MOMBASA, KENYA
KIONGOZI wa Chama cha ODM, Raila Odinga juzi alitetea makubaliano yake na Rais Uhuru Kenyatta, akisema hayamaamishi kumwondoa Naibu Rais William Ruto kutoka Chama tawala cha Jubilee.
Makubaliano yake na Rais Uhuru, alisema yalilenga kuzuia mmeguko wa taifa kufuatia uchaguzi wenye utata wa mwaka 2017, ambao ulisababisha aapishwe kuwa ‘rais wa watu’.
“Tungeendelea katika njia ngumu, lakini tulifikiria kwanza Ukenya wetu na kuamua kushikamana na Rais. Kuna wale wanaosema Raila anataka kuisambaratisha Jubilee na kufukuza watu. Huo ni upuuzi. Tunataka mabadiliko kwa nchi kwa ajili ya manufaa yetu wote,” alieleza Raila.
Wanasiasa wa kambi ya Ruto wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu kitendo cha Raila kushikama mikono na Rais Uhuru.
Wanadai mpango huo pamoja na mambo mengine umelenga kufanya mabadiliko ya katiba, ambayo yatamzuia Ruto kumrithi Uhuru.
Ruto pia katika matukio tofauti alionya kwamba Raila anaweza kumfuata na kumtosa kama alivyofanya ODM.
Hata hivyo Odinga alisema kushikana mikono kumeeleweka vibaya na kuchanganywa na suala la urais 2022.
“Watu walikuwa na hasira na walichoona ni giza tu. Rais alisema tunapaswa kuzungumza. Tulikubaliana kukomesha mapigano na kushughulikia vitu halisi vinavyochochea chuki miongoni mwa Wakenya na umasikini,” alisema Raila.
Alisema kwamba ni mapema mno na aibu kuanza kampeni kwa uchaguzi wa mwaka 2022.
Aliumwagia sifa mradi wa upanuzi wa Bandari ya Mombasa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi kuwa utatengeneza ajira zaidi kwa wakazi wa Pwani.
Raila ambaye juzi alifikisha umri wa miaka 74, alizungumza mjini hapa mbele ya Rais Uhuru, ambaye alizindua miradi mbalimbali.
Viongozi wengine waliokuwepo ni Waziri wa Utalii, Najib Balala na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho. Hata hivyo, viongozi wa Pwani walio kambi ya Ruto walisusa kuhudhuria tukio hilo.
Ukaribu baina ya Joho, Rais Uhuru na Raila ulionekana wazi wakati wakifanyiana utani huku gavana akimuita mkuu huyi wa nchi ‘bosi wetu’.