mrefu kwangu, ila ule muda ukifika watu wakijua kutunza misingi na kusema ukweli wazi wazi, hasa kwa mambo yanayohusu utaifa na uzalendo, ndio wakati tutagundua kuwa haupo tena nasi kama ambavyo leo sisi Watanzania tunavyomkumbuka Mwalimu Julius Nyerere.

Castro alipata kusema, “Wanajadiliana juu ya anguko la ujamaa, lakini yako wapi mafanikio ya ubepari katika bara la Afrika, Asia na Amerika ya Kusini?” Kauli hii ilikuwa sehemu ya mapambano yake dhidi ya mfumo wa kibepari ambao ulikuwa umeshika kasi duniani. Katika dunia hii ya kibepari tuna wanaume wachache sana wanaoweza kusema ukweli kama alivyokuwa Fidel Castro.

Dunia ya kibepari kwa muda sasa inazalisha viongozi vibaraka. Ubepari unazalisha vijana wenye kuogopa watu wakatili, huku wakiwa hawajui aina ya ukatili wanaouzungumzia, hasa baada ya vyombo vya habari kueleza aina ya ukatili kadiri ya wanavyosema wale wanaomchukia mtu anayepewa majina ya kikatili.

Kuua sio lazima utumie silaha, ila wengi tumeshatumia sana mdomo kumaliza uhai wa wengine. Kuua, au kama bado basi kuna siku midomo yetu itanena uasi wa aina ya kumzungumzia mtu vibaya au kumtakia mtu mauti, bado nitaamini kuwa alichokisema Fidel Castro kuwa ubepari kama mfumo wa maisha umefanikiwa magharibi na Marekani pekee, lakini hakuna ufanisi wowote katika maeneo ya Afrika wala Latini Amerika.

Castro uliipenda Cuba. Na kifo chako ni kweli watu muhimu wenye kupenda watu wao wanatoweka na ukweli kifo chako kimezidi kuipandisha thamani ardhi iliyo kwenye uso wa dunia hii. Ulikuwa unatoka mbali kuja kuziona tawala za Afrika. Uliwapenda watunza misingi wenzako Nelson Mandela, Julius Nyerere, Muamar Gaddafi, Malcolm X na wengine wengi ambao leo umekwenda kuungana nao huko ardhini.

Najua wale wahafidhina watasema ubaya wako na najua vibaraka watakusema kuwa ulikuwa mbaya na usiyejali usawa, ila thamani ya kifo chako ardhi ndio inatambua. Heshima kwako shujaa wangu Fidel Castro, Komredi, mjamaa mwenzangu, mtunza misingi mwenzangu. Ningekuwa na nauli ningesafiri nikuzike huko Cuba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles