23 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

PWANI YACHOMOZA KIVIWANDA

Rais Magufuli (wa pili kulia) akiwa na mmiliki wa kiwanda hicho Said Salim Bakhresa wakati wa ufunguzi wa kiwandahicho cha Azam Product Group Mwandege Mkulanga
Rais Magufuli (wa pili kulia) akiwa na mmiliki wa kiwanda hicho Said Salim Bakhresa wakati wa ufunguzi wa kiwandahicho cha Azam Product Group Mwandege Mkulanga.

Na Shermarx Ngahemera,

VIWANDA ni shughuli pevu na si kugeza kama tamthilia kwani ni utamaduni  wa kuzalisha bidhaa kwa kurudia rudia kwa wingi kwa kutumia mashine na watu kutoka rasilimali na mazao.

Ni mapinduzi ya uzalishaji mali kwa wingi kwa kuongeza thamani na upatikanaji wa bidhaa mpya au kutumia teknolojia kuunda vitu vipya kwa matumizi ya ziada na mashambani, kukiwa na nia ya kuongeza kipato na kiwango cha uzalishaji kwa kutumia mashine.

Tanzania ya Viwanda  ya Rais John Magufuli inawezekana na imeshaanza kushamiri katika Mkoa wa Pwani kwa matamko ya viongozi wa juu wa  Serikali na kuzingatia kile kinachotokea na kufanyika katika mkoa huo. Mambo makubwa yanafanyika karibu katika kila wilaya ya mkoa huo kwa kuanzisha viwanda vya haja kote huko na inatia moyo.

Watu wanasema mwanzo wa ngoma ni lele na hivyo basi mbio za viwanda vikubwa zimeanza kwa kujengwa mkoani Pwani kwa juhudi na maarifa ya Waziri wa Viwanda, Biashara  na Uwekezaji Charles Mwijage.

Mkoa wa Pwani wenye sifa ya umasikini uliobobea kwa kuwa uwani kwa Dar es Salaam na watu wake kudharau na kutopenda elimu, umetoa meli ngamani ambapo yote haya karibu yatakuwa historia na yenyewe kung’ara na kutukuka kama mkoa.

Pwani ya leo si ile ya jana kwani kuna mambo mengi yanafanyika na hivyo  kuhitimisha ule usemi kuwa kaa karibu ya waridi unukie.

Uwekezaji mkubwa umeanza kufanyika kimyakimya na watu binafsi mkoani Pwani na hivyo umma hushtukizwa na uzinduzi na si uwekaji jiwe la msingi kwani ni utamaduni mpya. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amedai bayana kuwa masuala ya viwanda katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na  Tanga  yatakuwa chini yake na amekwenda mbali zaidi kwa kuwagawia wawekezaji ardhi bure na kuwaagiza makatibu wakuu wake na wakurugenzi kugawana mikoa iliyobaki katika zoni nane za utendaji kama ilivyopangwa na wizara yake.

Uchunguzi wangu utaenda ndani zaidi kwenye Mkoa huo wa Pwani ambao ulishika mkia kwenye viwanda na sasa unaanza kuongoza katika viwanda vikubwa na vya aina mbalimbali.

Uwekezaji wa mabilioni umeanzishwa mkoani humo, mwingi ukiwa ni ule wa kuongeza thamani. Ni kweli, mapinduzi yakitokea walio nyuma huwa mbele na kinyume chake na hicho ndicho kilichotokea katika Mkoa huo wa Pwani.

Kiluwa Steel Group ni kiwanda kilichopo Mlandizi ambacho ni cha aina yake kwani kina urefu wa kilomita 1.5 na upana wa mita 300 na hivyo kukitembelea unahitaji uwe kwenye gari au kiberenge. Kimejengewa na TRL mkono wa reli (siding) wa kilometa tano wenye thamani ya Sh milioni 863 na kitatengeneza chuma na jasi zaidi ya tani milioni moja na nyingi itauzwa nje ya nchi na kuajiri watu 200. Dhana ya uwekezaji ya Ubia wa Umma na Binafsi (PPP) imetumika vilivyo.

Aliyechokoza kasi ya viwanda mkoani Pwani awamu hii ya Serikali ni Azam Products, mali ya mfanyabiashara mashuhuri wa vyakula nchini, Salim Said Bakhresa wa S&S Enterprises Ltd ambaye amewekeza sawasawa kule Mwandege (Mkuranga); ameanza na kiwanda cha kutengeneza juisi ya matunda na hupokea mzigo toka sehemu mbalimbali nchi nzima.

Kiumbo Mkoa  wa Pwani uko kama kiatu cha farasi na hivyo umeuzingira Mkoa wa Dar es Salaam na una wilaya sita zikiwamo Bagamoyo, Kibaha, Chalinze, Rufiji, Mafia na Mkuranga.

Kwa maelezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa kule Mlandizi ni kuwa Dar es Salaam eneo lake limejaa wakazi na hivyo hupumulia Mkoa wa Pwani kwa maendeleo ya viwanda na shughuli nyingine za uchumi.

Kile kilichoitwa awali kuwa ni uwani  na kufifisha maendeleo sasa ni barazani na kuna fursa kubwa.

Waziri Mkuu anasema Serikali imetwaa ardhi ya ukubwa wa hekta 14,000 mkoani Pwani, ili zipimwe na kugaiwa kwa ajili ya viwanda, makazi na uwekezaji na kuagiza wabadilike tabia na kuacha ubabaishaji wa mambo. Umeme wa msongo mkubwa umepelekwa mkoani humo kwenye Kiwanda cha Chuma cha Pua cha Kiluwa Steel Group pale Mlandizi na miundombinu imeboreshwa kukaribisha ujaji wa viwanda maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akielezea kwenye shughuli ya kuzindua umeme wa Uhakika Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba, alithibitisha kuwa kazi ya kufikisha umeme kama alivyoagiza Rais John Magufuli  wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Azam kuwa imebakia asilimia 13 tu na Desemba utakuwa umekamilika kote na hivyo kusisimua maendeleo ya viwanda mkoani Pwani.

Waziri Mkuu naye alirudia kauli hiyo alipofika Mlandizi mara ya pili.

Nao ugunduzi wa gesi asilia nyingi na mafuta Mkuranga umebadilisha sura ya uchumi wa mkoa huo na kuonekana kwa siku za usoni itakuwa tegemeo la nchi. Vile vile zao lake la korosho limeanza kupanda chati kwani mwaka huu limeongoza kwa bei na kufikia Sh 3700 kwa kilo baada ya kufuta kodi zote za karaha kwa mkulima.

Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons &Power Tanzania ya Falme za Kiarabu (UAE) imegundua gesi nyingi kiasi cha futi za ujazo trilioni 2.17 ambayo iko Mkoa wa Pwani nchi kavu kilomita 30 Magharibi ya Dar es Salaam na hivyo inachagiza uwekezaji katika mkoa huo.

Gesi nyingi ya Tanzania iko baharini Lindi na Mtwara zaidi ya kilomita 100 toka nchi kavu na hivyo hiyo ya Pwani kuwa machimbo ya karibu kabisa na Soko kuu la Dar es Salaam.

Dodsal wana imani ya kupata gesi nyingi zaidi katika visima vingine vitatu inavyochimba katika eneo hilo linaloitwa Ruvu Block.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dodsal,  Pilavulathill Surendran, anaelezea ugunduzi huo kuwa una thamani ya kito na hivyo kampuni yake itaongeza uwekezaji wa  ziada  wa dola  milioni 50 kwa mwaka mmoja zaidi.

Kiwanda cha magari na trekta

Serikali ya Tanzania ilipata mkopo kutoka Serikali ya Poland wa dola milioni 100 na kupanga kutumia pesa hizo kujenga kiwanda cha kuunganisha matrekta pale Kibaha Maili Moja wilayani Kibaha kwenye karakana iliyokuwa  zamani ya Scania. Eneo hilo  pia litajengwa maghala ya kutunzia  mazao ya vyakula, matrekta madogo ya mkono (power tillers) yataunganishwa hapo na magari ya zimamoto.

Alipoonana na wawekezaji kutoka Poland, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adrehelm Meru, alisema Serikali imeazimia kuwa na uchumi wa viwanda  na hivyo kuwakaribisha kwa  mikono miwili.

Wawekezaji  kutoka nje hupata matatizo ya ardhi ya kufanyia kazi na Serikali ya awamu hii imefuta kadhia hiyo kwa kuingilia mara kwa mara uzembe wa halmashauri husika. Waziri Mwijage amempatia bure ekari 50 za ardhi Mkurugenzi wa Elven Agri Ltd, Darpan Pandolin, ajenge kiwanda cha ukaushaji na usindikaji matunda.

Mwijage amechukua uamuzi huo baada ya kumuuliza mkurugenzi huyo iwapo yupo tayari kujenga kiwanda kingine katika eneo ambalo linalimwa zaidi mananasi, machungwa na maembe ili kukuza soko la wakulima na ajira.

Kwa sasa kiwanda hicho kinachoendelea na ujenzi kilichopo eneo la Mapinga mkoani Pwani kitakapokamilika Januari mwakani, kitakausha tani nne za matunda kwa siku na kusafirisha nje ya nchi.

Mwijage amechukua uamuzi huo ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu Rais John Magufuli ampatie bure ekari 10,000 mfanyabiashara maarufu nchini, Abubakar Bakhresa, wakati akizindua kiwanda cha Bakhresa Products Limited pale Mkuranga.

Alisema mwekezaji yeyote kutoka ndani na nje ya nchi aliye tayari kwa ujenzi na uwekezaji wa viwanda, apatiwe ardhi mara moja, badala ya kuwasubiri baadhi ya watu wanaohodhi ardhi kubwa bila kuiendeleza.

“Rais alitoa ardhi yenye ukubwa wa ekari 15,000 mkoani Pwani zitakazotumika kwa shughuli hizo za uwekezaji, ujenzi wa viwanda. Nasema aliye tayari kwa shughuli za maendeleo apewe asizungushwe,” alisema Waziri Mwijage.

Kukamilika kwa viwanda vinne vinavyojengwa mkoani Pwani mwanzoni mwa mwaka ujao 2017, vitatoa ajira kwa zaidi ya watu 700.

Viwanda hivyo ni vya uunganishaji matrekta, kuzalisha kemikali za viuadudu  na usindikaji wa matunda.

Anasema wakurugenzi, makatibu wakuu watazunguka nchi nzima kusukuma kasi ya ujenzi na kuahidi kuwa ifikapo Desemba 15, mwaka huu kutatolewa ripoti ya ujenzi wa viwanda ulipofikia.

Kiwanda cha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa kueneza malaria kilichopo wilayani Kibaha ni cha kipekee barani Afrika na kimeshaanza kuuza bidhaa zake kwa Senegal ambao wamenunua zaidi ya lita 100,000.

“Kiwanda hicho kitazalisha kemikali zitakazomwagwa katika mazingira na hivyo mbu kutoweka kwani kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 12,000 za dawa hiyo kwa siku,” alisema Waziri na kuongeza kuwa, alikabidhi eka 300 bure kwa mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kipya cha aina hiyo.

Halmashauri ya Chalinze haiko nyuma kiviwanda kwani kiwanda cha kusindika juisi cha Sayona kinachojengwa katika Kijiji cha Mboga, Kata ya Msoga, Wilaya ya Bagamoyo kinatarajiwa kukamilika Machi mwakani, kitakapoanza kazi kitasindika nyanya, machungwa, maembe na mananasi.

Kuna Kamal Steel pale Kerege wilayani Bagamoyo ambacho huzalisha chuma cha pua tani 80,000 kwa mwaka na bado kinaendelea kupanuliwa.

Kule Mkuranga kuna kiwanda cha Wachina cha kauri cha Afrika Goodwill Ceramics ambacho uwezo wa kiwanda ni tani 1,200,000 lakini nchi inahitaji tani 500,000 tu na hivyo vigae vingi vitauzwa nje na kupata fedha za kigeni.

Kiwanda hicho karibu kitaanza kufanya kazi baada ya umeme wa uhakika kufika huko. Anaelezea kuwa kiwanda cha kutengeneza vigae na kile cha ‘gypsum’ kinategemewa  kuzalisha ajira 4,500 kwa Watanzania.

Kampuni ya mzalendo Mohamed Dewji inayoitwa Mohamed Enterprises Limited (MeTL), Mkurugenzi wake alimwona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  na kumweleza kusudio lake la kuanzisha kiwanda cha sukari wilayani Rufiji mkoani Pwani, cha kutengeneza tani 120,000 kwa mwaka. Serikali imekubali na kiwanda hicho kiko njiani kwani ardhi imeshapatikana kule Utete na Ikwiriri.

Bilionea Mohamed Dewji anasema kiwanda hicho kitatumia miwa tani milioni moja na laki mbili kutengeneza sukari zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka. Dewji alitumia fursa hiyo kukanusha habari zilizokuwa zimezagaa wakati huo na kusema kuwa yeye hana mipango ya kuhamisha vitegauchumi vyake na mitaji.

“Hizo ni porojo za mitaani kwani badala ya kuondoka, sisi tunaongeza na kuzidisha kuwekeza nchini mwetu. Nimefufua kiwanda  cha mafuta ya pamba kule Chato, Mkoa wa Geita na kufufua kiwanda cha nguo  kule Musoma,” alisema Dewji.

Viongozi wako imara

Rais, makamu wa rais na waziri mwenye dhamana ya viwanda wote wako imara kufuatilia na kuhakikisha ndoto ya viwanda inafanya kazi kwa kufuatilia utekelezaji kwa karibu mkoani Pwani.

 Waziri Mkuu ametoa agizo kwa Halmashauri ya Kibaha Vijijini Novemba 19, mwaka huu wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani, mara baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani Pwani, kuwa wapime na kutenga maeneo ya makazi na viwanda au uwekezaji.

“Jiji la Dar es Salaam limejaa na Kibaha mjini pia hawana ardhi ya kutosha, kimbilio pekee hivi sasa ni Kibaha Vijijini. Baraza la Madiwani fanyeni maamuzi, pimeni ardhi na mtenge maeneo ya makazi, viwanda na taasisi za elimu ili mkipata wawekezaji iwe rahisi kuwapa maeneo,” anasema.

Anasema  maeneo mengi nchini yanahitaji magari ya zimamoto lakini halmashauri nyingi  zilikuwa  zinashindwa kumudu bei za magari hayo.

“Viwanja vya ndege, bandari, taasisi zilizo chini ya Tamisemi kama vile shule za sekondari za bweni, majiji, miji mikuu, manispaa na halmashauri za wilaya, ni baadhi ya maeneo nyeti yanyohitaji huduma za zimamoto.

“Kupitia kiwanda hiki, matrekta mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu,” aliongeza kusema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini, alimweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenye hatua ya kufunga mitambo ambayo iko njiani toka India.

Kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000 kwa mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya nchi.

Mangazini amelenga kuzalisha vipuri hapa nchini kwa asilimia 60,  ili umiliki wa magari haya na matrekta utakuwa ni wa Tanzania na si wa kampuni za nje tena na hivyo kuweza kuhamisha teknolojia na uzalishaji utaanza Machi  mwakani.

Mangazini anasema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika, cha kwanza kikiwa huko Bassa, Afrika Kusini na umiliki wa Kiwanda cha Equator SUMA JKT Ltd ni kati ya Equator Automech Ltd kwa asilimia 70 na SUMA JKT asilimia 30 ya  hisa za kiwanda chenye gharama ya Sh bilioni mbili .

“Kiwanda hicho mbali na magari ya zimamoto na matrekta, wataweza pia kuunganisha mabasi na zana za kilimo kama vile combine harvesters. Na hivyo kufanikiwa kuhamisha teknolojia kutoka Russia (magari ya zimamoto) na India na Poland (matrekta) na kuna uhakika wa soko hapa nchini katika Jumuiya za EAC na SADC,” anasema Mangazini,

Ni kweli hakuna masika yasiyo na mbu kwani watu wengine wanadai fidia.

Kuhusu fidia kwa wananchi na Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mkuu wa  Mkoa, Evarist Ndikilo, anasema  zinadaiwa Sh milioni 403, zikiwa za wananchi waliopisha njia wakidai fidia ya Sh milioni 95.76 na Halmashauri inadai Sh  milioni 307.26.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa, anasema shirika hilo limetumia Sh milioni 863 kukamilisha ujenzi wa reli ya kilomita 5 kutoka njia panda hadi kwenye kiwanda hicho ambapo kati ya hizo km.1.5 zimo ndani ya kiwanda

“Hadi sasa tumeshaweka njia nne za reli, moja ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe.

“Tumetumia fedha kidogo kwa sababu tumetumia mafundi wetu badala ya wakandarasi,” ameongeza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiluwa Steel Group, Mohammed Kiluwa, alimweleza Waziri Mkuu kuwa anatarajia kuanza uzalishaji Januari mwakani na kwamba ataajiri wafanyakazi wapatao 200.

“Tunataraji kuanza uzalishaji Januari  mwakani na uzalishaji utakuwa tani 2,000 kwa siku. Ila tumekubaliana na wawekezaji wenzangu tuweke pia viwanda vingine vitatu kwa sababu tunatarajia kufungua viwanda vinne vya kutengeneza jasi (gypsum powder), pikipiki, nguzo na vifaa vya kufungia nyaya za umeme mkubwa pamoja na karatasi za maliwato (tissue paper).”

Kwingineko

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Clifford Tandari, akiongea na MTANZANIA,  alisema  Kampuni ya China ya Hengya Cement itajenga kiwanda Tanga ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote nchini.

“Kiwanda kitazalisha ajira zaidi ya 10,000  kikiwa kiwanda kikubwa barani Afrika na kitawekeza kiasi cha dola bilioni 2.5,” anasema Tandari.

Huu ukiwa ni uwekezaji wa zaidi ya mara tano ya Dangote Cement ya Mtwara.

Pwani imezinduka na sasa ni kiboko ya njia ya viwanda vipya; Kwani kawia ufike .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles